*Wapigwa 7-0 na Algeria
*Waliahidi kufia uwanjani
Ndoto za Watanzania kufika angalau hatua ya makundi kwa ajili ya kutafuta kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018 zimefutika kwa aibu kubwa.
Stars walioanza harakati hizo vyema kwa kuwanyoa Malawi na kisha kuwakaribisha Algeria Dar es Salaam na kwenda sare ya 2-2 wamefia Algeria.
Vijana hao wanaonolewa na kocha Charles Boniface Mkwasa waligangamala kipindi cha kwanza jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya mkondo wa kwanza, kisha wakafanikiwa kuongoza 2-0.
Hata hivyo, Algeria walidhihirisha uzuri wao na uwapo wa wachezaji wazuri zaidi na wa kimataifa, wakiwamo wanaocheza ligi kubwa Ulaya na kulazimisha sare ya 2-2.
Hapo tayari walikuwa na faida ya mabao mawili ya ugenini, na huko kwao wangeweza kulazimisha suluhu au sare ya 1-1 lakini wakacheza kana kwamba walitakiwa kulipiza kisasi cha kufungwa mabao mengi kwenye mechi ya awali.
Ni katika hali hiyo, Taifa Stars walijikuta wakilambwa bao la kwanza dakika ya kwanza tu, ambapo hali ilianza kuonekana tete kwao, na kwamba yao ilikuwa ngoma ya kitoto isiyoweza kukesha au ngozi ya kitimoto isiyowambwa ngoma.
Taifa Stars hawakuwa wazuri, tofauti kabisa na kwenye mechi ya awali naAlgeria wakutumia fursa hiyo kujipigia vya kutosha.
Taifa Stars, kwa maana hiyo, wameondoka kwa kufungwa jumla ya mabao 9-2, wazisahau fainali hizo, warudi na kujipanga upya kwa ajili ya 2022.
Mabao ya Algeria yalifungwa na mchezaji anayewania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Yacine Brahim na F. Ghoulam.
Mvua iliendelea kuwanyeshea Stars ambao washabiki wanawananga wakidai ni sawa na kupewa kifurushi cha wiki kwa wenye simu za mkononi, kwani mabao mengine yalitoka kwa wachezaji wengine, baadhi wakijipigia mawili.
Kiungo wa Stars, Mudhathiri Yahya alionesha kadi nyekundu kwa mchezo wa rafu mara mbili na kuzidi kuwanyong’onyesha Stars.
Mchezaji aliyetegemewa zaidi kwa kuzifumania nyavu, Mbwana Samatta hakuweza kubadili matokeo hayo, na hata ile dhana ya kwamba hawangekubali kushindwa bali wangefia uwanjani haikuwezekana.
Stars wanatarajiwa kurejea nyumbani leo na haijajulikana hatua gani za muda mrefu au mfupi zitachukuliwa.
Pengine sasa macho yataelekezwa kwa walioitwa Kilimanjaro Stars – Timu ya Taifa ya Tanzania Bara, walio chini ya mzalendo mwingine, Abdallah ‘king’ Kibaden aliyekuwa pia mshauri wa Taifa Stars.