in

Rais Samia Suluhu tegemeo katika michezo

Samia Suluhu

Machi 26, 2021 ndiyo siku ya kuagwa aliyekuwa rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli huko Chato mkoani Geita. Kiongozi huyo amedumu madarakani kwa miaka mitano na siku 114, aliaga dunia kutokana na ugonjwa moyo na nafasi yake imechukuliwa na Samia Hassan Suluhu.

Machi 19 mwaka huu Makamu wa rais Samia Hassan SUluhu alikula kiapo cha kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuonesha kuwa sasa utakuwa mwanzo mpya uongozi wa rais huyo wa sita nchini.

Sekta ya michezo inamtegemea kiongozi huyo mpya kuimarisha sekta ya michezo. Kuanzia mchezo wa soka,ndondi,mpira wa pete,kikapu,mikono,riadha na mingineyo yote inamwangalia kiongozi huyo mpya.

Katika uongozi wa rais Benjamin Mkapa alijenga uwanja wa Taifa ambao sasa unaitwa uwanja wa Benjamin Mkapa. Hiyo ni kuthamini mchango wa kiongozi huyo katika sekta ya michezo.

Naye rais mstaafu Jakaya Kikwete alishiriki kwenye michezo kwa kuajiri kocha wa kigeni Marcio Maximo ambaye alileta mabadiliko makubwa ya mchezo wa soka nchini.

Katika kipindi cha Rais Magufuli tumeona hamasa kadhaa katika michezo ambako aliahidi kujenga ujwanja mkubwa wa michezo wa kisasa mkoani Dodoma.

Ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 80,000 unatarajiwa kuwa kimbilio la watu wengi ndani na nje ya nchi. Ni miongoni mwa zawadi ambazo wameachiwa Watanzania.

Kikwete na Magufuli walitupia macho mara kwa mara timu za taifa ili kuhakikisha ushiriki wao unakuwa na tija. Rais Samia Suluhu bila shaka anatarajiwa kutupia macho pia kwenye eneo hilo, kuanzia timu za taifa ya mpira wa kikapu,mikono,riadha,judo,pool table,kareti na kadhalika.

Sekta ya michezo nchini licha ya kuwa burudani inapaswa kuongezewa uwanja mpana wa kutoa tija kwa wananchi wake pamoja na kupanua biashara ya michezo.

Samia anatakiwa kutupia jicho viwanja vya michezo mingi, ambapo baadhi ya watoto na vijana wameonesha vipaji vyao. Kwa mfano mtoto mwenye kipaji cha kucheza mchezo wa Tenisi akiwa Mbagala anatakiwa kufuata uwanja wa mazoezi uliopo Gymkhana ili kuonesha kipaji chake.

Umbali huo unachangia kupoteza muda barabarani,kukosa ari,changamoto ya usafiri na kadhalika. Hii ina maana ili mtoto huyo aweze kucheza Tenisi maana yake inatakiwa kilashule za msingi na sekondari zizingatie mchezo huo ili kuibua vipaji.

Ni vigumu watoto wanaoishi kwenye mikoa ambayo hakuna viwanja vya mchezo wa gofu wala Tenisi, lakini ni jukumu la serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma hizo unakuwepo mashuleni ili kutengeneza vipaji vitakavyoleta tija kwa nchi.

Shule za msingi na sekondari zina walimu wa michezo ambao wanaweza kuchangia kuibua vipaji vya wanamichezo zaidi nchini. Kwahiyo serikali ya Rais Samia inatakiwa kuzingatia michezo kama mojawapo ya biashara zenye tija kwa taifa.

Mwezi Julai mwaka huu dunia itashuhudia mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika nchini Japan, ambapo Alphonce Simbu mwanariadha wa Tanzania atakuwa miongoni mwa washiriki.

Lakini serikali ya Rais Samia inatakiwa kutathmini ushiriki wetu kwenye mashindano hayo. Kwamba kwanini tanzania inakuwa na washiriki wachache? Je ni kweli Tanzania hakuna vipaji vya kurusha tufe,kuruka juu (High Jump),ngumi,kuruka chini (Long jump), kuruka vihunzi,mbio za vijiti na michezo kedekede inayofanyika kwenye Olimpiki?

Kama nchi zingine zinafuzu kwa mashindano ya Olimpiki ni kwanini Tanzania isiwe miongoni mwao? Kama tulifanikiwa kufuzu mashindano ya AFCON baada ya miaka takribani 30 viweje tushindwe kufurukuta pale Morocco ili twende Japan? Inakuwaje kila mwaka wa mashindano tuishie kwenye majaribio ya kutafuta viwango vya kushiriki Olimpiki?

Ni muhimu kama taifa kutafakari aibu hii kwa watu zaidi ya milioni 40 hatuna uwezo wa hata kurusha tufe,mshale au mbio za kuruka vihunzi? Ni muhimu serikali kupitia Baraza la Michezo na wanachama wake waone aibu namna taifa linavyokosa uwakilishi kwenye mashindano mbalimbali ya nje.

Serikali ya Samia ijadili kwanini hatuna mafanikio kwenye mashindano ya Afrika ya Kanda Tano na mengineyo ambayo tumeshindwa kupata medali. Tunafahamu kuwa vipaji tunavyo kuanzia shule mza msingi,sekondari hadi vyuo vikuu.

Taifa letu linahitaji vijana wenye uchu kama Hassan Mwakinyo na mabondia wengine ambao watapeperusha vema bendera yetu. Ni wakati wa kuwaweka kitimoto viongozi wote wa vyama vya michezo nchini ili watuoneshe kwa maneno na vitendo kutekeleza na kupata mafanikio ya michezo wanayosimamia nchini.

Tumechoshwa na siasa za michezo ambazo zimekuwa zikivuruga na kutawala zaidi kwenye vyama vya michezo kuliko mafanikio ya michezo husika.

Ni wakati wa Rais Samia Suluhu kutuonesha njia ya mafanikio. Ni wakati wa rais wetu kuwaambia viongozi wenzake wa CCM kuwa wanatia aibu kwa viwanja vibovu,vichafu na visivyo na heshima hata kwa Ligi Kuu Tanzania Bara. Ni wakati wa kuwaambia viongozi wenzake wa CCM kuwa soka linavutia wachezaji wa kigeni na viongozi wa kigeni kwahiyo ni muhimu kuwa na viwanja vyenye ubora kwa kila mchezo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Jamie Vardy

JAMIE VARDY NI MFANO WA KUIGWA KWA WACHEZAJI WA “NDONDO”

Tanzania Sports

Taifa Stars wamtumia ujumbe Rais Samia Suluhu