Raha ilioje ukienda kuandika katika gugo ‘Google’ jina la nyota wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta linatokea vizuri huku Wikipedia yake ikiandikwa habari za kweli juu ya maisha yake ya soka.
Unajisikiaje kuona ndugu yetu huyu anafanya vizuri kule England katika timu ya Aston Villa.
Nafikiri dua nyingi sana zinamuendea nyota huyo ili aweze kufanya vizuri, uzuri wake Wabongo wako vizuri katika mitandao ya kijamii katika kukishabikia chao kiwe kizuri au kibovu.
Hajafika bure bali juhudi binafsi zimemfanya afike huko alipo hata ukiangalia namna alipopitia unaona alikuwa ‘serious’ kiasi gani hadi kutusua.
Ndio maana wanaobana wachache ila wanaomuombea dua njema ni wengi mno.
Wakati tunaendelea na kumalizia stori yetu na mwanariadha nguli Tanzania Gidamis Shahanga naye alikuwa na neno lake juu ya mchezaji huyo ambaye siku ya jumatano timu yake itacheza na Sheffield United katika kiporo hii baada ya tamko la kurejea kwa ligi kuu England baada ya COVID-19.
Shahanga ameweka wazi kuwa Mbwana Samatta anastahili pongezi na kuheshimiwa kwa juhudi zake hadi kufika hapo alipo, naye ameungana na Watanzania wengine kuweza kumtakia mafanikio mchezaji huyo.
“Samatta anatakiwa kupongezwa kwa juhudi zake, naamini atazidi kufanya vizuri zaidi ya hapa alivyo sasa, hii inatokana na juhudi zake binafsi pamoja na nidhamu zake,”alisema.
Nguli huyo wa riadha amewataka wanaomponda juu ya uchezaji wake na wanaotaka kuona maendeleo ya haraka kwa Samatta wapunguze munkari wanatakiwa wafahamu kuwa ataendelea vizuri na atafanya makubwa huko mbele.
Amesisitiza kuwa bado mazoea na wachezaji wenzake hajakaa sawa ila atafika pazuri kwani uwezo na nia anayo.
“Wanaohitaji mafanikio ya haraka kwa Samatta wasubiri kwanza ni mchezaji mzuri atafanya vizuri kikubwa bado hajazoeana vizuri na wenzake waache kumtukana na waambia atafanya maajabu sana,”aliongeza.
Kwa upande wangu ninaona yupo sahihi mzee Shahanga kwani hata sie tunaoingia katika vibanda umiza huwa tunaona hali ya mashabiki kutaka mafanikio ya haraka kwa nyota huyo hivyo ni wakati wa kufanya subra.
Samatta alifunga goli lake la kwanza ndani ya EPL dhidi ya timu ya Bournemouth na ameandika historia ya Mtanzania wa kwanza kufunga goli ndani ya ligi hiyo.
Pili ni Mtanzania wa kwanza kufunga goli katika uwanja wa taifa wa nchini England yaani Wembley dhidi ya Manchester City katika kombe la ligi maarufu kama Carling Cup maarufu kama EFL.
Mtanzania wa kwanza kufunga katika michuano ya klabu bingwa Ulaya maarufu kama ‘UEFA’ tena alilifunga dhidi ya Liverpool wakati huo akiitumikia KRC Genk ya nchini Ubelgiji.
Rekodi hizo zitabakia katika vitabu vya historia katika maisha yake na Tanzania kwa ujumla kwani mtangzaji Jon Champion au Peter Drury na Jim Beglin wakiitaja nchi yetu kupitia Samagoal unajisikiaje ?
Labda tujikumbushe kuwa Samatta alianza soka katika timu ya African Lyon msimu wa 2008/10.
Baada ya kuonesha kiwango kizuri msimu wa 2010/11 aliitumikia Simba na mechi yao dhidi ya TP Mazembe ya klabu bingwa ya Afrika ndio imempa ulaji na kusogea ligi ya Kongo huo msimu wa 2011/16.
Mwaka mmoja wa Simba alicheza michezo 25 na alifunga magoli 13.
Misimu mitano TP Mazembe alicheza michezo 103 na kufunga magoli 60.
Alifanikiwa kuchukua mchezaji bora wa ndani wa Afrika kabla ya tuzo hizo hazijafutwa.
Nyota imeng’aa msimu wa 2016/20 KRC Genk ya nchini Ubelgiji imemnasa na kuitumikia timu hiyo kwa mafanikio amecheza michezo 101 magoli 43.
Ndipo zikaanza tetesi kuwa anatakiwa timu hii mara ile hatimaye ametua Aston Villa ndio kwanza wa moto amecheza michezo 3 amefunga goli 1 la EPL ila pia ana goli moja EFL.
Huyo ndiyo mbwana Samatta, wewe mchezaji unayeozea ligi kuu Tanzania Bara wakati uwezo unao, una kwama wapi? hebu badilika ukale kuku kwa mrija huko ulimwenguni.
Ila sasa wazazi wengi watakuwa wameshaamka juu ya kuwatafutia timu watoto wao hii baada ya kugundua kuwa katika soka kuna mtonyo mwingi.
Usisahau kuuliza au kusema lolote juu ya unachokisoma hapo chini kuna sehemu ya kufanya hivyo.
Comments
Loading…