in , , ,

Pazia Ligi Kuu England lafunguliwa

*Zijue timu tano zitakazopewa nafasi
*Gareth Bale kutoanza mechi Spurs
*Scott Parker QPR, Bent atua Fulham

Washabiki wa soka wameshajiweka tayari kutazama mechi za msimu mpya wa Ligi Kuu England (EPL), wakiwa na shauku ya kujua nani atatwaa taji hilo lenye hadhi kubwa.

Klabu zinazoangaliwa sana na kupewa nafasi ni zile zilizomaliza nafasi tano za juu; mabingwa watetezi, Manchester United, Manchester City, Chelsea, Arsenal na Tottenham Hotspur.
Wapo wanaoziangalia Arsenal na Spurs kama timu zinazolenga tu kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na si kuukamata ubingwa wenyewe.

Maswali ambayo si rahisi kupata majibu katika fikra za watu ni iwapo United watamudu kutetea taji lao bila ya kocha wao kwa miaka 26, Sir Alex Ferguson aliyemwachia mikoba David Moyes.
Je, mhandisi na kocha mpya wa Manchester City, Manuel Pellegrini ataweza kurejesha kombe hilo Eastlands lilipokuwa kwa msimu mmoja kabla ya United kuwapokonya msimu uliopita?

Ama maswali ni mengi zaidi’ Jose Mourinho atarejesha heshima Stamford Bridge kwa kutwaa kombe hilo kama alivyopata kufanya kabla ya kuihama klabu hiyo.

Arsene Wenger anaweza kuwa na jeuri ya kuwaongoza vijana wake washike nafasi ya kwanza kwa kuwapiga vikumbo vigogo hao wengine pamoja na timu nyingine? Andre Villas-Boas naye je, ataongeza mafanikio Spurs waliomaliza nafasi ya tano msimu uliopita?

Manchester City

Kuwasili kwa Pellegrini Etihad kulionesha nia ya wamiliki kutaka ubingwa, baada ya kumwondoa Roberto Mancini kabla msimu uliopita haujamalizika.

Kadhalika Pellegrini ametumia pauni milioni 90 kusajili wachezaji aliodhani wanaweza kurejesha hadhi ya ubingwa ambao Mei 13, 2012 waliwanyang’anya United kwa bao la Sergio Aguero na kukata kiu ya ukame wa ubingwa kwa miaka 44.

Msimu huu wamesajili wachezaji nyota wanne, Mbrazili Fernandinho; wachezaji wawili kutoka Sevilla, Alvaro Negredo na Jesus Navas pamoja na mpachika mabao, Steven Jovetic kutoka Fiorentina.

Kuondoka kwa Carlos Tevez aliyekwenda Juventus na mlinzi Kolo Toure aliyehamia Liverpool hakuoneshi kuwagharimu City kwa namna yoyote ile, na wanajidai kwamba wanao washambuliaji bora kuliko timu zote za EPL.

City wakiwa na wachezaji wengine waliokuwa nao kama Yaya Toure, Vincent Kompany, Joe Hart, David Silva na Sergio Aguero wanaweza kuwa tishio kubwa msimu huu.

Chelsea

Jose Mourinho amerejea na kiu ya washabiki wengi wa Stamford Bridge ni kuona wakichukua ubingwa.

Hata hivyo, Mourinho amerejea baada ya msimu ambao hakuwa na mafanikio sana nchini Hispania, akiwa na Real Madrid, alikoondoka licha ya kusaidi mkataba wa miaka minne mwaka jana tu.

Mwenyewe anasema atahakikisha anawapandisha taratibu Chelsea na kuwasimika kwenye kilele cha mafanikio England na bila shaka kuwarejeshea heshima barani Ulaya.
Licha ya kutwaa Ubingwa wa Ligi ya Europa, kwa hadhi yake, Chelsea hawawezi kujisifu na kujidai sana kwa kombe hilo, kwani hucukuliwa ni mashindano ya timu za daraja la pili zilizotupwa nje ya Ligi ya Mabingwa au kukosa nafasi humo.

Wachezaji nyota waliosajiliwa msimu huu ni Andre Schurrle kutoka Bayer Leverkusen na Marco van Ginkle aliyekuwa Vitesse Arnhem. Hao wanaongeza nguvu kwenye kikosi chenye vipaji kibao tayari, wakiwamo akina Romelu Lukaku, Kevin de Bruyne na Juan Mata ambaye ni kama injini ya timu.

Bado Mourinho anaweza kumfufua Fernando Torres na kumrejesha katika hali yake nzuri ya upachikaji mabao, maana bado Roman Abramovich anaamini bei ya pauni milioni 50 iliyomnunulia inatakiwa ioneshe thamani yake uwanjani.

Wachezaji wengine muhimu klabuni hapo ni kipa Petr Cech, David Luiz, Frank Lampard na Eden Hazard.

