in , , ,

Tumekuwa Sio Wachambuzi Tena Ni Machawa wa Timu

Katika ulimwengu wa soka, hasa katika nchi za kiafrika kama Tanzania, tumeshuhudia ongezeko kubwa la watu wanaojitokeza kama wachambuzi wa mpira wa miguu. Sote tunakubaliana kuwa mpira wa miguu unavutia wengi, ndiyo maana baadhi hujitokeza kudhamini, kujiunga uanachama, kununua jezi na vitu mbalimbali kuhusu timu yao. Lakini pia mpira wa miguu unahitaji uvumilivu katika kupata matokeo, kwahiyo si kila mmoja anayeingia kwenye mchezo huu anaelewa au anafahamu mambo ya msingi na maendeleo yake.

Hivyo hivyo kwa wachambuzi si kila mmoja anaelewa mambo ya msingi, mipaka, mbinu, na ufundi wa kuchambua mchezo wenyewe na wahusika wake kama vile makocha,wachezaji na wataalamu wengine.

Kwenye suala la uchambuzi ndipo mahali ambako washabiki wanategemea kuhabarishwa, kufahamishwa, kufafanuliwa na zaidi kupewa mambo ya msingi katika mchezo wenyewe.

Tanzania Sports
Nikichambua soka, kupitia Dira ya Dunia, ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London

Hata hivyo, ukweli mchungu ni kwamba wengi wa hawa wanaojitambulisha kama wachambuzi hawana uelewa wa kina kuhusu mchezo huu na badala yake wamegeuka kuwa wapiga kelele na machawa wa timu fulani. Hali huyo inashusha viwango vya mijadala mipana kuhusiana na soka.

Nimepata bahati kubwa maishani ya kuwahi kuwa mchambuzi wa michezo kupitia Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC. Pia kuwa mchambuzi wa kwanza kuchambua ‘Live’ fainali za Kombe la Dunia, Afrika Kusini 2010, mtangazaji akiwa Charles Hilary. Katika kukupa kumbukumbu tu, fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 zilifanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika.

Tanzania Sports
Miaka hiyo nikiwa mchambuzi wa michezo kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London.

Tuseme zilikuwa fainali za Kiafrika na kwa ajili ya Waafrika wote. Wakati CAF ikiwa imepokea rekodi ya mwanachama wake wa kwanza kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 maana yake nami nilikuwa miongoni mwa wachambuzi wa kwanza kuchambua na kuwapa burudani wapenzi wa kandanda barani Afrika.

Ifahamike BBC husikilizwa na takribani watu Milioni 60  wanaozungumza lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki yote na Nchi za Maziwa Makuu, hivyo mchango wangu kama mchambuzi umekuwa Mkubwa na umewafikia ambao wamenufaika kwa elimu ya michezo.

Baada ya kusema hayo, sasa nije kwenye hoja ya misingi ya uchambuzi. Unapokuwa mchambuzi wa mpira wa miguu inahusu wachezaji, kwahiyo unatakiwa kuelewa karibu Kila kitu muhimu kuhusiana nao. Nitatoa mifano ifuatayo ili kuwajengea uwezo wachambuzi na kuelewa dhima yake.

1. Takwimu za mchezaji na timu;– Huu ni wajibu wa msingi sana katika kukamilisha kazi hii. Ni muhimu kufuatilia kiwango cha wachezaji na mwenendo wa timu nzima; uwezo wao, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, mchango wake na hata washirika wake wa kukamilisha ubora. Safu ya ulinzi, viungo wa ulinzi , viungo washambuliaji, mawinga na washambuliaji.

2. Mbinu za kiufundi – Kuelewa na kuelezea mbinu zinazotumiwa na makocha katika mchezo.  Mpira unahusu mifumo, lazima uelewe aina ya mifumo inauotumika; mfano Kuna makocha wanapenda mifumo fulani ambayo inawafaa wachezaji. Lakini pia wapo wachezaji wanaoonesha ubora wao katika mfumo fulani. Mfano 3-4-3 au 4-4-2, 4-5-1, 3-5-2, 4-1-3-1-1 na kadhalika. Msikilizaji, mtazamaji au msomaji anatarajia Mchambuzi utaeleza sababu za mchezaji Fulani kumudu au kutomudu mfumo fulani au kwanini umefanikiwa kiasi fulani katika uwajibikaji.

Tanzania Sports
Nikichambua Fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini, sambamba na Mtangazaji Nguli, Charles Hilary

3. Uchambuzi wa mabadiliko – Kutafsiri uamuzi wa mabadiliko ya wachezaji na athari zake kwenye mchezo. Hapa lazima uelewe kocha amebadili mchezaji wake kwa ajili ya kuimarisha timu lakini huenda ikawa kinyume chake. Mchambuzi lazima utafsiri aina ya mabadiliko hayo na matokeo chanya au hasi yanayotokea. Maana unatakiwa kujua mabadiliko yoyote yamefuata mbinu mpya au ileile. Unatakiwa kufahamu vizuri mwenendo wa kimbinu unatokana na mabadiliko ya makocha.

Maswali yanayopaswa kuuliza kabla hujafanya uchambuzi;

1. Uchambuzi wako unamsaidia msikilizaji kwa kiasi gani?
2. Je unaweza kutumia takwimu kutafsiri mwendo wa timu au mchezaji?
3. Je takwimu zina umuhimu gani katika mafanikio ya kocha au timu na nini maana yake ili msikilizaji au mtazamaji au msomaji aelewe?
4. Je katika uchambuzi huo unatumia lugha gani? Je lugha yako inamfundisha msikilizaji, mtazamaji au msomaji ama ni Ile isiyo na mwelekeo?
5. Je sifa yako iwe uchambuzi au shabiki wa mrengo fulani wa mpira miguu?
6. Je, unaweza kudhibiti mapenzi yako kwa timu Kisha ukachambua kwa haki?
7. Kipi muhimu mapenzi yako au kazi yako ya uchambuzi kwa ajili ya wasomaji, wasilikiliza au watazamaji wa Televisheni?

