in

‘Ligi ya wahenga’ kupindua utawala Juventus?

Paulo Dybala

Msimu mpya wa Ligi Kuu Italia maarufu kama Serie A umeanza wikiendi iliyopita. Fiorentina  walikumbana na Torino, kisha Hallas Verona wakamenyana na AS Roma. Timu hizo ndizo  zilifungua dimba, lakini zipo habari nyingi za kuzungumzia katika Ligi hiyo hadi kukamilika  kwake. Ni nini mabingwa watetezi Juventus watafanya msimu huu? Je Cristiano Ronaldo na  Zlatan Ibrahimovic wataendelea kucheza kwa viwango vya juu? Na vipi kiungo kutoka  Marekani, Weston McKennie ataleta ladha gani katika Ligi hiyo? Vipi kocha mpya Andre Pirlo  ataleta miujiza mipya Juventus ama taji lao litawatoroka? Tanzaniasports inakuletea majibu ya  maswali yote. 

MBIO ZA UBINGWA 

JUVENTUS: Halitakuwa jambo la ajabu Juventus wakitafuta ubingwa wa kumi mfululizo wa  Serie A. hii itakuwa timu ya kufuatiliwa mno msimu huu, hasa ikiwa na kocha mpya ambaye  alikuwa miongoni mwa wanakandanda wakali dimbani, Andrea Pirlo. Juventus wameanza  msimu huu bila wachezaji Gonzalo Higuain na Miralem Pjanic ambao wamehamia Inter Milan  na Barcelona. Naye Blaise Matuidi ameondoka Juventus. Msimu huu utaonesha kama  wamemerika zaidi au wameshuka. 

Arthur Melo amewasili Serie A atakuwa sehemu ya kikosi cha Pirlo. Mbrazil huyo aliawahama  miamba ya soka Barcelona baada ya kukosa namba kikosi cha kwanza pamoja na msimu mbovu  wa timu hiyo. McKennie kuhamia Juventus nako ni habari kubwa ingawa mabosi wa Turin  wanaona usajili wa Herculez Gomez ni spesho kwao kuliko McKennie. 

INTER MILAN: hawa walishika nafasi ya pili msimu uliopita. Wananonelewa na kocha  Antonio Conte, nao wana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Serie A. Antonio Conte anatakiwa kuleta  ubingwa klabuni hapo, vingine vyo hataweza kutwaa tena taji hilo. Arturo Vidal amewasili Inter  Milan akitokea Barcelona. Sandro Tonali ataungana na Vidal kuimarisha eneeo la kiungo, wakati  Achraf Hakimi aliyewika Bundesliga alipokuwa Borussia Dortmund kwa mkopo msimu uliopita,  naye ni sehemu ya kikosi cha Antonio Conte akitokea Real Madrid. Conte amefanikiwa  kumbakiza mshambuliaji wake Lautaro Martinez ambaye ndiye chachu ya mafanikio klabuni  hapo.  

ATALANTA: Inaonekana kama vile mechi ya watani wa jadi Serie A m,aarufu kama Derby  d’Italia zitakuwa ngumu zaidi, kwa sababu huwezi kuiweka kando Atalanta ambao wamekuwa  wkwenye kiwango bora kwa misimu miwili sasa. Msimu uliopita walibakiza dakika chache  kucheza nusu fainali kabla ya kutolewa na PSG.

TATU; Timu tatu za Napoli,Roma na AC Milan nazo zinafanya jitihada za kuboresha vikosi  yao., lakini wana kazi ya ziada ili kuzifikia timu tatu tulizozitaja hapo awali.  

LAZIO: Wakati huo huo Lazio nayo itakuwa tayari kwa mashindano wakiwa na mataumini  msimu huu ni nafasi yao ya kunyakua ubingwa. Lazio wameingia msimu huu wakiwa na  maumivu baada ya kumkosa David Silva katika dakika za lala salama baada ya nyota huyo wa  zamani wa Manchester City kubadili uamuzi na kurejea La Liga katika klabu ya Real Sociedad  ya Hispania. Uamuzi huo ulimkera mkurugenzi wa ufundi wa Lazio, Igli Tare. 

RONALDO AU ZLATAN? 

Mastaa wawili wenye sifa kemukemu katika soka wataziwakilisha klabu zao za Juventus na AC  Milan. Ni rahisi kusahau namna wanavyocheza katika umri wao wa sasa, lakini msimu uliopita  Ronaldo alipachika mabao 31 katika mechi 33 za Serie A akiwa na Juventus waliotwaa ubingwa.  Kwahiyo kulingana na takwimu hizo, tunaweza kumwongelea Ronaldo wa msimu mpya na  Juventus yake, wataleta nini zaidi?  

Mabosi wa Jeventus wanaamini Ronaldo bado hajaonesha kiwango chake kikubwa. Juventus  wanatafuta mchezaji sahihi anayeweza kushirikiana na Ronaldo katika safu ya ushambuliaji.  Mchezaji ambaye atafanya kazi ya kumtengeneza Ronaldo nafasi za kufunga. Juventus wanataka  kuona kombinesheni kama ya Ronaldo na Karim Benzema iliyowapa mataji Real Madrid.  

Ronaldo ana miaka 35 kwa sasa, ana nguvu nab ado anaonekana mpambanaji akiwa amebakiza  misimu minne kabla ya kutundika daruga. Upande mwingine yupo Zlatan Ibrahimovic ambaye  katika mchezo wa kwanza alipachika mabao mawili kwa AC Milan kwenye mechi ya kwanza ya  Serie A msimu huu. Zlatan ana miaka 38, lakini anaonekana bado ana vitu vya kuwanufaisha AC 

Milan. 

