in , , ,

YANGA, AZAM ZAKABANA KOO

 

Mbabe hakuweza kupatikana ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam hii leo ambapo Yanga na Azam walitoshana nguvu kwa kutoka sare ya bao moja kwa moja kwenye mchezo uliokuwa wa kuvutia kupita kiasi hasa kwenye kipindi cha pili.

Yanga ndio waliotangulia kupata bao kupitia kwa Donald Ngoma katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza kabla ya Kipre Tchetche kuwasawazishia Azam kwenye dakika ya 81 na kuzifanya timu hizo kugawana alama kwenye mchezo huo.

Kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo timu hizo zilishambuliana kwa zamu lakini hakukuwa na mashambulizi makali. Washabiki walilazimika kusubiri mbaka dakika ya 45 ambapo mlinzi wa kulia wa Yanga Juma Abdul alipiga krosi safi iliyomkuta Donald Ngoma ambaye aliweka mpira kifuani na kufunga bao maridadi lililoiweka Yanga mbele wakati wa mapumziko.

Mshambuliaji huyo wa Yanga raia wa Zimbabwe alimjaribu tena mlinda mlango wa Azam Aishi Manula kwa shuti kali kwenye dakika ya 59. Safari hii golikipa huyo namba mbili wa timu ya taifa ya Tanzania alifanya kazi ya ziada na kuokoa mpira ule.

Dakika 10 baadae mwalimu wa Azam Stewart Hall akafanya mabadiliko kwa kumtoa ndani ya uwanja Allan Wanga na kumuingiza Kipre Tchetche. Mabadiliko haya yalionyesha kuwa na manufaa kwa upande wa Azam baada ya mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast kufunga bao la kusawazisha akimalizia kazi nzuri ya winga machachari Farid Mussa.

Advertisement
Advertisement

Dakika ya 84 ya mchezo ikamshuhudia mwamuzi Abdallah Kambuzi akiwazawadia Yanga penati iliyokuwa na utata baada ya Simon Msuva kuangushwa na Aishi Manula kwenye eneo la hatari. Golikipa huyo alionyeshwa kadi ya manjano lakini alitulia na kuokoa mkwaju wa penati uliopigwa na kiungo kutoka Zimbabwe Thabani Kamusoko.

Kwa matokeo haya timu hizi mbili zimeendeleza rekodi zao za kutopoteza mchezo kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu kila moja ikiwa imekusanya alama 16 kwenye michezo sita. Mabingwa watetezi Yanga wanaendelea kubaki kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya mabao na Azam wanabaki kwenye nafasi yao ya pili.

Kwenye mchezo mwingine uliopigwa ndani ya dimba la Sokoine jijini Mbeya Wekundu wa Msimbazi Simba walivunja mwiko kwa kuwapiga Mbeya City bao moja kwa sifuri.

Bao hilo lilifungwa na mlinzi Juuko Murshid raia wa Uganda mapema kwenye dakika ya 3 ya mchezo na kuiwezesha timu yake kupunguza tofauti ya alama walizokuwa wameachwa nyuma na watani wao wa jadi, Yanga. Sasa ni alama moja pekee inayowatenganisha Simba walio kwenye nafasi ya tatu na vinara wa ligi Yanga.

Simba sasa wana alama 15 sawa na Mtibwa Sugar ambao pia wamepata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Coastal Union ndani ya dimba la Mkwakwani jijini Tanga leo hii.

Matokeo mengine; Majimaji FC 1-0 African Sports, Ndanda FC 0-0 Toto Africans na Stand United 3-0 Prisons.

 

 

 

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

USHABIKI HUKU UNATAABIKA KUJENGA HIMAYA ZA WENYE MALI

Tanzania Sports

Manchester, Arsenal, Chelsea safi