in ,

Thamani ya jezi namba 10 imebaki ileile?

fikiria thamani ya jezi nambari 10

HIVI karibuni rafiki yangu mmoja alinitumia picha ya video ikimuonesha mshambuliaji wa Italia, Francesco Totti akifunga penati yake kwa staili ya Panenka dhidi ya golikipa Edwin van Der Sar. 

Ulikuwa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya (Euro) mwaka 2000 kati ya Italia na Uholanzi. Fainali za Euro za mwaka 2000 ziliandaliwa kwa ushirikiano wa nchi za Ubelgiji na Uholanzi.

Kwenye fainali hizo Francesco Totti na Fracensco Toldo walikuwa miongoni mwa wachezaji waliovuma mno. Toldo alikuwa mlinda mlango mahiri na Totti akiwa kiungo mshambuliaji matata zaidi kwenye kikosi cha Italia. Kikosi chao kilijaa vipaji wenye viwango vizuri wakiongozwa na Paolo Maldini. 

Totti alikuwa anavaa jezi nambari 20 katika kikosi cha Italia kilichoshiriki michuano ya Euro mwaka 2000. Hapo kwenye nambari ya jezi ndipo penye mjadala wangu wa leo nanyi wasomaji. 

Labda msomaji hebu fikiria thamani ya jezi nambari 10 ilivyozoelezwa katika kandanda. Fikiria namna ambavyo maelfu ya mashabiki wanavyothamini mchezaji anayevaa jezi nambari 10.

Kazi ya Totti

Namna mabenchi ya ufundi na wachambuzi wanavyowazungumzia wachezaji wanaovaa jezi nambari 10. Wanaonekana kuwa ni wachezaji wa kipekee mno katika mchezo wa kandanda. 

Si Ulaya pekee, bali hata kwenye nchi zetu za Afrika kumekuwa gumzo juu ya wachezaji wanaovaa jezi namba 10. Ni wachezaji wanaoheshimika na wenye hadhi ya juu. 

Mimi nahusudu wachezaji wenye sifa na hadhi wapewe jezi nambari 10 katika kikosi. Ni wakali, mafundi, wana ujuzi kuliko wenzao na pia wanabeba majukumu ya ushindi ya timu zao.

Nakumbuka baada ya fainali za Euro 2000 uliibuka mjadala nchini Italia, juu ya nani anastahili kuvaa jezi nambari 10. Je, ni Francesco Totti au Alessandro Del Pierro? Mjadala huo ulikuja kujibiwa miaka miwili baadaye.

Zilipofika fainali za kombe la dunia mwaka 2002 Del Pierro alipewa jezi nambari 7 badala ya nambari 10. Jezi namba 10 alikabidhiwa Francesco Totti.

Maajabu ni kwamba katika mechi dhidi ya Mexico Totti alicheza dakika nyingi takribani 80 uwanjani lakini alishindwa kuisaidia Italia kusawazisha bao ambalo lingewaokoa na kusonga mbele.  Wakati wote huo Del Pierro alikuwa amekaa benchi akiwa amevalia jezi yenye nambari mpya 7. Hiyo ilikuwa na maana hadhi ya Del Pierro iliporomoka, hivyo Totti akawa kipenzi cha makocha na mashabiki pia.

Licha ya kucheza dakika nyingi katika pambano hilo, Totti hakufanikiwa kuzifumania nyavu za wapinzani wao. Ndipo kocha wa Italia alimwinua Del Pierro kuingia uwanjani.  Totti alitolewa kumpisha  Del Pierro. 

Ndani ya dakika chache alizoingia Del Pierro akatupia bao la kusawazisha na kuinua matumaini ya Italia kusonga mbele katika hatua ya raundi ya kwanza mtoano. 

Nakumbuka mchezo wao na Mexico ulikuwa na kituko kimoja muhimu. Italia walitumia dakika za mwisho mwisho kupasiana kwenye eneo lao bila kushambulia lango la adui kwa lengo la kulinda pointi moja waliyovuna wakati huo. 

Italia hawakupiga pasi kwenda mbele, nao Mexico wakatulia tuliiii. Refa naye akabaki amesimama tu hana cha kufanya zaidi ya kuzungusha kichwa kutazama pasi za Italia kwenye lango lao. 

Mjadala ukarudi tena. Ni nani alistahili kuvalishwa jezi nambari 10 kati ya Del Pierro na Totti? Kwa mwaka 2000 wakati Euro ilionekana Del Pierro amefulia kiwango. Lakini mambo yakapinduka mwaka 2002 baada ya kuonekana Totti hakukata kiu ya mashabiki na wachambuzi wa soka. 

Mgongoni akiwa na jezi nambari 10 uzito wake ulionekana kumwelemea. Jina la Del Pierro likarudi kwenye chati. Kocha alaumiwa kwa maamuzi ya kumpora jezi nambari 10. 

Inasadikika jezi nambari 10 inabeba heshima ndani ya kikosi chochote. Hata kwenye kikosi chetu cha Taifa Stars jezi nambari 10 inayovaliwa na nahodha Mbwana Samatta ina heshima yake. 

Mchezaji anayepewa jezi hiyo maana yake anakabidhiwa hadhi fulani. Ni utamaduni uliozoeleka kwenye mpira wa miguu. Lakini je, ile hadhi imebaki ileile? Unaweza kuiona hacdhi hiyo kwa Luka Modric. Neymar, Eden Hazard, Mesut Ozil na wengineo wa kizazi hiki?

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Morrison ni mkubwa kuzidi Yanga

Morrison ni mkubwa kuzidi Yanga !

Manara, Muro na Nugaz nani zaidi?