in , , ,

Siri ya Yanga kufungwa Ligi Kuu hii hapa

UKIIFUNGA timu nyingine lazima nawe utafungwa. Unapopata ushindi ugenini nawe unaweza kupoteza pointi kwenye uwanja wako wa nyumbani. Wakati unashangilia kushinda katika mashindano makubwa mfano Ligi ya Mabingwa Afrika au labda Ulaya kwenye uwanja wa ugenini lazima utambue unaweza kufungwa katika mechi ya marudiano au katika mchezo wa uwanja wako wa nyumbani. 

Uchunguzi wa TANZANIASPORTS unaonesha kuwa ushindi wa timu unapatikana katika viwanja viwili; ugenini ua nyumbani. Ndiyo maana Wabrazil bado wanalia na jinamizi la ‘Maracanazo’ baada ya kushuhidia wakipigwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia ndani yua dimba lao la Maracana na kushuhudia kombe likisafiri kwenda Uruguay. Huo ulikuwa mchezo wa fainali, lakini hata katika mechi za Ligi Kuu au mashindano yoyote, timu zinaweza kukutana na vipigo vya kushangaza.

Kwa mfano, Simba waliwahi kuwafunga Jwaneng Galaxy ya Botswana wakiwa ugenini. Ulikuwa ushindi uliowasisimua mashabiki na wadau wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa. Simba walishinda ugenini, nao Jwaneng Galaxy wakaja kwenye dimba la Benjamin Mkapa wakaibuka na ushindi wa mabao 4. Yanga walikubali kipigo cha bao 2-1 kwenye mchezo wa fainali ya kwanza ya Kombe la shirikisho kwenye dimba la Benjamin Mkapa, lakini wakaibuka ushindi wa bao 1-0 ugenini ambao haukuweza kuwapatia kombe hilo. 

Yanga vilevile waliwafunga TP Mazembe kwenye dimba la Benjamin Mkapa, kisha wakaibuka na ushindi kwenye uwanja wa ugenini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hii ina maana kuwa Yanga walikuwa imara na ubora ambao uliwatetemesha TP Mazembe. Ushindi wowote ambao timu inaupata kwenye uwanja wa ugenini unapaswa kutafsiriwa kuwa hata kwenye uwanja wao wa nyumba mgeni anaweza kushinda. 

Yanga ya Jijini Dar Es Salaam ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania na wawakilishi wetu katika Ligi ya Mabingwa hivyo wanalo jukumu la kupeperusha bendera ya Tanzania. Hata hivyo kwenye Ligi Kuu Yanga wamepoteza mechi mbili wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, Azam Complex. Walianza kwa kufungwa na Azam FC kwa bao 1-0 kisha wakala kichapo cha mabao 3-1 toka kwa Tabora United. Kipigo cha Yanga kimezua gumzo na kusababisha kibarua cha kocha wao Miguyel Gamondi kuota mbawa. 

Ndiyo, kocha wao ametimuliwa katika kikosi cha Yanga kwa sababu wamefungwa mechi mbili mfululizo. Pengine mashabiki wanafahamu sababu ni kufungwa mechi hizo pekee, lakini sababu za ndani zinaelezwa kuwa uongozi wa Yanga umekwazwa na maendeleo ya wachezaji binafsi, uwiano wa kucheza kati ya wanaokaa benchi na wanaoanza kikosi cha kwanza, pamoja na misimamo baina ya pande hizo mbili. Tukiachana na uamuzi wa Yanga kumtimua Miguel Gamondi, tueleze sababu za timu hiyo kuteleza.