Baada ya kusema hayo, kwa bahati mbaya, wachambuzi wengi wa kisasa wameacha vigezo hivi muhimu sana katika mpira wa miguu.

Siwezi kusema wachambuzi wote lakini kwa sasa hali imezidi na naona kabisa vipindi vingi vya redio na hata vya Televisheni vimegeuka vijiwe vya kuchambua kihisia zaidi na kuonesha kwa namna gani mtu anakuwa kwenye mrengo fulani wa timu au kama tunavyosema kuwa hao ni bendera fuata upepo.

Wachambuzi badala ya kufafanua mbinu za mchezo, wamejikita zaidi katika kushabikia timu wanazozipenda au kushambulia timu pinzani, na kuharibu kabisa dhana ya uchambuzi wa mpira wa miguu.

Katika muktadha wa sasa, ukiwa katika vijiwe mbalimbali vya soka utakuta kuwa wengi sasa wametolewa katika ile hali ya kuonekana wachambuzi na wapo baadhi ya mashabiki wa soka wanadiriki kusema kuwa wamekuwa ni wapiga kelele na machawa wa timu ambao wameamua kuvaa uhusika wa uchambuzi wa soka.

Na haya yote husababisha kukosekana kwa utulivu kwenye timu na kuwepo kwa migogoro kwani wachambuzi wanapokuwa wanaingia katika mrengo huo ndiyo wale ambao sasa badala ya kutoa uchambuzi wa kina wanakuwa wanachochea malumbano yasiyo na tija kati ya mashabiki wa timu mbalimbali.

Wachambuzi wengi wa sasa wamekuwa sasa wakiingia katika lile dimbwi la kutumia mitandao yao ya kijamii kwa kueneza taarifa zisizo sahihi kuhusu wachezaji, makocha, na hata viongozi wa timu mambo amabyo wakati mwingine tunakua tunasema kuwa tunatoka kwenye ile dhana halisi ya uchambuzi wa soka na kuwa tuko kwenye udaku wa Habari za Soka.

Wanapokuwa wengi wanaojihusisha na uchambuzi bila maarifa, wachambuzi halisi wanapoteza nafasi na heshima yao.

Mashabiki wanashindwa kutofautisha kati ya mtaalamu na mshabiki wa kawaida jambo ambalo sasa badala ya kusaidia kuboresha mchezo kupitia uchambuzi wa kina, mjadala wa soka umekuwa wa kishabiki. Hii inawafanya hata wachezaji na makocha kushindwa kupata maoni yenye tija ya kuimarisha viwango vyao.

Tanzania Sports
Nikiwa na Aliyekuwa mtangazaji wa BBC, Yusuph Dayo, Nikichambua Ligi Kuu ya England, kupitia Dira Ya Dunia TV.

Tabia ya kupendelea timu fulani katika uchambuzi husababisha mashabiki kushindana na kuendeleza chuki badala ya kuhamasisha mshikamano katika soka.

Katika kukabiliana na changamoto ya wachambuzi uchwara ni muhimu kuzingatia mambo ya misingi ya uchambuzi wa soka kama ifuatavyo;-

1. Elimu na Mafunzo: Wachambuzi wapate mafunzo ya kitaalamu kuhusu uchambuzi wa soka.

2. Utaalamu Huru: Vyombo vya habari vihakikishe kwamba wachambuzi wanazingatia weledi badala ya mapenzi ya timu.

3. Majukwaa ya Kitaalamu: Kuanzisha vipindi vya mijadala ya soka vinavyoongozwa na wataalamu wenye ujuzi wa mchezo huo.

Kama una ndoto za kuwa mchambuzi wa soka basi unatakiwa kufahamu kuwa uchambuzi wa soka ni sanaa inayohitaji weledi na uelewa wa kina. Wakati umefika kwa wachambuzi wa soka kujitathmini na kuhakikisha wanatumikia kazi hii kwa uaminifu na uwazi. Wapiga kelele na machawa wa timu wanapaswa kujifunza na kuacha kutumia majukwaa yao kueneza ushabiki, bali kuchangia katika kuendeleza mchezo wa soka nchini Tanzania.

Dondoo muhimu za kuwa mchambuzi wa michezo:

– Kuwa mwenyewe/Usijifanye kuwa mtu asiye wewe
– Unapofanya uchambuzi, uhalisia wako ndiyo unaoonekana
– Shauku na mapenzi yako ya michezo yanatakiwa yaonekana katika uchambuzi wako
– Fanya maandalizi na hakikisha unakijua unachokiongea
– Jenga mahusiano mazuri na watu walio katika tasnia ya michezo
– Weka umakini katika kutimiza malengo yako
– Achana na mazoea, thubutu kujifunza/kujua zaidi
– Jifunze ustadi wa mawasiliano – kuwa na uwezo wa kusikiliza, kuchambua taarifa, kupokea mrejesho na kuutmia huo mrejesho ipasavyo
– Usikate tamaa! Kutakuwa na nyakati za mafanikio na nyakati za changamoto, lakini kwakuwa unafanya unachokipenda, usikiache!

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

52 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Siri ya Yanga kufungwa Ligi Kuu hii hapa

Tanzania Sports

Taifa Stars katika rekodi muhimu