in , , ,

Soka imeharibiwa isivyo kifani

Soka imeharibiwa isivyo kifani

Mchezo wa soka unapita katika nyakati za kukosa uwiano kifedha na kiushindani. Ni vipi tumefikishwa hapa na je, utawala wa matajiri mchezoni utakuwa wa kudumu?

“Hatutaki Leicester City wengi humu,” ni maneno ya mmoja wa maofisa waandamizi wa klabu zile sita zilizozoea kuwa juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) na zenye uwezo zaidi kifedha, zikijulikana zaidi kama ‘The Big Six’.

“Historia ya soka inaonesha kwamba washabiki wengi wanapenda kuona timu kubwa zikishinda mechi. Si mbaya kuwapo kiwango fulani cha kutotabirika, lakini ligi yenye demokrasia zaidi itakuwa mbaya kwa biashara,” anaongeza ofisa huyo akiwa kwenye moja ya hoteli kubwa za hapa jijini London.

Wawakilishi wa ‘The Big Six’ hawatakiwi kuwa na wasiwasi. Hawa ni wa klabu za Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur. Haiwezekani kwamba mchezo wote unaelekezwa kwenye hali ambayo klabu za aina ya Leicester – zilizo nje ya wigo wa klabu zenye msuli mkubwa kifedha zinatwaa ubingwa.

Ndiyo maana hata msimu ule wa 2015/16 Leicester walipotwaa ubingwa wa England, ilikuwa habari kubwa sana kwani hakuna aliyetarajia. Leicester walipewa nafasi ndogo sana ya kutwaa taji licha ya kuwa na mserereko wa ushindi kwenye mechi zao.

Rais wa zamani wa Real Madrid, Ramon Calderon alipata kusema kwamba soka wakati wote iekuwa namna hiyo, na huo ndio ukweli. Mambo yanabadilika kadiri muda unavyokwenda na inavyoonesha si ajabu ya kale yasijirudie kama uchunguzi huu unavyobainisha.

kundi dogo la klabu tajiri zinalindwa kifedha hivyo kwamba zinashinda mechi nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali, tena kwa idadi kubwa ya mabao, zikivunja rekodi za zamani na kuutanua mchezo hivyo kwamba imebidi wote wabadilike kuelekea huko.

Hayo ni matokeo ya mlipuko wa fedha kwenye gemu, ikimaanisha kwamba unahitaji walau kima cha chini cha mapato ya mwaka (€400m mwaka 2020, tukienda kwa takwimu za Deloitte) ili walau kuanza kushindana.

Kwa upande mwingine, pale klabu kama Liverpool au Manchester City wanapoongeza kwa kiasi kikubwa mapato kupitia intelijensia basi matokeo yake kutakuwa na tofauti kubwa. Tafsiri yake ni kwamba wigo unazidi kuwa mkubwa hata uwanjani. Ndiyo maana sasa tunaona rekodi nyingi za kihistoria zikivunjwa msimu baada ya msimu.

Kwa muongo uliopita pekee, unaowakilisha kupanda kwa ukweli kwa klabu tunazoweza kusema ni ‘super-clubs’ pamoja na kiasi kikubwa cha fedha, ulishuhudia klabu moja ikitwaa makombe matatu ndani ya msimu mmoja ambapo kwa Hispania ilikuwa mara ya pili, Ujerumani mara ya kwanza sawa na Italia; England ilikuwa makombe ya nyumbani kwa mara ya kwanza wakati kwa Ufaransa ilikuwa kwa mara ya nne.

Muongo ulishuhudia kwa mara ya kwanza timu ikifikisha idadi ya alama 100 kwenye ligi ya nyumbani katika msimu mmoja nchini England, Hispania na Italia. Msimu wa ‘Invicibles’ ulijirejea kwa Italia, Ureno, Uskochi, Italia na katika ligi nyingine saba za Ulaya.

Ligi 13 kati ya 54 za Ulaya zinashuhudia timu fulani zikienda bila makombe kwa muda mrefu zaidi au moja ikitawala sana. Kubwa ni kwamba ilitokea klabu moja ikatwaa ubigwa wa Ulaya kwa miaka miaka mitatu mfululizo, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 42.

Mengi ya mambo kama haya yalidhaniwa kwamba hayawezekani kwa miongo kadhaa lakini yametokea kwenye muongo mmoja tu uliopita, kukiwapo matuimaini ya mengi zaidi kuja. Haina hata haja kueleza kwamba mafanikio hayo yamechukuliwa na klabu tajiri zaidi kwenye mashindano hayo. Kikolezo cha fedha kimekoleza ubora wa kiwango na hivyo mafanikio.

Hii si kusema kwamba hapatakuwapo wanaosogezwa pembezoni na kuwa kama wageni, kama misimu ya karibuni wanakopita kwa tabu Manchester United au Arsenal au kwamba hawatakuwapo wasiotarajiwa wala hawajawekeza wanaochanua – kama Leicester.