Wageni wenye viwango viwanjani

Kama kuna sababu ambayo inasababisha timu vigogo zifungwe basai ni ujio  wa wachezaji wa kigeni. Wachezaji nao wameimarisha timu nyingine ambazo hazipewi nafasi ya kutwaa ubingwa wala kuwakilisha katika mashindano ya kimataifa. Misimu kadhaa iliyopita, Biashjara United ya mkoani Mara ilikuwa inawakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho na ilikuwa na wachezaji wa kigeni. Uwepo wa wachezaji hao uliwasaidia kuimarisha timu yao. Hali kadhalika katika timu mbalimbali za Ligi Kuu kama vile Namungo Fc ya Ruangwa mkoani Lindi, Singida Black Stars, Azam Fc, Coastal Union,Tabora United, Pamba Jiji au Dodoma Mji ni miongoni mwa timu ambazo zimeajiri wachezaji wa kigeni ambao wameleta ushindani. 

Tazama mfano wa hivi karibuni jina la Jonathan Sowah limetajwa kusajiliwa katika klabu Singida Black Stars. Nyota huyo alikuwa akikipiga katika klabu ya Al Nasr Benghazi ya Libya. Zamani ilikuwa rahisi kubashiri kuwa angejiunga na timu mbili kubwa; Yanga na Simba. Kama ingetajwa timu ya tatu basi ingekuwa Mtibwa Sugar. Katika nafasi ya Mtibwa Sugar kuna Azam Fc ambayo imesajili nyota kutoka Amerika kusini. Hii inakupa ujumbe kuwa uwezo wa wachezaji wa kigeni umekuwa chachu ya ushindani na ubora wa Ligi Kuu ya Tanzania.

Makocha wasaka fursa na viwango

Makocha wote wa kigeni wanapoajiriwa ni matokeo ya kusaka fursa. Kwa maana hiyo makocha hao wanaleta maarifa mapya na ya kisasa. Zamani ilikuwa rahisi kuona makocha wa kigeni wakitua Yanga na Simba, lakini timu ya tatu ilikuwa Mtibwa Sugar, na baadaye A zam FC nao wamekuwa wakiajiri walimu wa nje ili kujenga timu yao. 

Hata hivyo nafasi zimeongezeka kwenye timu mbalimbali ambapo baadhi ya wataalamu kama Wakurugenzi wa michezo, wachambuzi wa timu na makocha wamekuwa wa kigeni. Namungo, Tabora United, Kagera Sugar, Pamba Jiji, Dodoma Mji,Mbeya City,Coastal Union na nyinginezo zimewahi au zinaendelea kuwa na walimu wa kigeni. Walimu wa kigeni wanapokuja nchini maana yake ushindani wa Ligi unaongezeka, timu zinapata maarifa kuanzia uongozi,uchezaji na uendeshaji mzima wa mpira wa miguu. Kwa maan nyingine uwezo wa timu ndogo umeongezeka na kuwa tayari kushindana na timu kubwa. Walimu hawa wanalipwa vizuri na wanafurahia fursa yao ili kuzinoa timu za Ligi Kuu Bara. 

Hitimisho

Kwa vyovyote vile yaliyotajwa hapo juu yanachangia kushuhudia vipigo vya kushtusha kwenye mchezo wa soka.  Yanga ilizoea kushinda, lakini ilipokutana na mabadiliko ya kimbinu iliambulia kipigo kikali. Wachezaji na makocha wa kigeni wamekuja kuandaa vizuri sifa zao (CV) kwahiyo watafanya kila njia na kila mbinu kuhakikisha wanaziandaa timu zao kuibuka na ushindi. Ushindi ndiyo unawafanya waongeze thamani ya  sifa zao. Kwahiyo suala si la Yanga kufungwa mechi mbili kama vile wameonewa au hawatakiwi, bali ushindani wa Ligi ndiyo umewafikisha kwenye vipigo hivyo. Watu wamekuja Ligi ya nyumbani kuonesha uwezo wao na maarifa waliyonayo kwahiyo kushuhudia vipigo kwa vigogo lisiwe jambo la ajabu kama ilivyotokea kwa Yanga, labda hawajui siri hii hadi wameamua kufukuza benchi la ufundi ambalo limeiacha timu ikiwa nafasi nzuri tu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

55 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Je ni nani huyu kocha Sead Ramovic wa Yanga?

Tanzania Sports

Tumekuwa Sio Wachambuzi Tena Ni Machawa wa Timu