in

Simba siyo sehemu sahihi kwa Ndemla

Ndemla

Natamani kumuona Said Khamis Ndemla akicheza mara kwa mara. Hii ndiyo tamaa yangu kwa sasa kila nikimuona Said Khamis Ndemla.

Inawezekana Simba ndiyo sehemu ambayo kipaji chake kilizaliwa , kikakuzwa na kulelewa vyema lakini cha kusikitisha ndiyo sehemu ambayo kipaji chake hakitumiki vyema ndiyo maana natamani kumuona Said Khamis Ndemla akicheza mara kwa mara.

Natamani kumuona kwa sababu miguu yake kwa sasa ina thamani kubwa ya kupata dakika nyingi uwanjani za kuonesha kiwango chake kuliko kupata dakika nyingi za kukaa benchini.

Ameongeza mkataba mpya na Simba. Kitu ambacho ni kizuri , Lakini angefikiria namna ambavyo anaweza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Hili ni swali kubwa ambalo linatakiwa kuanzia na neno wapi.

Wapi anaweza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ? Simba ? Simba ambayo kila sehemu ambayo unagusa kuna wachezaji wa moto ambao ni ngumu kuwatoa ni suala gumu.

Simaanishi kuwa Said Khamis Ndemla hana uwezo wa kugombania namba akiwa Simba lakini aina ya wachezaji waliopo Simba ni ngumu kwa Said Khamis Ndemla kupata nafasi mbele yao.

Said Khamis Ndemla anacheza nafasi mbalimbali kwenye eneo la kiungo cha kati. Eneo ambalo kwa kiasi kikubwa lina utajiri wa vipaji vikubwa ndani ya timu ya Simba.

Unategemea kumuona Said Khamis Ndemla akimtoa Jonas Mkude katika eneo la kiungo cha kuzuia ? Eneo ambalo Said Ndemla anaonekana kama chaguo la tatu ?

Unategemea kumuona Said Khamis Ndemla akimtoa Fraga? Au unategemea Said Khamis Ndemla amtoe Lary Bwalya? Kiungo ambaye kwa sasa kila mwana Simba anatamani kumuona akiwa uwanjani?

Unategemea Claoutus Chota Chama aporwe namba na Said Khamis Ndemla? Ni maswali ambayo ni magumu, maswali ambayo yanaambatana na neno , wapi Said Khamis Ndemla anaenda kucheza ndani ya kikosi cha Simba.

Wengi tunampenda sana Said Khamis Ndemla. Wote tunatamani kumuona Said Khamis Ndemla akicheza mara kwa mara kwa sababu tunaamini anakipaji kikubwa lakini swali gumu linalokuja kwetu ni wapi atacheza mara kwa mara ?

Huwezi kumtoa Said Khamis Ndemla kwake yeye anaamini ndiyo sehemu sahihi. Inawezekana ikawa sehemu sahihi kimaslahi. Lakini ukweli ni kwamba siyo sehemu sahihi katika kuendeleza kipaji chake.

Anaweza asiondoke Simba, lakini akaomba nafasi ya kwenda kwa mkopo sehemu ambayo atapata namba mara kwa mara. Said Khamis Ndemla yuko kwenye umri ambao anatakiwa kucheza mara kwa mara.

Yuko kwenye umri ambao anatakiwa kumshawishi kocha wa timu ya taifa kumchagua kwenye timu ya taifa. Huwezi kumshawishi kocha wa timu ya taifa ukiwa sehemu ambayo wewe ni chaguo la tatu.

Anatakiwa kwenda sehemu ambayo atakuwa chaguo la kwanza. Aoneshe uwezo wake.  Naamini kupitia uwezo wake kuna nafasi kubwa ya yeye kuitwa timu ya taifa na Simba kutamani kumrudisha tena kwenye kikosi chake.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
PSG

Neymar, Mbappe na Di Maria ni MSN ndani ya PSG

Leeds United

Leeds United kubebwa tena na uchawi wa Bielsa?