Msweden huyo anaonekana ni mfalme wa San Sirro. Baada ya kujiunga na AC Milan Januari  mwaka huu akiwa chini ya Stefano Pioli alichangia mabao 10 kati ya mechi 18 alizocheza na  anaonekana bado ana vitu adimu vya kusaidia klabu hiyo. Wengi wanaweza kusema wanatarajia  msimu huu utakuwa wa Ronaldo tena, lakini Zlatan huwa ana matukio ya kusisimua zaidi. 

SURA MPYA ZA KUTAZAMA 

Jumla ya pauni milioni 540 zimetumika kufanya usajili wa wachezaji 129 hadi wakati  yanaandikwa makala haya. Dirisha la usajili Italia litafungwa Oktoba 5 mwaka huu.  

Arthur Melo; Juventus wamelipa kiasi cha pauni milioni 64 kutoka Barcelona. Atakuwa  mchezaji mwenye uchu wa kufanya kazi na Andrea Pirlo, akitarajiwa kuunda kombinesheni na  Weston McKennie na Dejan Kulusevski aliyesajili januari mwaka huu. 

Achraf Hakimi; usajili wenye kila aina ya pongezi kwa Inter Milan, ambao wamenunua beki  huyo wa kulia kwa pauni milioni 36 kutoka Real Madrid. Hakimi alikuwa nyota msimu uliopita 

pale Borussia Dortmund na alikuwa mmoja w amabeki wanaosakwa zaidi barani Ulaya. Inter  Milan walichukua uamuzi wa haraka na makini kumsajili nyota huyo.  

Barella na Sensi; Aleksandar Kolorov ni beki wa akiba upande wa kushoto, lakini eneo hilo  limeongezewa nguvu kwa usajili wa Nicolo Barella na Stefano Sensi kutoka Vagliari na  Sassuolo. 

Vedat Muriqi; Lazio wao wameirisha kikosi chao kwa kuwasajili washambuliaji Vedat Muriqi  kutoka Kosovo. Awali Muriqi alisajiliwa na Napoli, lakini baada ya kumnasa Victor Osimhen  kutoka Lille kwa pauni milioni 63 wakaamua kumuuzaMuriqi. Kikosi cha Genaro Battuso  kitanufaika na usajili wa Muriqi. 

Kwingineko AS Roma wamemsajili Pedro kutoka Chelsea, lakini wana kazi ya kuboresha kikosi  chao. Fiorentina wamemsajili Spfyan Amrabat kutoka Verona, na Cagliari wamekuwa kwenye  hekaheka za kukamilisha usjaili wa Diego Godin, wakati AC Milan wameongeza mkataba wao  na Zlatan, wakati Brahimi Diaz amechukuliwa kwa mkopo.  

VITA YA NDUGU WAWILI  

Filipo Inzaghi alikuwa mshambuliaji hatari uwanjani. Amewahi kuzichezea Atalanta, Parma,  Juventus na AC Milan na mshindi wa kombe la dunia mwaka 2006, pamoja na Ligi ya  Mabingwa mara mbili. Lakini ndugu yake Simone Inzaghi hakufanikiwa kama kaka yake Filipo.  Simone alitumia muda wake kucheza klabu ya Lazio ambako alitwaa mataji ya Serie A na UEFA  Cup, lakini hakuwa na mafanikio zaidi. 

Kwa sasa wapo ndugu wawili Simone Inzaghi na Filipo Inzaghi ambao ni makocha. Simone  Inzaghi ana miaka 44 aliteuliwa kuwa kocha wa Lazio mwaka 2016 kuchukua mikoba  iliyoachwa na Marelo Biesla. Tangu awe kocha wa Lazio amechukua mataji matatu; Coppa Italia mara moja na Italian Supercoappa mara mbili. Lazio wamekuwa washindani wa Juventus katika  kipindi ambacho kibibi kizee cha Turin kimeshika hatamu Serie A. 

Filippo Inzaghi ana miaka 47, alianza maisha ya ukocha mwaka 2014 baada ya kukabidhiwa  mikoba ya AC Milan, kabla ya kufukuzwa baada ya miezi 12 baada ya timu yake kushika nafasi  ya 10 katika msimamo wa Ligi. Baadaye alikuwa kocha wa Venezia iliyofanikiwa kutwaa taji la  Ligi daraja la Pili. Baadaye alihamia Bologna lakini alifukuzwa baada ya kushinda mechi 2 kati  ya 21. Mbaya zaidi alifugwa mabao 2-0 na kikosi cha mdogo wake Simone Inzaghi, Lazio. Msimu uliopita Filipo Inzaghi alikuwa kocha wa Benevento ya daraja la pili ilitotwaa taji hilo na  kufanikiwa kutengeneza falsafa yake ya kucheza. 

MATAJIRI WA MAREKANI 

Serie A imeshuhudia kuibuka vipaji kutoka Marekani katika uongozi na uwnajani. Juventus  wamemsajili McKennie kwa dau kubwa la kihistoria Marekani. Msimu huu umeshuhudia 

matajiri wa Marekani, Kyle Krauser akinunua Parma na Dan Friedkin ikiinunua AS Roma.  Matajiri hao wa Marekani wameungana na Paul Singer aliyenunua Fiorentina 

USIKOSE MECHI HIZI 

Juventus vs Napoli; Oktoba 10 

Inter Milan vs AC Milan; Oktoba 17 

AC Milan vs Juventus; Januari 1, 2021 

Lazio vs Roma; Januari 17, 2021. 

Inter Milan vs Juventus; Mei 16, 2021

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Samatta Aandaliwe Kisaikolojia

Mbwana Samatta

Wachezaji wa Tanzania watafute ‘Connection’