Timu ya soka ya Simba inasubiriwa kutegua kitendawili cha ubingwa ligi kuu ya soka Tanzania Bara mkoani Mbeya, endapo itafanikiwa kupata alama mbili tu na haziwezi kupatikana sharti washinde mchezo huo.
Mwishoni mwa wiki hii Simba SC itacheza mchezo wa mwisho mkoani Mbeya wa ligi kuu Tanzania Bara kabla ya kugeukia mashindano ya FA.
Ni Juni 28 watarejea tena katika uwanja wa Sokoine kucheza dhidi ya Tanzaniaa Prisons.
Simba kwa sasa inahitaji alama 2 tu iweze kutangaza ubingwa wa ligi ya Tanzania Bara kwa misimu mitatu mfululizo je wataweza kuwabangua wanajeshi wana wajerajera? Swali ambalo watalijibu wenyewe.
Katika mchezo huo tunaweza kusema ‘do or die’ mana wakishinda watatawazwa kuwa mabingwa wakitoa sare basi itawabidi wasubiri alama moja nyingine.
Hii ilitokana na washindani wake wakaribu Azam FC na Yanga kuboronga katika michezo yao iliyotangulia.
Ambapo kama Azam ikishinda michezo yote itakuwa na alama 79 huku Yanga nayo ikishinda itafikisha alama 78 na Simba yenyewe hadi unasoma habari hii ina alama 78.
Azam FC walianza kwa kipigo cha goli 1-0 dhidi ya Kagera Sugar wakati huo Yanga wametoa sare magoli 2-2 dhidi ya Namungo FC mchezo uliopigwa uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Katika michezo mitano ya mwisho ya Simba wamepoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga wakivuna alama 10 kwa maana ya kushinda michezo mitatu na kutoa sare mmoja dhidi ya Ruvu Shooting.
Katika michezo 31Simba SC imeshinda mara 25 sare tatu imefungwa michezo mitatu , timu hiyo imefunga magoli 69 na kufungwa michezo 16, magoli 69 kutoa 16 utapata magoli 53 ni mengi zaidi ya timu zote msimu huu. Kwa magoli hayo Simba inaweza kugawa kwa Mbao FC na Singida united bado yatabaki.
Ni wakati ambao wanaweza wakatengeneza fulana za ubingwa mapema maana inawezekana kabisa ikawa siku ya furaha jumamosi ya Juni 28 pale katika uwanja wa Sokoine.
Wapinzani wake Azam FC imekusanya alama kumi katika michezo mitano ya mwisho ambapo wameshinda michezo 3 sare moja dhidi ya Yanga na kufungwa mmoja dhidi ya Kagera Sugar.
Katika michezo mitano ya Yanga imeshinda mchezo mmoja huku ikitoa sare mara nne katika mikikimiki ya ligi kuu Tanzania Bara.
Katika timu ambayo imefanya vibaya zaidi miongoni mwa timu 20 VPL ni Singida United ambayo imefungwa michezo mitano na kushinda mmoja. Ndio timu ambayo imefungwa 54 ni mengi zaidi kuliko nyinginee yoyote huku ikifunga magoli 17 ni machache zaidi kuliko timu nyingine yoyote.
Simba SC inaweza kumaliza presha mkoani Mbeya ili sasa ijikite katika michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambapo mchezo wao wa robo fainali watakutana na Azam FC ambayo nayo itakuwa na hamu kushinda ili isonge mbele katika hatua inayofuata.
Inawezekana ni wakati muafaka wa kumaliza kazi ili ijiandae vyema, lakini timu inayokutana nayo Tanzania Prisons iko nafasi ya 10 ikiwa na alama 42, ni timu ambayo inaweza kufanya jambo lolote na wakati wowote. Timu hii imekua ikizisumbua Simba na Yanga kwa misimu ya hivi karibuni.
Katika michezo mitano ya mwisho imeshinda michezo 2 imetoa sare 2 na kufungwa mmoja safu ya ushambuliaji imepata magoli 29 huku upande wa ulinzi umeruhusu magoli magoli 23, timu hiyo imeshinda michezo 9, imepoteza michezo 7 na kutoa sare 15.
Tanzania Prisons huwa inacheza vizuri sana na mbungi itapigwa sana siku hiyo kikubwa tusubiri na kuweza kuona nani ataibuka na ushindi.
Bado tunarudi nyuma ni kweli Simba itategua kitendawili cha ubingwa ligi kuu Tanzania Bara mkoani Mbeya?
Comments
Loading…