Michezo yote 10 ya wiki ya sita ya EPL imeshachezwa. Kwenye makala hii mwandishi wetu amechagua kikosi cha wachezaji 11 waliofanya vizuri kwenye michezo ya EPL wiki hii.

 

Golikipa: ADRIAN (West Ham)

Adrian, kipa hodari sana...
Adrian, kipa hodari sana…

Adrian alikuwa amerejea kutoka kwenye kifungo cha mechi tatu hapo juzi ambapo West Ham waliwafunga Manchester City mabao mawili kwa moja. Alisimama imara langoni akazuia michomo kadhaa ya hatari na kuihakikishia ushindi timu yake.

 

Mlinzi wa Kulia: SIMON FRANCIS (Bournemouth)

SIMON FRANCIS, Alikuwa chachu ya ushindi kwa timu yake.
SIMON FRANCIS, Alikuwa chachu ya ushindi kwa timu yake.

Alitawala upande wake wa kulia kwenye mchezo dhidi ya Sunderland. Francis aliongoza kwa kuwanyang’anya mipira wachezaji wa Sunderland na akapandisha vyema mashambulizi ya Bournemouth walioibuka na ushindi wa 2-0.

 

Mlinzi wa Kati: WINSTON REID (West Ham)

WINSTON REID, Amekuwa na mchezo mzuri sana hivi karibuni.
WINSTON REID, Amekuwa na mchezo mzuri sana hivi karibuni.

Washambuliaji wa Manchester City hawakuweza kufua dafu dhidi ya ulinzi imara wa West Ham hapo juzi. Kazi kubwa ilifanywa na Winston Reid ambaye aliondosha mpira kwenye eneo la hatari mara 21 ambayo ni rekodi ya msimu huu.

 

Mlinzi wa Kati: ASHLEY WILLIAMS (Swansea)

Nahodha huyu alitoa changamoto imara dhidi ya washambuliaji wa Everton kwenye mchezo wa juzi. Mara kadhaa aliondosha mpira kwenye eneo la hatari katika mazingira magumu na hivyo timu yake ikamaliza mchezo bila kufungwa bao.

 

Mlinzi wa Kushoto: ALBERTO MORENO (Liverpool)

Alihusika zaidi na mshambulizi ya upande wa kushoto na akatengeneza nafasi nyingi hasa kwenye kipindi cha kwanza dhidi ya Norwich. Kiwango alichoonyesha jana kinaweza kumpa moja kwa moja nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool.

 

Kiungo wa Kati: CESC FABREGAS (Chelsea)

Achana na pasi ya bao aliyotoa kwenye mchezo ule dhidi ya timu yake ya zamani hapo juzi. Kinachomuweka Cesc Fabregas kwenye kikosi cha wiki hii ni namna alivyoweza kulitawala eneo la kiungo kwenye mchezo huo kadri alivyotaka.

 

Kiungo wa Kati: KEVIN DE BRUYNE (Manchester City)

Jitihada za kiungo huyu na kiwango kikubwa alichokionyesha kwenye mchezo dhidi ya West Ham vilitosha kabisa kumfanya aifungie timu yake bao la kufutia machozi. Mbali na bao alilofunga alihusika na sehemu kubwa ya mashambulizi ya Man City.

 

Kiungo wa Kulia: MATT RICHIE (Bournemouth)

Bila shaka Ritchie alikuwa nyota wa mchezo dhidi ya Sunderland. Winga huyu aliweka kifuani mpira uliookolewa na walinzi wa Sunderland kisha akapiga shuti kali lililompita golikipa Pantilimon na kuwashangaza waliotazama mchezo ule.

 

Kiungo wa Kushoto: SON HEUNG MIN (Tottenham)

Son alikuwa mchezaji wa Tottenham aliyejituma zaidi hapo jana kwenye mchezo dhidi ya Crystal Palace. Usumbufu wake uliwapa tabu mno wachezaji wa Crystal Palace na akafunga bao pekee la mchezo huo lililoipa timu yake alama tatu.

 

Mshambuliaji: ANTHONY MARTIAL (Manchester United)

Martial alitulia na akamalizia vyema nafasi alizopata na kufunga mabao mawili dhidi ya Southampton hapo jana. Anajaribu kukilipa mapema kiasi cha paundi milioni 36 ambazo Manchester United walizitumia kumnunua wiki chache zilizopita.

 

Mshambuliaji: GRAZIANO PELLE (Southampton)

Mshambuliaji huyu hahitaji maelezo mengi. Kiwango alichoonyesha dhidi ya Manchester United na mabao mawili aliyofunga vingetosha kuipatia timu yake alama tatu muhimu kama wachezaji wa nafasi nyingine nao wangejitoa mhanga.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

MZUNGUKO WA TATU LIGI KUU BARA

Tanzania Sports

Samatta wa Ulaya