Madhali ni wanadamu wanahusishwa kwenye soka, lazima kutakuwapo kupanda na kushuka. Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin alizungumzia suala hilo kwa mapana na marefu, akieleza vitisho na hatari za utandawazi unaojadidishwa na tofauti kubwa ya mapato kwa klabu.

Zaidi sana pale linapkuja suala la Deloitte’s Football Money League – onyo likitolewa juu ya utokeaji wa hali ambayo matokeo ya uwanjani yana msingi ulioegemea na kusababishwa mno na rasilimali fedha zilizopo kwa baadhi ya klabu. Hiyo inaelezwa kwamba ni hatari sana kwa uadilifu na kutotabirika kwa thamani na tunu ya muda mrefu ya gemu hii.

Rais wa La Liga, Javier Tebas, anaiweka katika ukali zaidi akisema: “Tusiporekebisha tatizo hilo sasa, ndani ya muda mfupi sekta ya soka itaporomoka na kuanguka.” Hii inasababishwa na mambo kadhaa yanayozunguka sekta yenyewe, ikiwani pamoja na hali mbaya ya kifedha kwa klabu zilizo nje ya uzio, mvutano baina ya klabu kubwa na hizo nyingine, lakini pia mvutano baina ya Uefa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Upo pia mvutano na uhasama kati ya maslahi binafsi na yale ya pamoja kiasi kwamba yanaharibu taaluma ya soka.

Miaka ile ya ’80 mambo yalikuwa tofauti sana. Fedha hazikuwa zikimwagwa kama sasa. Ligi Daraja la Kwanza England – kama ilivyoitwa wakati huo, ilikuwa na mkataba wa televisheni wa pauni milioni 5.2 tu na haki za jumla kimataifa zilikuwa £50,000 tena kutoka Skandinavia.

Fungu la mishahara kwa klabu tajiri zaidi lilikuwa pungufu ya mara tatu ya ile masikini zaidi, ikimaanisha kwamba kulikuwapo wakati wachezaji waliolipwa vyema zaidi England – Michael Robinson na Steve Foster – wote walikuwa wakichezea klabu za Brighton na Hove Albion.

Kadhalika ilimaanisha kwamba klabu 13 zilikuwa na uwezekano wa kumaliza msimu wa ligi katika nafasi nne za juu kwenye msimamo nchini England, 12 nchini Hispania na timu za Aston Villa, Steaua Bucharest, PSV Eindhoven na Red Star Belgrade zingeweza kuitwaa ubingwa wa Ulaya. Soka ilikuwa sekta ndogo sana tofauti na sasa ambapo wachezaji ndio wanalipwa zaidi ya wanataaluma wengine na mikataba ya biashara, matangazo na televisheni imekuwa ya kiasi kikubwa sana cha fedha.

Tazama kima cha haki za matangazo ya televisheni EPL kwa kipindi cha 2019-2022; thamani yake ni £8.4bn. zawadi za jumla kwenye UCL ni €2.04bn, zikipanda kutoka €583m miaka 10 tu iliyopita. Nguvu hizo zimeshuhudia Manchester United wakipanda kutoka mapato ya £117m mwanzoni mwa milenia hadi £627.1m msimu wa 2018-19. Miongo kadhaa iliyopita, klabu kubwa zilikuwa saizi ya maduka makubwa ya mjini kwao.

Tukirudi kwenye mishahara, utandao kutoka chini hadi juu kwenye EPL umetoka 2.85x kwenye msimu wa kwanza 1992-93 hadi 4.7x mwaka jana. Huko Hispania mvutiko umekwenda mbali zaidi hadi 17.2x, na kwenye ligi nyingine za kati kama Uswisi ni zaidi ya 20x.

Hili ni muhimu kutazama kama wanavyosema kwa kurudia watafiti Stefan Szymanski na Tim Kuypers – hali hii inaathiri matokeo kwa kiasi kikubwa kuliko mambo mengine. Hapo hujazungumzia ununuzi na uuzaji wa wachezaji.

Katika kitabu chake ‘The Ball Doesn’t Go In By Chance’ Mtendaji Mkuu wa Manchester City, Ferran Soriano anadai kwamba kununua wachezaji ghali zaidi hakusababishi moja kwa moja matokeo mazuri uwanjani, bali kuwa na wachezaji wazuri kwenye timu na kuwalipa mishahara wanayostahili.

Kwa takwimu zilizopo, ni kwamba ‘The Big Six’ wanalipa asilimia 51.3 ya mishahara ya klabu zote 20 za EPL. Tofauti hiyo kubwa inaendana kwa kiasi kikubwa na matokeo na hivyo kufanya kile soka ilichokuwa – kutotabirika, kuanza kupotea, na hiyo ndiyo ‘damu kwenye mwili wa soka’.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Soka: Mkataba wa kocha una thamani ya karatasi uliochapiwa

Tanzania Sports

Soka: Maslahi ya mabepari yanavyoiua