Manchester United

Kocha mpya David Moyes ana wakati mgumu wa kuwahakikishia wadau kwamba anaweza kuendeleza vyema klabu iliyotwaa makombe mengi zaidi.

Anatoka Everton ambao hawakupata kuwa mabingwa katika miaka yake 11, lakini walau amepata liwazo kwa kutwaa Ngao ya Jamii walipocheza na Wigan ambao hata hivyo wameshuka daraja.
Hana uzoefu wa kuongoza klabu kubwa kama hii, lakini pengine uzoefu wa wachezaji unaweza kutumika. Usajili mpya mkubwa ni ule alioachiwa na Fergie, wa Wilfred Zaha.

Ana tatizo la kutatua kumhusu Wayne Rooney anayetaka kuondoka, akiwa ameshatamka hivyo zaidi ya mara mbili tangu enzi za kocha Fergie lakini anakataliwa. Je, akibakishwa kwa nguvu atacheza vyema?

Moyes ameshindwa zaidi ya mara moja kumpata kiungo Cesc Fabregas wa Barcelona, ambapo mchezaji mwenyewe amesema hataki kuhama. Kutokana na kutosaini wachezaji wapya, watawategemea zaidi akina Robin Van Persie, Rio Ferdinand, Ryan Giggs na Phil Jones, lakini pia Nemanja Vidic na Rooney kama atawika.

Arsenal

Washika Bunduki wa London wameshindwa kutwaa taji kwa mwaka wa nane sasa. Je, kuna dalili yoyote ya mabadiliko msimu huu mpya?

Safari hii kocha Arsene Wenger alijaribu kutoa fedha kusaini wachezaji wenye majina makubwa kama Gonzalo Hoguain, Luis Suarez na Wayne Rooney, lakini mpaka sasa hajapata hata mmoja.

Amesaini mchezaji mmoja mdogo Yaya Sanogo kutoka Auxerre, lakini anasisitiza kwamba wataendelea na jitihada za usajili hadi siku ya mwisho ya usajili, wikiendi ya kwanza ya mwezi ujao.
Angempata Suarez, Arsenal wangekuwa na nguvu sana, ambapo viungo mahiri kama Jack Wilshere, Alex Oxlaide-Chamberlain, Theo Walcott na Santi Cazorla wangemlisha vyema mipira na angeitumbukiza wavuni kirahisi kuliko ilivyo kwa Liverpool.

Raia huyo wa Uruguay ambaye amekanusha kusema anabaki Liverpool na bado anaitazama Arsenal, angeungana vyema na washambuliaji wengine, Lucas Podolski na Olivier Giroud na wangekuwa na uhakika wa kupata kombe mojawapo.

Lakini sasa hawana uhakika naye, wala hawana nyota mwneye uwezo wa kupachika mabao kati ya 20 na 30 kwa msimu, je, Sanogo ataweza au Giroud na Podolski watabadilika?
Walcott na Wilshere wataweza kuisaidia sana klabu dimbani na nguzo yao nyuma atakuwa beki wa kati, Mjerumani Per Mertesacker

Tottenham Hotspur

Je, Andre Villas-Boas atafanikiwa kuwawezesha Spurs waingie kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya au atawapa zawadi kubwa zaidi?

Historia inaonesha Spurs hawajapata kutwaa ubingwa, lakini mwelekeo wao ni mzuri mwaka hadi mwaka, japokuwa ni vigumu kusema msimu huu wapo tayari kupigania ubingwa wa England.
Ikiwa watabaki na Gareth Bale, na Arsenal wakabaki bila Suarez, watakuwa na karibu nguvu sawa ya kupigana kikumbo kuwania nafasi ya nne kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Spurs wamejiimarisha vyema, kwa kuwasajili watu kama Paulinho na Chadli.

Iwapo Emmanuel Adebayor ataondoka kama inavyodaiwa, ina maana Spurs watabaki na mshambuliaji mmoja wa ukweli, Jermain Defoe, baada ya Clint Dempsey kurudi kwao Marekani kuchezea Seattle Sounders.

Bale anahitajika sana Spurs, maana msimu uliopita ni yeye aliwabeba, lakini kwa kuwa alisukwa na Villas-Boas, anaweza akaibuliwa mwingine msimu huu.

Ikiwa atakwenda Real Madrid kwa pauni milioni 85, Spurs wanaweza kununua mchezaji mwingine mzuri, lakini tatizo ni muda wa usajili unaoelekea kumalizika na uwapo wa wachezaji wazuri wenye nia ya kwenda kuja Spurs.

Tusishangae kuona klabu kama Liverpool ya Brendan Rodgers na Everton ya Roberto Martinez wakipanda kuwafukuzia vigogo hawa watano, au walau Arsenal na Spurs.
Wachezaji muhimu kwa Spurs msimu huu ni Kyle Walker, Bale, Lewis Holtby na Paulinho.

GARETH BALE KUTOANZA SPURS

Nyota wa Tottenham Hotspur, Gareth Bale anayewaniwa na Real Madrid hatacheza katika mechi ya kufungua pazia la Ligi Kuu ya England dhidi ya Crystal Palace.

