Jana shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, TFF limeachana na aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Ettiene Ndaragije. Ettiene Ndaragije aliiwezesha timu hiyo ya taifa kufika katika michuano ya CHAN.
Tukumbuke pia kabla ya Ettiene Ndaragije kuondolewa kwenye nafasi ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) pia mtangulizi wake Emmanuel Amunike mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria alifukuzwa.
Emmanuel Amunike alifukuzwa baada ya kufanikiwa kutupeleka kwenye michuano ya Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39. Mara ya kwanza Tanzania tulifanikiwa kufuzu mwaka 1980 na Emmanuel Amunike alitupeleka Afcon mwaka 2019.
Lakini baada ya michuano hiyo Emmanuel Amunike alifukuzwa ndani ya timu yetu. Kama ilivyo kwa Emmanuel Amunike, Etienne Ndaragije na yeye alifukuzwa baada ya michuano ya CHAN.
Tuanze kwa kujiuliza, tatizo liko wapi? Tatizo lipo kwa makocha au tatizo lipo kwa TFF? Ukiniuliza mimi hilo swali jibu pekee ambalo nitakupa ni kukuambia tatizo lipo kwa TFF.
Kwanini nasema tatizo lipo kwa TFF? Tuanzie kuitazama ligi kuu ya Tanzania bara. Tuachane na madudu ya waamuzi kwenye ligi kuu Tanzania na madudu mengine unayoyafahamu, turudi kutazama idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu.
Kanuni za ligi kuu Tanzania zinaruhusu timu kusajili wachezaji kumi wa kigeni. Tutazame timu kubwa ambazo ndizo huwa zinazalisha wachezaji wengi kwenye timu yetu ya taifa.
Ukizitazama timu kubwa asilimia kubwa ya wachezaji ambao wanapata nafasi ya kucheza ni wachezaji wa kigeni. Mfano Simba SC leo itacheza na As Vita lakini asilimia kubwa ya wachezaji watakaopata nafasi kwenye kikosi cha kwanza ni wachezaji wa kigeni.
Kwenye mechi hizi za kimataifa ndiyo sehemu pekee ambayo wachezaji wetu wanatakiwa kupata uzoefu mkubwa na mechi za kimataifa lakini kwa bahati mbaya wanaopata nafasi ya kucheza ni wachache ukilinganisha na hitaji letu.
Kwa hiyo TFF wanatakiwa kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu ili kuwatengenezea nafasi kubwa wachezaji wetu ya kucheza kuanzia kwenye ligi kuu mpaka kwenye mechi za kimataifa ngapi ya vilabu.
Ukitazama mashirikisho mbalimbali ya mpira wa miguu Afrika yana mashirikiano na vilabu mbalimbali vikubwa duniani au mashirikisho mbalimbali ya nchi katika ujenzi wa vituo vya kuibua, kukuza na kulea vipaji yani Academy.
Morroco ndiyo mabingwa wa CHAN. Ukiwatazama kwa undani utagundua kuwa wana mahusiano ya kubadilishana mitahala ya mpira wa miguu na Borrusia Dortmund pamoja na timu kumi na sita za ulaya.
Barcelona FC kwa kushirikiana na shirikisho la soka nchini Zambia wamefungua kituo cha kuibua, kulea na kukuza michezo kama ilivyo kwa Rwanda ambako Barcelona na PSG wanampango wa kufungua.
Mashirikiano haya hayapo kwa kiasi kikubwa ndani ya nchi yetu. Shirikisho la soka nchini TFF limekosa namna ya kufanya mashirikiano ambayo yanaweza yakazalisha wachezaji bora ambao wataisaidia timu yetu ya taifa.
Comments
Loading…