in , , , ,

‘Remontada’ imeenda, maana ya Simba wangebeba !

KAMA mchezo huo unatumia lugha ya kigeni basi neno sahihi lilikuwa kusema ‘Remontada’ likiwa na maana ya kiingereza, ‘comeback’. Kama angekuwa Sir Alex Ferguson basi angetumia msamiati wake maarufu wa ‘Bouncebackability’ akiwa na maana ya uwezo wa timu kutoka nyuma hadi kusawazisha na kuibuka na ushindi. Mara nyingi misemo hiyo inakuja pale ambapo timu inahitaji ushindi ili kusonga mbele. Lakini Simba walikuwa na ‘remontada’ yao ili kutwaa taji kubwa la pili barani Afrika yaani Kombe la Shirikisho. Waswahili wangesema, Simba alipania kupindua meza, ingawaje haijapinduka lakini wameleta thamani kubwa katika mchezo wa soka na Ligi Kuu Tanzania.

Hakuna kitu muhimu katika mchezo wa soka kama ushindi. Ushindi wowote ule ambao unawapa thamani wachezaji na benchi la ufundi ni sehemu ya mafanikio. Lakini kushindwa katika mazingira yaliyoshuhudiwa kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar bila shaka yoyote kuwa Simba wangebeba na wana kila sababu ya kubeba kombe hili msimu ujao. 

Maelfu ya watazamaji waliojazana kwenye uwanja wa Amaan waliwapigia makofi wachezaji wa Simba kama ishara ya kuwapongeza na kuwashukuru kwa hatua waliyofikia. Simba ilikubali kulikosa kombe la Shirikisho baada ya kulazimishwa sare 1-1 na wageni wao RS Berkane. Wakati Simba akihitaji kuongeza bao la pili ili kusawazisha mwamuzi wa mchezo alimlima kadi nyekundu kiungo mkabaji wa Simba Yusuf Kagoma.

TANZANIASPORTS katika uchambuzi wa picha mjongeo wa tukio hilo unaonesha kuwa mwamuzi angeweza kumpa onyo la mdomo Yusuf Kagoma kuliko kuiharibu fainali nzuri na ya kuvutia ya Kombe la Shirikisho kuliko hata ile iliyotangulia ya mchezo wa kwanza kati ya Mamelodi Sundowns na Pyramids ya Misri kwenye dimba la Loftus Versfiedl jijini Pretoria.

Dakika 45 za kwanza

Simba waliuanza mchezo huo kwa kasi ya kawaida tu lakini walionesha thamani kwanini wamefika hatua hiyo. Uchezaji wao ulikuwa katika msingi wa kutafuta bao. Simba walicheza soka la kikubwa ambalo lilikuwa kivutio kutazama na usingedhani hilo ni kombe la pili kwa umaarufu baada ya Ligi ya Mabingwa. Kocha Fadlu Davids alimweka benchi winga wake Kibu Dennis na nafasi yake akampanga Joshua Mutale. 

Mpango wa kocha Fadlu ulikuwa kucheza kwa kasi kubwa, huku Joshua Mutale akifahamika kwa mchezo huo. Alimhitaji Joshua Mutale kukimbizana na RS Berkane ili kuwarudisha nyuma zaidi. Katika boksi ya adui yaani ndani ya 18 za RS Berkane Simba walikuwa na ingizo la wachezaji watatu; Jean Ahoua, Stephen Mukwala na Joshua Mutale. Watatu hao walitengeneza kombinenga ya hatari. Katika mfumo wa viungo wawili wa ulinzi, mgawanyo wa majukumu ulikuwa Yusuf Kagoma kulinda na Frabrice Ngoma kushambulia. 