Licha ya kukosa mechi ya Jumamosi hii kocha wake, Andre Villas-Boas nasema anatumaini mchezaji wao huyo muhimu hatahama White Hart Lane.

Bale, 24, anatakiwa na Santiago Bernabeu msimu huu, lakini Villas-Boas anadai kutoanza kwake mechi hii ni kwa sababu ya majeraha ya hapa na pale aliyopata mchezoni.

“Tumekuwa wawazi sana kuhusu mchezaji huyu na nia yetu ya kubaki naye. Ni wazi kwamba katika soka chochote kinaweza kutokea, lakini ni aina ya mchezaji aliyetusaidia na tungependa kuendelea kuwa naye hapa,” Villas-Boas akasema.

Inadaiwa kwamba bado Real Madrid wanajiandaa kuvunja rekodi ya usajili wa dunia kwa kumchukua winga huyo mzaliwa wa Wales, ambapo kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema mazungumzo yanaendelea.

Bale mwenyewe amesisitiza kwamba anataka kwenda kuchezea miamba hao wa nchini Hispania. Bale amecheza mechi moja tu ya maandalizi ya msimu, Julai 16 dhidi ya Swindon na pia hakucheza mechi ya taifa lake dhidi ya Jamhuri ya Ireland Jumatano iliyopita.

SCOT PARKER KWENDA QPR?

Kocha wa Queen Park Rangers (QPR) inayocheza ligi daraja la pili (Championships), Harry Redknapp amesema wamekubaliana na Tottenham Hotspur kumchukua mchezaji wao, Scott Parker.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 alicheza chini ya Redknapp hapo Spurs na sasa anataka kuungana naye QPR baada ya kucheza mara 30 akiwa na Spurs msimu uliopita.
“Tumeshakubaliana na Tottenham, kwa hiyo sasa ni juu ya Scott mwenyewe kuamua iwapo anataka kuja au la,” akasema Redknapp.

QPR wamekuwa wakijaribu kuuza wachezaji wake wa bei kubwa wanaochukua mishahara minono ili kuwa tayari kumudu bajeti ya msimu ujao, ambapo hawatakuwa na mapato makubwa, tofauti na walivyokuwa EPL msimu uliopita.

Habari hizo ni za kushangaza kidogo kwa Parker kucheza daraja la chini, mtu aliyepata kucheza timu ya taifa pia, lakini Redknapp anasema inaweza kuwa raha zaidi kuchezea timu inayolenga kupanda daraja kuliko ile iliyo tayari juu.

Parker alijiunga Spurs kutoka West Ham Agosti 2011 kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 5, na amepata pia kuchezea Chelsea na Newcastle.

DARREN BENT AENDA FULHAM

Mpachika mabao wa Aston Villa, Darren Bent aliyekuwa haelewani na kocha wake, Paul Lambert amesajiliwa Fulham kwa mkopo.

Bent alipoteza makali baada ya Lambert kumsajili mshambuliaji wa Ubelgiji, Christian Benteke, aliyeibuka na mabao 17 msimu uliopita, akimwacha Bent benchi muda mrefu hapo Villa.
Bent alisajiliwa kwa pauni milioni 18 zilizovunja rekodi ya klabu hiyo mwaka 2011, lakini alianza kutocheza alipoumbia nyama za paja kabla ya Benteke kupanda chati.

Msimu uliopita, Bent mwenye umri wa miaka 29 alifunga mabao sita tu katika mechi 23, lakini walikuwa wakifokeana na kocha wake, hali iliyomjengea mazingira magumu ya kucheza vyema.

LIVERPOOL WAMCHUKUA SISSOKHO

Klabu ya Liverpool imemsajili kwa mkopo beki wa kushoto wa Valencia, Aly Cissokho (25).
Hata hivyo, Mfaransa huyo aliyelichezea taifa lake mechi moja, hatakuwapo wakati wa mechi ya ufunguzi dhidi ya Stoke Jumamosi hii, kwani anatarajiwa kutinga Liverpool wiki ijayo.

Kocha Brendan Rodgers amefanikiwa, walau hadi sasa, kumzuia Luis Suarez kwenda Arsenal, na amesajili golikipa Simon Mignolet kutoka Sunderland kwa pauni milioni tisa, Iago Aspas kwa pauni milioni sana, Luis Alberto kwa pauni milioni 6.8m na Kolo Toure kama mchezaji huru kutoka Manchester City.

Wanatarajia kumsajili mshambuliaji wa Anzhi Makhachkala, Willian, pengine ili kuwa na uhakika wa mtu makini kwenye safu ya ushambuliaji, kwani Suarez asipoondoka sasa anaweza kuaga Januari.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

KAMATI YAPITIA USAJILI, NGASA KUCHEZEA YANGA

MICHEZO YA MTU MMOJA MMOJA IPATE VIONGOZI WAKE