in , , , ,

TUHAMASISHE MCHEZO WA BAISKELI

Mchezo wa baiskeli ni mojawapo ya michezo ambayo imesahaulika nchini Tanzania lakini ni michezo ambayo husaidia kujenga afya ya mchezaji kwa kiwango kikubwa. Barani ulaya mashindano ya kuendesha baiskeli ni mojawapo ya mashindano makubwa sana na ambayo huwa yana ufuatiliaji mkubwa sana. Mashindano hayo yanachezwa sehemu za wazi na mara nyingi huchezwa katika barabara kubwa ambapo mamlaka za majiji hushirikishwa na kutengeneza mazingira mazuri ambapo waendeshaji hao wa baiskeli huwekewa mazingira rafiki kwa afya zao kuhakikisha kwamba pindi wanapoendesha baiskeli hawahatarishi afya zao pamoja na afya za watembeaji kwa miguu. Siku za mashindano hayo ya baiskeli askari polisi wa usalama barabarani huwepo kuhakikisha hakuna migongano baina ya watumiaji wa barabara ambao wenye magari, waendesha baiskeli pamoja na raia ambao wanaotembea kwa miguu.

Kwa nchini kwetu Tanzania mashindano ya baiskeli sio mchezo maarufu sana na hata tabia ya kuendesha baiskeli kwa siku zinavyoenda mbele ni tabia ambayo inapotea kwa kasi sana. Kuna maeneo unaweza ukakaa hata siku nzima usione hata mtu mmoja ambaye anaendesha baiskeli. Katika miaka ya nyuma baiskeli ilikuwa ndio chombo kikuu cha usafirishaji miongoni mwa raia wengi wa Tanzania. Kwa sasa maeneo yaliyobaki ambayo angalau utakuta waendeshaji wengi wa baiskeli ni maeneo ya kanda ya ziwa ya nchi katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Kagera. Maeneo mengine waendesha baiskeli wapo ila kwa siku zinavyosonga wanazidi kupungua. Kwa maeneo kadhaa ya vijiji nchini Tanzania kuna watu wanajishughulisha na shughuli za kukodisha baiskeli kwa watu ambao wanaohitaji kutumia usafiri huo kwa kujiendesha wenyewe.

Wafanyabiashara hao huachaji kuanzia shilingi elfu 2 mpaka 3 kwa siku. Uingizwaji wa pikipiki kwa wingi umesababisha utumiaji wa usafiri wa baiskeli upungue kwani pikipiki zimeonekana kama ni mbinu haraka ya kusafiri kutoka sehemu moja mpaka nyingine. Waendesha pikipiki hao wamejipatia umaarufu kwa jina la waendesha bodaboda. Baadhi ya wadau wamekuwa wanalalamika juu ya madhara ya bodaboda licha ya kwamba imepatia ajira za mda mfupi waendesha pikipiki hizo wengi lakini nazo zimekuja na majanga yake ikiwemo ajali nyingi sana barabarani zimeongezeka kutokana na baadhi ya waendesha bodaboda kutokuwa makini na kanuni za usalama barabarani. Ajali hizo zimesababisha vifo pamoja na vilema vya kudumu kwa wahanga wa ajali hizo.

Kwa muono wangu mimi ni muda muafaka kwa sasa kuanza kuhamasisha uendeshaji wa baiskeli katika maeneo mbalimbali nchini. Naweza kusema hivyo kwa hoja zifuatazo;

Mosi kupunguza uchafuzi wa mazingira. Tunafahamu kwamba matumizi ya vyombo vya motokaa kwa wingi vinatoa hewa ambazo zinaenda kuharibu tabaka la O zone ambalo ndio tabaka ambalo linalosaidia kupunguza madhara ya jua kwa wanadamu na viumbe vingine katika ulimwengu. Hewa chafu zinapotolewa kwa wingi huwa zinaenda kutoboa tabaka la O zone na kusababisha ufa uzidi kuongezeka. Baiskeli huwa haisababishi kutolewa kwa hewa yoyote chafu bali ni mfumo rafiki wa usafiri. Kwa kusema hivyo simaanishi watu waache kabisa kutumia usafiri wa vyombo vya moto hapana ila nahamasisha wapunguze tu. Nchi zilizoendelea kama vile Uholanzi zinahamasisha kwa wingi sana raia wake watumie usafiri wa umma pamoja na baiskeli katika matumizi ya kila siku.

Pili kuendesha baiskeli kuna faida lukuki za kiafya kwa mwendeshaji baiskeli. Faida ya kwanza husaidia kupunguza uzito. Mtu akiwa anaendesha baiskeli mara kwa mara anakuwa anachoma mafuta hatari katika mwili wake (cholesterol) ambayo mafuta ndio huwa yanasababisha unene kupita kiasi ambao mbeleni humletea matatizo ya kiafya. Pili wataalamu wanasema kwamba mtu ambaye anaendesha baiskeli mara kwa mara anajiweka katika mazingira mazuri ya kuzuia hatari ya ugonjwa wa kupooza(stroke), hujiweka katika mazingirfa mazuri ya kujizuia ugonjwa wa kisukari(diabetes). Tatu wataalamu wanasema kwamba kitendo cha kuendesha baiskeli humsaidia mwendeshaji kutuliza akili yake kwa hivyo hatimaye humsaidia katika kupunguza athari za msongo wa mawazo (sonono). Nne wanasema kwamba uendeshaji wa baiskeli humsaidia mwendeshaji kupunguza nyama ambazo zinazokuwa zinapatikana katika makalio na hivyo kumfanya mwendeshaji awe na muonekano mzuri ambao ulionyooka.

Nne kuhamasisha kuendesha baiskeli kutasaidia katika kupunguza foleni katika baadhi ya barabara katika baadhi ya miji. Baadhi ya miji imekuwa ni kero sana kwa watumiaji wa barabara hizo ambapo wamekuwa wanakumbana na adha ya foleni ambazo huwa zinasababishwa na msongamano wa magari. Nchi zilizoendelea katika baadhi ya maeneo zimekuwa zinahamasisha sana hivyo na baadhi ya maeneo wamefanikiwa katika hilo.

Jukumu la kuhamasishana kutumia baiskeli kwa ajili ya ustawi wa maisha yetu kiafya na kiuchumi ni jukumu la kila mtu kuanzia viongozi wa serikali, sekta binafsi mpaka kwa raia wa kawaida. Tufahamu pia kwamba haiba hii ikijengeka vizuri basi itakuwa ni rahisi sana kwa watanzania wengi kushiriki mashindano ya kimataifa ya uendeshaji baiskeli na kuibuka mabingwa katika mashindano hayo. Halikadhalika kwa kuwa baiskeli nyingi hazitengenezwi nchini Tanzania nashauri serikali kuweka mazingira rafiki ya kodi katika uingizwaji wa bidhaa hiyo nchini.

Suala la hamasa ya kuendesha baiskeli kwa wingi lianzie kwa wanafunzi wa shule za vijijini ambao gharama za usafiri kutoka nyumbani kwenda mashuleni ni kubwa ambapo hupelekea wanafunzi wengi sana kutembea kwa miguu kilomita nyingi mpaka mashuleni ambapo hupelekea wengi wao kuchoka mapema na kuanza tabia hatarishi kama utoro na hatimaye kuacha kabisa kusoma.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

SIFA ZA MAKOCHA WANAOTAKIWA LIGI KUU BARA

Tanzania Sports

MAPATO NA MATUMIZI YA VYAMA VYA MICHEZO..