Refa, VAR katika Dakika 45 za mwisho

Simba waliingia kipindi hiki wakiwa na nia moja tu, kutafuta bao la kusawazisha. Lakini juhudi zao ziliishia mikononi mwa refa wa mchezo huo ambaye alipomlima kadi nyekundu Yusuf Kagoma ilikuwa na maana kuwapa ahueni wageni RS Berkane na kuwaweka katika wakati mgumu Simba. Simba kwa muda mwingi wa mchezo walicheza wakiwa na pungufu, lakini ari yao ya kusaka bao ilizaa matunda pale walipotumbikiza mpira kimyani kupitia kwa Stephen Mukwala, lakini mwamuzi alijulishwa kuangalia marudio kabla ya kufungwa bao hilo. Kwa kutumia teknolojia ya VAR, mwamuzi aliwasikiliza wenzake waliooko kwenye chumba cha ukaguzi na hivyo wakamweleza bao hilo halikuwa halali kwakuwa mfungaji alikuwa ameotea. Hivyo basi refa akafuta bao hilo ambalo lilikuwa na pili kwa Simba wakiwa pungufu. Mwamuzi wa mchezo huo alipoteza ladha kwa kutoa kadi nyingi bila kuanza na onyo kwa wachezaji na benchi la ufundi, hali ambayo iliharibu utamu wa fainali hiyo.

Kuzaliwa Joshua Mutale

Kasi kubwa, uwezo wa kukaa na mpira, kuwapunguza wapinzani na bao la kuongoza kisha kupewa mchezaji bora wa mchezo, ilionesha wazi kuwa Joshua Mutale alikuwa tayari kuwadhihirishia watanzania kuwa hakusajiliwa ilia je kuwa msindikizaji. Uwezo wa kupiga chenga, kuomba nafasi na kutoa nafasi, pamoja na kucheza kitimu ilimwezesha Joshua Mutale kuonesha makali yake katika mfumo wa kushambulia wa 4-3-3 akicheza kwa ukaribu na Jean Ahoua na Stephen Mukwala. Ingawaje Simba wamelikosa kombe hili, lakini watanzania wameona kipaji kikubwa cha Joshua Mutale.

Kukua soka la Tanzania

Unaweza kuwacheka Simba lakini ukweli ni kwamba soka la Tanzania linapiga hatua. Mwaka 1993 Simba walipofika fainali ilikuwa kama nasibu. Lakini soka la Tanzania likapotea tena hadi mwaka 1998 baada ya Yanga kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kisha mwaka 2003 Simba kutinga robo fainali. 

Klabu za Tanzania zilikuwa zinapitia nyakati ngumu kwenye mashindano ya CAF na hazikuwa zikipewa nafasi ya kufanya vizuri. Hata hivyo kwa miaka takribani 10 sasa, klabu za Soka za Tanzania zinazidi kunawiri na kuchanua Kimataifa. Simba wamekuwa wakitinga robo fainali za Ligi ya Mabingwa mara nyingi na robo fainali Kombe la shirikisho. Lakini msimu huu Simba wamefika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho na kudhihirisha Ligi Kuu Tanzania ni moto wa kuotea mbali. Hali kadhalika watani wao wa jadi Yanga walitinga fainali ya Kombe la Shirikisho na kuonesha kuwa soka letu linazidi kuchanja mbuga hatua kwa hatua.

Kombe la Pili

Kwa mara ya kwanza klabu ya Simba ilileta kombe la CAF mwaka 1993 wakati ilipocheza fainali na Stella Abdijan ya Ivory Coast kwenye Kombe la Abiola. Simba wameweka rekodi ya pili kulileta kombe la mashindano ya CAF nchini. Hii ni mara ya kwanza kwa  uwanja wa Amaan Zanzibar kuwa mwenyeji wa mchezo wa marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho. Mara kwanza mchezo wa marudiano kati ya Simba na Stella Abidjan ulichezwa kwenye uwanja wa Uhuru (ambao zamani uliitwa uwanja wa Taifa).

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

58 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Simba wana kila sababu kupindua meza

Tanzania Sports

Mamelodi Sundowns hawajui kumaliza mechi