in

Simba,Yanga zina wachezaji wenye miguu mitatu?

Simba SC

Mazoea ya soka la Bongo ni kuona timu za Simba na Yanga zinashinda  kila mechi. Mazoea hayo yapo kwa mashabiki, viongozi na baadhi ya  wadau wanaoamini kuwa timu hizo hazipaswi kufungwa katika  mfululizo wa mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara.  

INGEKUWAJE SIMBA WANGEKUWA AL AHLY? 

Hivi karibuni kiongozi mmoja wa klabu ya Simba alizungumza kwenye  redio moja maarufu nchini Tanzania akidai kuwa kwa usajili waliofanya  mabingwa watetezi Simba hawakutakiwa kufungwa na timu kama  Tanzania Prisons na JKT Ruvu.  

Kauli hiyo inamaana kuwa Simba  haitakiwi kufungwa mchezo wowote, ni sawa na Simba ilivyowahi  kuifunga A Ahly ya Misri ambayo ilikuwa na mchezaji mwenye dau  kubwa lenye uwezo wa kusajili kikosi chote cha Simba.  

Kwa kauli ya kiongozi huyo ana maana hata Simba haikustahili  kuwafunga A Ahly kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika  kwa vile mabingwa hao wa Misri wamekuwa na usajili wa nguvu. 

Hali hiyo si kwa Simba peke yao, hata upande wa Yanga viongozi  wao,mashabiki na wadau wao wanaamini kuwa haitakiwi kufungwa na  timu kama Mwadui, Biashara au Lipuli kwa vile nao wanakuwa na usajili  wa nguvu.  

yanga na simba
yanga na simba

Mara nyingi yamezungumzwa hayo kwenye vijiwe vya kahawa lakini  sasa yanaonekana wazi kutamkwa na viongozi kana kwamba timu  zingine zinakuwa hazijasajili wala kujiandaa kwa ushindani wa Ligi. 

VIPI SIMBA NA YANGA WANGEKUWA BARCELONA? 

Msimu uliopita dunia ilishuhudia mchezaji bora wa dunia na wa kipekee  aliyeshinda tuzo sita za ugwiji wa soka, Lionel Messi alikuwa sehemu  ya kikosi cha Barcelona kilichochakazwa kwa mabao 8-2 kwenye  mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.  

Barcelona walipokea kipigo hicho kutoka kwa Bayern Munich ambao  walifanikiwa kutwaa taji hilo. Barcelona wanakumbuka kutandikwa  mabao 4-0 ndani ya dimba la Anfield na Liverpool ambao walikua kuwa  mabingwa wa Ulaya.  

Barca walifungwa mabao hayo licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3- 0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nyumbani kwao Camp Nou.  Barca licha ya kuwa na mchezaji bora dunia, lakini Messi hakuzuia  kipigo cha timu yake na wala hatukusikia kuwa hawakustahili kufungwa  nao.  

Kwamba Barcelona waliona kipigo hicho ni ujumhe wa kawaida kwenye  mchezo wa soka ambapo kila timu inakuwa imejiandaa na hivyo  walizidiwa maarifa pamoja na kutakiwa kujipanga upya.  

Kwenye mchezo wa El Clasico Barcelona wakiwa nyumbani walipigwa  mabao 3-1 wakiwa na Lionel Messi. Kwenye Ligi Kuu Hispania si  jambo la ajabu kuona Barcelona wakipokea vichapo kutoka kwa  wengine.  

KAMA SIMBA NA YANGA ZINGEKUWA REAL MADRID 

Klabu ya Cadiz ni ndogo mno katika historia ya soka Hispania. Lakini  msimu huu imewashangaza maelfu ya washabiki wa soka baada ya  kuikung’kuta Real Madrid bao 1-0. 

Bajeti za Real Madrid na Cadiz ni mbingu na radhi, hazifanani hata  kidogo. Lakini hilo halikuzuia Real Madrid kuzabwa kwenye La Liga.  Kwenye historia ya soka Real Madrid iliwahi kuzabwa mabao 6-2 na  Barcelona na maisha yakaendelea.  

Vipigo vya aina yake vimetokea mara nyingi kwenye uwanja wa  nyumbani wa Real Madrid wa Santiago Bernabeu. Hilo limekuwa  sehemu ya mchezo kwani wachezaji wote wana miguu miwili na tofauti  zao za kiuchumi na uwezo bado haziwezi kuandaa matokeo ya mchezo.  

YANGA,SIMBA WANGEKUWA ARSENAL? 

Kipigo cha mabao 8-2 kimewahi kuwakumba Arsenal kutoka kwa  Manchester United. Kilikuwa kipigo cha aina yake kwenye EPL miaka  kadhaa iliyopita, lakini Arsenal walifahamu ni sehemu ya mchezo, na  wanalazimika kukubali kujirekebusha pale wanapokuwa wamezidiwa  maarifa au uwezo wa timu hizo. Vipi Yanga wangekuwa Arsenal  waliozabwa mabao 8-2? Ingekuwaje Simba ndio waliofungwa 8-2?  

Je viongozi wa soka wa Yanga na Simba wanataka kutudhihirishia kuwa  wachezaji wa timu zao wana miguu mitatu? Kwa,mba wanatakiwa  kushinda karibu kila mechi wala hawana nafasi ya kufikiri kuwa kuna  kuzidiwa kwenye mchezo wa kandanda? 

Viongozi wetu wawe chachu ya maarifa kwa mashabiki ili wajifunze  mpira katika hali halisi na ambayo itrapunguza presha na kudhani kuwa  Simba na Yanga ni timu pekee duniani ambazo zinatakiwa kushinda kila  mchezo.  

Na zaidi wachezaji wao hawana miguu mitatu na kwamba watafanya  maajabu kuliko wengine duniani. Kina Cristiano Ronaldo, Messi wana  miguu miwili iliyotamba duniani kwa miaka 15 mfululizo lakini  wameshuhudia vipigo katika timu zao. 

Pep Guardiola pamoja na sifa lukuki alizonazo amewahi kutandikwa  mabao 5 katika mchezo mmoja. Ni jambo la kawaida, kwa vile  wachezaji wake wana miguu miwili tu. Hivyo basi wachezaji wa Simba  au Yanga ni binadamu kama wengine. 

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Wabongo Hawana Shukrani Kwa Kiduku

cedric kaze

Tathimini za Kaze kazini Yanga