VYOVYOTE unavyoweza kusema, lakini ukweli ni kwamba timu ya taifa ya Brazil haina makali kama yaliyozoeleka miaka ya nyuma. Nchi hiyo ina jumla ya watu milioni 212. Kama ni ubingwa wa Dunia mara ya mwisho wametwaa mwaka 2002. Mataji ya Kimataifa yamekauka mno. Umahiri wao umeshuka. Wachezaji wao wengi si wale wa Daraja la juu la akina Ronaldinho, Ronaldo De Lima na kadhalika. Katika soka la Kibrazil, sifa kubwa ni Samba. Miaka mingi Samba limepotea na kushindwa kuibuka na mafanikio.
Tite ndiye kocha alyejaribu kuimarisha timu hiyo, lakini iliishia robo fainali ya Kombe la Dunia katika fainali zilizopita. Kwa msingi huo ujio wa kocha mpya Brazil una maana kubwa na mzigo ni mkubwa sana, kiasi kwamba maelfu ya mashabiki wanataka kuona kila kitu kinafanyika vizuri na kuwarudishia furaha yao iliyopote.
Kiushawishi, Brazil bado wana ushawishi mkubwa katika soka duniani kwa sababu ni mabingwa mara tano ya Kombe la Dunia na ambapo Mataifa mengine hayajafikia rekodi hiyo. Ili kurudisha ufalme wao, Brazil inahaha kila kukicha na sasa imetangaza kumwajiri kocha wa kigeni kutoka Italia, Carlo Ancelotti ambaye anafundisha Real Madrid ya Hispania. Kibarua ya Carlo Ancelotti kinatarajiwa kuanza mapema Mei 26.
Kwa sifa zake za timu bora duniani, Brazil inakabiliwa na shinikizo kubwa la kuhakikisha inarejesha makali yake. Kwenye fainali za Copa Amerika, Brazil haikufua dafu kwani iliishia robo fainali. Kisha katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia, Brazil waliambwa mabao 4-1 kutoka Argentina hali ambayo ilisababisha kibarua cha kocha Dorival Junior kuota mbawa na timu kuanza mchakato wa kumpata kocha mpya hadi walipoinasa Saini ya Ancelotti. Kocha huyo amekuwa akihusishwa na nafasi hiyo kwa kipindi kirefu, kwani Ednaldo, rais wa chama cha soka cha Brazil (CBF) alitangaza bayana kutamani kuona Mwalimu huyo anakiongoza kikosi chao.
Kana kwamba haitoshi hata Ronaldo De Lima ambaye alikuwa anataka kugombea urais wa CBF alitangaza kuwa endapo angechaguliwa angemwajiri Carlo Ancelotti kuwa kocha wa Brazil. Haijulikani ni sababu zipi za ndani zilizochangia kumwajiri kocha huyo, lakini zile za nje zinajulikana kuwa ametwaa mataji mengi katika nchi tofauti. Pengine jambo la nyongeza ni kwamba amewafundisha wachezaji wengi wa Kibrazil hivyo anafahamu tabia zao, soka lao, na namna ufundi wao ulivyo. Kuanzia akiwa mchezaji hadi AC Milan, kisha Chelsea, Everton, na PSG lakini hakuwahi kufundisha timu ya taifa. Pengine isiwe sababu lakini kwa hakika kibarua cha Carlo Ancelotti ni kikubwa sana.
Uwezo wao wa kujiamini umepungua kwa kiasi kikubwa ingawaje siku zote inatarajiwa kuona Brazil inayojiamini kutokana na historia yao. Kwa mujibu wa wachambuzi mbalimbali wanaamini kuwa Brazil imepungua kujiamini kutokana na matokeo mabaya Pamoja na mafanikio hafifu waliyopata miaka ya karibuni. Wabrazil hawajihisi kuwa wanao uwezo mkubwa, hiyo inachangia kuwa katika mazingira yanayowanyima maarifa ya kuendeleza historia nzuri.
