in

Taifa Stars wamtumia ujumbe Rais Samia Suluhu

Bao lililofungwa na mshambuliaji wa Taifa Stars, Simon Msuva lilitosha kulinda heshima na kunyakua pointi tatu ambazo ni sawa na kutuma ujumbe wa kumkaribisha rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyeingia madarakani Machi 19 mwaka huu kufuatia kifo cha rais John Magufuli. Rais Magufuli alifariki Machi 17 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es salaam kwa matatizo ya moyo.

Ushindi huo wa Taifa Stars ulipa nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi J ambalo linaundwa na vinara Tunisia,Guinea Ikweta, Tanzania na Libya. Ni mataifa mawili ndiyo hufuzu kwa mashindano ya AFCON ambayo ni Tunisia na Guinea Ikweta.

Taifa Stars wakicheza kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kikosi cha Taifa Stars kilimenyana na Libya katika mchezo wa mwisho wa kuwania kufuzu.

Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa wamevalia vitambaa vyeusi kuashiria kuwa majonzi ya kufiwa na Rais wa nchi John Magufuli. Katika michezo yote michezo yote miwili waliyocheza walikuwa wamevalia vitambaa vyeusi.

Tanzania Sports
Msuva

Hata hivyo mchezo huo haukuwa na nafasi ya kufuzu AFCON kutokana na washindani wao wawili Guinea Ikweta na Tunisia kuwa tayari wamefuzu katika kundi lao. Tunisia wao waliinyuka Libya mabao 4-2 katika mchezo uliopita, wakati Tanzania ilinyukwa bao 1-0 na Guinea Ikweta.

Ushindi wa Tunsia ulimaanisha wamejikusanyia pointi 13 huku mshindi wa pili akiwa Guinea Ikweta aliyejikusanyia pointi 9, ambao kama wangetoka suluhu na Tanzania nafasi yao ya kufuzu ingelikuwa finyu.

Ushindi wa Taifa Stars bado usingeweza kuivusha Taifa Stars, lakini wangekuwa na matumaini kama mchezo wao na Guinea Ikweta wangetoka uluhu au sare ya aina yoyote.

Ufundi wa Wydad Casablanca

Simon Msuva amekuwa na msimu mzuri katika klabu yake ya Wydad Casablanca katika mashindano ya klabu Bingwa Afrika. Akiwa ndani ya kikosi cha Wydad amekuwa mfumania nyavu mahiri,anayejituma na kutumia kila nafasi anayopatya. Msuva wa sasa ameongezeka uimara wa mwili,anajiamini, anao uzoefu na ufundi wa kutosha kwa sasa. Kwa hakika anawakilisha ufundi aliopata Wydad katika Ligi Kuu Morocco.

Alama moja nyuma

Wakati Taifa Stars inafuzu kwa mashindano ya AFCON mwaka 2019 ilimaliza kwenye kundi lake ikiwa na pointi 8. Ni pointyi hizo ndizo ziliipeleka Taifa Stars kwenye mashindano hayo yaliyofanyika nchini Misri. Lakini katika hatua za awali za kufuzu kwa mashindano ya AFCON mwaka 2021 Taifa Stars imejikusanyia pointi 7 ikiwa alama moja nyuma ya mwaka 2019.

Nyota wa kigeni

Taifa Stars ikiongozwa na nahodha wake Mbwana Samatta anayekipiga katika klabu ya Fenebahnce ya Uturuki ilikuwa na mastaa wengine wanaocheza soka la kulipwa katika nchi mbalimbali. nyota hao walilijumuika kutafuta pointi tatu na kumkaribisha Rais Samia katika uongozi wake. Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo), Nickson Kibabage (Difaa el Jadida, Morocco), Simon Msuva (Wydad Casablanca, Morocco) na Himid Mao (ENNPI, Misri). Wengine ni Shaban Chilunda, Yohana Nkomola,

Mwanzo mpya,kocha mpya

Huu ni mchezo wa pili wa kimashindano wa kocha mpya Kim Poulsen tangu alipochukua kibarua hicho kutoka kwa Ettiene Ndayiragije. Katika kipindi cha Ndayiragije Taifa Stars ilifuzu mashindano ya CHAN yaliyofanyika nuko Cameroon. Katika mchezo wa kwanza kikosi cha Kim Poulsen kilifungwa bao 1-0 na wenyeji Guinea Ikweta, lakini amefanikiwa kushinda mchezo wa nyumbani dhidi ya Libya. Kim Polusen ameongoza Taifa Stars katika michezo minne hadi sasa, ambapo michezo miwili ya awali ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Kenya.

Katika kikosi chake kocha Kim Poulsen amemweka benchi beki kisiki Bakari Mwamnyeto na badala yake anatumia Kennedy Juma. Nafasi ya beki wa kushoto amewaita wote watatu; Mohamed Hussein (Simba), Yassin Mustapha (Yanga) na Nickson Kibabage (Difaa el Jadida). Lakini ni Kibabage na Hussein wamecheza mechi za kimashindano, wakati Mustapha amecheza mechi za kirafiki dhidi ya Kenya.

Safu ya kiungo bado inawategemea Feisal Salum na Jonas Mkude, wakati Baraka Majogoro aliyekuwa anapewa nafasi ya kocha Ettiene Ndayiragije akiachwa nje ya kikosi cha Taifa Stars licha ya kuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki mashindano ya CHAN nchini Cameroon na akapachika bao moja.

Mawinga Deus Kaseke na Hassan Dilunga wamepangwa katika mchezo wa pili dhidi ya Libya. Kwenye ukuta wapo Kennedy Juma na Erasto Nyoni. Ni kocha mpya na mwanzo mpya.

Katika safu ya ushambuliaji Mbwana Samatta na Simon Msuva hawatemeki, wakati Thomas Ulimwengu aliambulia sekunde chache kwenye mchezo dhidi ya Guinea Ikweta, lakini kwenye mchezo dhidi ya Libya hakuwepo katika oridha ya wachezaji waliopangwa hata kukaa benchi. Ni wmanzo mpya wa Kim Poulsen.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Samia Suluhu

Rais Samia Suluhu tegemeo katika michezo

comoro

COMORO WAMEWEZA SISI TUSHINDWE WAPI?