*Brazil wabanwa na Mexico
*Urusi sare na Korea Kusini
Kikosi kikali cha Ubelgiji kimepambana na Algeria na kutoka nyuma kwa bao 1-0 hadi kushinda 2-1 katika fainali za Kombe la Dunia.
Algeria walitangulia kupata bao kwa penati ya Sofiane Feghouli aliyechezewa rafu na beki wa Tottenham, Jan Vertonghen.
Hata hivyo, Ubelgiji walipambana na kupata mabao kupitia kwa Marouane Fellaini na Dries Mertens na kujiweka pazuri katika Kundi H.
Fellaini anayechezea Manchester United alitokea benchi kipindi cha pili na alifunga kwa kichwa wakati Mertens alifunga dakika 10 kabla ya mechi kumalizika.
Mshambuliaji mahiri wa Chelsea, Romelu Lukaku alishindwa kabisa kung’ara ambapo alishambulia sambamba na Eden Hazard.
MEXICO WAWABANA BRAZIL
Wenyeji Brazil walibanwa na Mexico katika mechi ya pili ya Kundi A, ambapo sasa timu zote zimefikisha pointi nne kwani zilishinda mechi zao za kwanza.
Ukiachilia mbali mchezo mzuri wa Mexico, kikwazo kikubwa kwa Brazil kilikuwa kipa wa Mexico, Guillermo Ochoa aliyeokoa mabao kadhaa ya wazi.
Neymar na nahodha Thiago Silva walizuiwa na kipa huyo huku Jo aliyechukua nafasi ya. Fred akishindwa kujipanga vyema ili kufunga akiwa kwenye nafasi nzuri.
Kipa wa Brazi, Julio Cesar naye alikuwa vyema langoni mwake na aliokoa hatari kadhaa. Timu zote mbili zina fursa ya kushika nafasi ya kwanza kwenye kundi, Brazil wakiwa wamebakisha mechi dhidi ya Cameroon huku Mexico wakiwasubiri Croatia.
URUSI SARE NA KOREA KUSINI
Urusi wamekwenda sare ya 1-1 na Kora Kusini katika mechi ngumu ya Kundi H.
Korea walianza kupata bao kwa mkwaju wa mbali wa Lee Keun-ho uliombabatiza mikono kipa Igor Akinfeev na kuzama nyavuni.
Urusi wanaofundishwa na Fabio Capello walipigana kiume na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa Aleksandr Kerzhakov.
Mfungaji huyu anaungana na Vladimir Beschastnykh kama wafungaji wa mabao mengi zaidi katika historia ya Urusi, ambapo wamefikisha mabao 26.
Ubelgiji wanashika nafasi ya kwanza kwenye kundi hili wakifuatiwa na Korea na Urusi huku Algeria wakiwa na kazi ngumu.
Comments
Loading…