MABAO mawili ya wapinzani wa Simba si jambo la kushtusha kwa sababu klabu hiyo imewahi kusawazisha na kuibuka na ushindi. Mechi nyinbgi ambazo Simba wamecheza katika kutafuta matokeo ya kuvuka kwenye hatua ya mtoano, wamefanikiwa kuibuka na ushindi katika mazingira magumu kuliko hata mchezo wa sasa. Ushiriki wa Simba kwenye mashindano ya CAF umeonesha namna ulivyopitia ushindani mkali na uwezo wao katika kupindua meza. TANZANIASPORTS inakuleta hoja za msingi ambazo zinaweza kuwapa Simba nafasi ya kupindua meza kwenye mchezo wao wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Wapinzani wao wa karibu
Kama ulikuwa hujui basi Simba na RS Berkane zina ushindani mkali nje ya uwanja katika kutafuta hadhi. Kwa mujibu wa shirikisho la soka la Afrika, Simba wanashikilia nafasi ya nne katika ubora wao. Ni nafasi ambayo wameipata kutokana na ushiriki wa mashindano ya Kimataifa huku wakifanya makubwa licha ya kukosa kombe. Kwa maana hiyo Simba inaendelea kujitangaza na kuweka msingi wa kusaka mafanikio zaidi barani Afrika, lakini wanakabiliana na mpinzani wao wa karibu katika viwango vya soka.
RS Berkane inashika nafasi ya tano katika ubora wa timu, ikiwa na maana imetanguliwa na Simba. Kwa maana hiyo Simba wana kila sababu ya kuwashinda wapinzani wao hao mara mbili ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Simba wana kila sababu ya kuwahakikishia wapenzi wao kuwa hawakuwa nafasi ya 4 kwa ubora kwa bahati mbaya, na hivyo wanataka kuidhihirishia Afrika kuwa Berkane kwao itabaki kuwa nafasi ya 5. Kusawazisha mabao 2-0 waliyofungwa katika mchezo uliopita ni jambo linalowezekana kwa Simba.
Ubora wa mshindani, meza ni ya Simba
Unawza kuwasifia RS Berkane kwa kila kitu. Unaweza kusema ni timu imara na imecheza na Simba kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho ikiwa inatoka kuzifunga mabao ya kutosha timu shindani. Lakini mbele ya Simba RS Berkane ilipambana kwa nguvu na maarifa kusaka mabao zaidi lakini ikaambulia ushindi wa mabao 2-0. Katika dakika 90 za mchezo huo utakaofanyika kwenye dimba la Amani visiwani Zanzibar, Simba watakuwa na kazi ya kurudisha mabao 2 ili kuwa sare ya 2-2 ili kutafuta ushindi. RS Berkane wanasifiwa kwa kucheza kitimu kuanzia kujilinda hadi kushambulia, hata hivyo Simba wana kila sababu ya kuhakikisha wanaifunga timu hiyo kwneye fainali hii. Hatua ya kwanza wanayotakiwa kukabiliana nayo ni katika mipira ya adhabu ndogo kwani zimeonesha zinaweza kuleta madhara katika lango la Simba. Pia katika mshindani huyu ameonesha bayana kuwa anafungika kwa sababu aliruhusu kushambuliwa mara kadhaa. Hivyo basi hatua ya kwanza ni kuifanya kuwa makini katika kuzuia na kushambulia. Uwiano wa pande hizi mbili utasaidia Simba kukabiliana na mshindani huyu mzuri.
Kutumia makosa
Simba waifungwa bao la pili na RS Berkane kwa sababu ya makosa yaliyokuwa yamefanywa na kiungo waka Yusuf Kagoma katika kumiliki mpira vyema. Haya ni makosa binafsi yaliyoigharimu timu lakini hayakuwa matokeo ya kuishusha timu katika ari ya ushindi. Safu ya ulinzi ya Simba inatakiwa kuhakikisha inacheza mitindo yote; kumkaba mchezaji mmoja mmoja na kuzuia kwa kuzingatia pande (zonal marking). Katika mazingira hayo RS Berkane hawatumii mawinga kwa wingi, bali wanatumia pasi ndefu na kukimbia kutoka nyuma kwenda mbele. Wachezaji wao wa pembeni ni washambuliaji wa kati kwa maana ya kwamba kocha wao amewaondoa mawinga halisi na kuwapa majukumu washambuliaji kutumia maeneo ya pembeni kuingia eneo la hatari. Muundo wa RS Berkane unatokana na viungo wengi kuliko wachezaji wa kushambulia lango la adui. Kwa maana hiyo Simba wanapaswa kutambua kuwa makosa wanayofanya yanatumiwa na wapinzani wao kuwaumiza, na wao wanapaswa kutumia makosa ya wenzao kuibuka na ushindi. Mfano RS Berkane si wazuri katika ‘one on one’ kwenye eneo lao la ulinzi, lakini endapo watapangiwa mshambuliaji mmoja wa kupewa pasi za juu ili apambane na mabeki wa Berkane itawawia rahisi mno kuzuia. Hivyo Simba wanatakiwa kuingia kama nyuki eneo la 18 la Berkane na kupigiana pasi fupi fupi za haraka ili kuwavuruga wapinzani wao.
Kupunguza kujisahau
Mchezo wa soka ni dakika 90. Kila dakika au sekunde ina umuhimu wake. wachezaji wa Simba wanatakiwa kuzingatia sana hili, ili wapunguze kujisahau katika mchezo huu wa pili. Mfano wakati golikipa anaanzisha mpira kwenda kwa mcehzaji mwenzake, wachezaji wa Simba hasa wa ulinzi na viungo hawakuwa na utayari kuhusiana na hatari inayoweza kuwakumba na hivyo wakajikuta wanafungwa bao kirahisi. Wachezaji wa eneo hilo wanapaswa kuongezewa dozi ya umakini ili waweze kulinda nembo ya Simba na kuwakilisha vema Tanzania pamoja nafamilia zao kwenye mashindano ya Soka. Katika hali hiyo kila idara ya Simba uwanjani inapaswa kucheza kwa ajili ya mwingine kwa maana ya kusaidiana ili kuipa ushindi klabu yao.
Hatari ya dakika 15
Aina ya mchezo wa RS Berkane ni ule wa kuwashughulikia wapinzani wao ndani ya dakika 15 ili kuwavurugia mbinu zao. Dakika hizo ndizo wanazotumia kutafuta mabao kwa udi na uvumba ili wapinzani watakapokuja kukaa sawa wanakuwa wamechelewa. Kwa maana hiyo dakika 15 za mchezo zitakuwa muhimu na kuamua nani anaweza kulinda lango lake bila kutikiswa. Na kikatika dakika hizo Simba wanatakiwa kuhakikisha wanapata mabao mawili safi ili kuweka mchezo katika sare. Hakuna linaloshindikana.
Comments
Loading…