Ukiwa umebaki mwaka mmoja kabla ya fainali za Kombe la Dunia kufanyika yaani mwaka 2026 lakini kwa upande wa Brazil hawaonekani kuwa tayari kimashindano. Kwanza hawana timu ya uhakika ambayo inaweza kushindana na mataifa mengine. Kukosekana na kwa kikosi cha uhakika cha kuibuka na ushindi ni sababu mojawapo inayowafanya wawe katika nyakati mbovu. Jambo linguine linalowang’arimu ni kukosa mbinu sahihi za kuivusha mbele timu hiyo. Brazil hawaonekani kuwa mabingwa kimbinu katika soka miaka ya karibuni, kutokana na kukosa aina ya wachezaji wao Pamoja na msingi wa kutafuta mafanikio.
Kwa mfano katika safu ya ulinzi wanakabiliwa na wachezaji wasio na viwango vya juu. Hata wale ambao wana viwango vya juu bado hawaonekani kuwa suluhisho katika timu yao. Marquinhos ni nahodha wa PSG na mmoja walinzi wazuri katika Ligi Kuu Ufaransa na Ulaya. Gabriel Magalhaes wa Arsenal anaonekana kuwa mlinzi mzuri sambamba na Eder Militao wa Real Madrid. Lakini walinzi wote hawo wanaotegemewa Ulaya wameshindwa kuwa nguzo muhimu ya mafanikio katika timu ya Taifa. Kati ya wachezaji 65 waliofanyiwa majaribio katika safu ya ulinzi tangu fainali za Kombe la Dunia za Qatar bado hawajaonesha umahiri unaoweza kuwafanya wabakizwe kwenye kikosi cha Brazil. Hivyo kuhitimisha kuwa Brazil wanalo jukumu kubwa la kutafuta suluhisho la muda mrefu mbali ya kuajiri kocha wa kigeni.
Kuanzia Januari mwaka 2023 hadi Mei 2025 wamekuwa na makocha watatu tofauti. Kila kocha anakuwa na mbinu ambazo hazizalishi matokeo mazuri kwa Brazil. Ni hali ambayo inawagharimu kila kukicha.
Kuwakosa baadhi ya wachezaji muhimu ni jambo ambalo liliwagharimu. Mfano Bruno Guimaraes anatarajiwa kurudi kikosini baada ya kutumikia adhabu. Hivyo kiungo huyu wa Newcastle United anatarajiwa kucheza mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia mwaka 2026. Ujio wa Carlo Ancelotti maana yake Carlos Casemiro atarudishwa kundini katika safu ya kiungo.
Safu ya ushambuliaji nayo inakabiliwa na changamoto. Katika klabu ya Real Madrid, wachezaji wawili tegemeo ni rai awa Brazil; Vinicius Junior na Rodrygo Goes. Wachezaji hawa wanaunda safu ya ushambuliaji ambayo inategemewa pia kutumika katika kikosi cha timu ya Taifa. Mjadala mkubwa ni namna ambavyo kocha huyo atakavyowatumia wachezaji hao katikat ya rundo la atakaloita.
Mfano katika safu ya ushambuliaji atahitaji mshambuliaji nambari 9, kisha atawahitaji Raphinha, Gabrieli Martinelli, Vinicius Junior, Rodrygo Goes ambao wanacheza nafasi zinazofanana. Nani ataanzia benchi na nani atapangwa kikosi cha kwanza. Katika mazingira hayo aina ya mshambuliaji ambaye anaweza kutegemewa ni Richarlison wa Tottneham Hotspurs. Ancelotti na Richarlison waliwahi kufanya kazi Pamoja walipokuwa Everton. Mbali ya hao atakuwepo Neymar Junior ambaye anategemewa kuwa mshambuliaji namba mbili katika kikosi chao. Ukiongeza na wachezaji wengine ambao wameshindwa wameshindwa kuziba pengo la Neymar tangu mwaka 2010. Nyota huyo atampa kibarua kigumu kocha wake ili kuamua nani apangwe naye kwenye kikosi cha kwanza.
Ukitazama Brazil ya sasa, utagundua rais wa CBF, Edinaldo Rodrigues anakabiliwa na kibarua kigumu sana na ambcho kinamganya awe mpweke katika uongozi. Mtu pekee ambaye anaweza kuokoa utawala wake ni Carlo Ancelotti. Je kocha huyo ataweza kubadili mambo katika kikodi cha Brazil? Hilo ndilo swali linalotazamwa na kufikiriwa zaidi.
Comments
Loading…