in ,

Roy Keane atawavusha ‘Class of 92’?

Roy Keane

Nimesoma mahali taarifa ya mpango wa kuajiriwa kocha mpya wa klabu ya Salford City. Kocha huyo ni nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane. Salford Citry inamilikiwa na marafiki wakubwa, Paul Scholes, Nick Butt, Ryan Giggs, David Beckham, Phil Neville na Gary Neville ambao ni maarufu kama ‘Class of 92’.

Keane amekabidhiwa mikoba ya kuinoa Salford baada ya mabosi hao kumfukuza kazi kocha wao Graham  alexander mwanzoni mwa wiki hii. Hata hivyo wakati mchakato wa kumpatia timu hiyo Roy Keane, jukumu la kukinoa kikosi hicho kwa sasa lipo mikononi mwa Paul Scholes kwa muda ambaye atakiongoza hadi apatikane kocha mpya. Salford City ipo kwenye mikakati ya kutafuta nafasi ya kupanda daraja hadi la kwanza. 

Aidha, Salford wapo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi daraja la pili, ikiwa imeshinda mechi tatu na kutoka sare mara mbili katika mechi tano walizocheza.

Taarifa inabainisha kuwa Roy Keane aliongozana na wamiliki wa timu hiyo kwenda uwanjani kuwatazama walipomenyana na tranmere  ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Roy Keane aliachana na kazi ya ukocha mwaka 2018 wakati huo akiwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ireland Kaskazini chini ya Martin O’Neill. Keane amewahi kuzinoa timu za Aston Villa, Ipswich Town na Nottingham Forest.

Nyota huyo anafahamika kuwa miongoni mwa viungo bora wa ulinzi katika soka duniani, akiwa amecheza kwa mafanikio chini ya kocha Alex Ferguson. Keane ni mchambuzi mzuri wa soka hususani Ligi Kuu England.

Kukabidhiwa jukumu la kuinoa Salford City kulinifanya nicheke kidogo. Inachonichekesha ni kwamba ni washkaji wameamua kupeana dili za kazi ama kama wasemavyo vijana wa mjini ‘kupeana shavu’. Ni kweli Roy Keane anatafuta timu ya kufundisha, lakini hakuna mmiliki wala klabu yoyote ambayo imetamani kumwajiri nguli huyo. 

Kwa vile hana kazi hiyo zaidi uchambuzi Sky Sports, ni wazi ana uchu wa kupewa timu yoyote bila kujali iko daraja gani. Kama sifa za kocha mwenye hadhi yake sidhani kama angekubali kwenda kuinoa Salford ili ipande daraja la pili. 

Inawezekana kuna ofa nono anayotarajiwa kupewa na mabosi wa timu hiyo, lakini swali ni kwamba nini kinampeleka huko? Pengine tunaweza kusema kocha anaweza kufundisha popote na akafanya maajabu, lakini haiwezekani leo hii Jurgen Klopp, Zinedine Zidane, Pitso Mosimane waende kuzifundiha timu za daraja la pili ili kuhangaika ipande hadi daraja la kwanza. Hadhi ya Roy Keane kutoka kufundisha timu ya taifa hadi kwenda daraja la pili iliko Salford ndicho kichekeshe chenyewe. 

Najua kuna mashabiki watasema Salford ni timu yenye malengo makubwa lakini katika ngazi waliyopo sasa sio ya kutaka kuaminisha kwamba imefikia hadhi ya kuvutia makocha wenye sifa za hali ya juu. 

Kinachowabeba Salford City ni majina ya wamiliki wao. Ni wamiliki ambao wamewahi kuwa wachezaji wa kiwango cha juu, huku Ryan Giggs akiwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Wales. 

Hivi, ikiwa Salford City itaboronga katika mechi ikiwa chini ya Roy Keane, ni kweli wamiliki hao watakubali kumtupia virago kiongozi wao wa zamani pale Manchester United? 

Class of 92 watakuwa tayari kumfedhesha Roy Keane na aonekana ni kocha asiye na lolote kwa vile kashindwa kuimudu hata timu ya daraja la pili? Nachora picha, watawezaje kumtimua kazi rafiki yao kama atashindwa kufanya vizuri kwenye timu? 

Inaeleweka kuwa suala la mkataba ni ajira inayopaswa kufuatwa misingi, lakini haiba ya pande zote mbili zinafahamika kwa hadhi yake kwahiyo kwa akili ya kawaida kabisa unaweza kujiuliza itakuwaje kuwaje hiyo timu?

Ikiwa malengo ya kupanda daraja hayatafikiwa, Keane atatazamika vipi mbele ya wachezaji wenzake wa zamani na ambao sasa watakuwa mabosi wake? 

Ukocha wa Keane kwenda Salford City tunaweza kabisa kufananisha na mwenendo wa Rafa Benitez ambaye akiwa katika timu mbili za Valencia na Liverpool alipata mafanikio makubwa. Timu ya tatu ni Chelsea, ambako alikwedna kufanya kazi kwa muda. Ni kama wasemavyo vijana wa mjini, kuwa Benitez alikuwa anafanya deiwaka tu. Hali kadhalika akiwa Newcastle United hakufanikiwa, ni kama ilivyokuwa kwa Real Madrid ambako aliishia kufukuzwa.

Najiuliza heshima ya Roy Keane inaweza kuvunjwa na marafiki ambao ambao walikuwa wachezaji wenzake miaka ya nyuma? Je, ubabe wa Keane na matamshi yenye utata yataweza kumpa heshima akiwa kocha Salford Citry au nao watamchinjia baharini na kuvunja heshima yake?

Labda, tuseme Roy Keane anataka kusafisha nyota yake katika ukocha, hivyo anaweza kujiunga na timu ya wachezaji wenzake wa zamani. Lakini hiyo haihalalishi kuwa atakuwa kocha wa kudumu klabuni hapo kwa vile tabia za wamaliki zitakuwa zinaendelezwa na jamaa zake hao. 

Ni ukocha au kusaka malisho mengine kupitia Salford City? Au jamaa zake wanamtengenezea sifa nyingine kuwa aliwahi kuinoa Salford City? Kwa vile timu yenyewe imebebwa na umaarufu wa majina ya wamiliki sitoshangaa kuona Keane akitangaza kuachia ngazi mwenyewe pale mambo yatakapokuwa magumu badala ya wamiliki kutangaza wamemfukuza.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Metacha

Metacha Ajitathimini Yanga

Tanzania Sports

Mambo 10 yanayomkabili kocha mpya wa Yanga