in , ,

Taifa Stars katika rekodi muhimu

HAKUNA lisilowezekana chini ya jua, ni msemo muhimu sana katika kusaka matumaini na ufanisi wa jambo. Wachezaji wa Taifa Stars wana kila sababu ya kuandika rekodi tatu muhimu wakati ambao wanakutana na miamba ya Afrika magharibi, Guinea kwenye mchezo wa mwisho  wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2025. Fainali za Kombe hilo zinatarajiwa kufanyika nchini Morocco. 

TANZANIASPORTS inakufahamisha masuala muhimu kuelekea mchezo wa Taifa Stars ambao utachezwa kwenye dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar Es Salaam huku kukiwa na shamrashamra nyingi kabla ya mchezo huo.

Rekodi ya mabao

Safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars inaingia katika mchezo huo ikiwa na kibarua cha kuvunja rekodi ya Mrisho Khalfan Ngassa. Katika kikosi cha sasa wachezaji wawili tegemeo ndiyo wanaweza kuvunja rekodi ya Mrisho Ngassa. Wachezaji ni Mbwana Samatta na Simon Msumva. Mrisho Ngassa ndiye mshambuliaji mwenye mabao mengi katika  kikosi cha Timu ya Taifa, akiwa amezifumania nyavu mara 25. 

Mchezaji wa pili anayefuatia kwa rekodi hiyo ni Simon Msuva ambaye amefunga mabao 23 na kubakiza mawili kufikia rekodi ya Ngassa. Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amepachika wavuni mabao 22 katika kikosi hicho hivyo analo deni la mabao matatu kufikia rekodi ya Mrisho Ngassa. Wachezaji hawa wawili wanao uwezekano wa kuvunja rekodi ya Ngassa ikiwa wataichapa Guinea ya Moussa Camara, golikipa wa Simba kisha kufuzu kwa Fainali za AFCON 2025.

Mechi nyingi Taifa Stars

Wakati Mrisho Ngassa akijivunia rekodi yake ya kupachika mabao mengi, anayo nyingine ya kucheza mechi zaidi. Ngassa amecheza mechi 100 akiwa Taifa Stars na kuwaacha mbali washindani wake kwenye rekodi ya kupachika mabao yaani Msuva na Samatta. Hata hivyo Mrisho Ngassa anazidiwa kwa mechi 7 zaidi na kiraka wa zamani Erasto Nyoni ambaye amecheza mechi 107 akiwa kikosi cha Taifa Stars. 

Nyoni ametumikia nafasi tofauti, beki wa kati, beki wa kulia, beki wa kushoto na kiungo mkabaji (ulinzi). Mchezaji wa tatu ni Kelvin Yondani ambaye amecheza mechi 97 katika kikosi cha timu ya Taifa. Kwahiyo Nyoni (107), Ngassa (100) na Kelvin Yondani (97) wana kila kitu cha kuwahamasisha wachezaji wa Taifa Stars kusaka rekodi hizi muhimu kwa kuishinda Guinea kisha kufuzu fainali za AFCON 2025.

Kufuzu mara ya tatu mfululizo

Kizazi kipya kina kila sababu ya kujivunia kwa rekodi yao ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mara mbili mtawalia. Lakini hilo litaonga zaidi endapo watafuzu kwa mara ya tatu na kudhihirisha kuwa wao ni baba lao. Kwa mara ya kwanza Tanzania ilifuzu Fainali za AFCON mwaka 1980, kisha wakafanya hivyo mwaka 2019 kabla ya kwenda tena kwenye fainali hizo mwaka 2023. Kwahiyo wanayo kila sababu ya kuweka rekodi mpya na muhimu kufuzu mara tatu mfululizo, yaani 2019, 2023 na mpya ya 2025. Hayo yatawezekana tu iwapo wataifunga Guinea katika mchezo wa mwisho.

Majirani wametangulia

Wakati Taifa Stars ikiwa nyumbani kwenye mchezo wa mwisho wa kundi lao kuwania kufuzu, majirani zao wametangulia Morocco baada ya kufanya vizuri katika mechi zao za mwisho. Uganda ambao ni mwanachama mwenza wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wao wamefuzu fainali hizo baada ya kuzikosa zile za mwaka 2023 zilizofanyika nchini Ivory Coast. 

Hali kadhalika mwanachama mwenza wa Tanzania katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Zambia wamefanikiwa kutinga katika Fainali hizo sambamba na mwenzao Afrika kusini. Tanzania ina uhusiano wa karibu nan chi hizo kwa sababu za kisiasa na kimichezo. Mastaa kadhaa wa Zambia na Uganda wanacheza soka katika vilabu vya Tanzania hususani Yanga na Simba. Zambia walifuzu kwa bao la Kennedy Musonda, wakati Khalid Aucho aliwaongoza Uganda kuandika rekodi yao mpya ya kinara wa kufuzu AFCON kwa ukanda wa Afrika Mashariki wakiungana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). DRC na Uganda ndiyo Mataifa yaliyofuzu mara nyingi zaidi kuliko mengine hapa Afrika Mashariki. 

Vita ya Makipa wa Simba

Golikipa namba moja wa klabu ya Simba ni Moussa Camara raia wa Guinea. Ndiye anayekaa langoni kwenye mchezo huu dhidi ya Taifa Stars. Katika mchezo huo atakabiliana na mastaa wenzake wa Simba, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein na Aishi Manula. Taifa Stars langoni itakuwa na golikipa namba mbili wa Simba, Aishi Manula. Kwa upande wao Guinea watakuwa na golikipa namba moja wa klabu ta Simba, Moussa Camara. Nani zaidi katika mchezo huo? Ni jambo la kusubiri na kuona. Kila la heri Taifa Stars, inawezekana kushinda.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

47 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Tumekuwa Sio Wachambuzi Tena Ni Machawa wa Timu

Taifa Stars

Hongera Tanzania Kufuzu AFCON, Mko Vizuri Sana