in , , ,

NIPENI NAMBA YA MOURINHO TAFADHALI

 

 

Juzi Jose Mourinho alikutana na kipigo cha mabao matatu kwa moja kutoka kwa Southampton ndani ya dimba la Stamford Bridge. Kipigo hicho ni cha nne kati ya michezo nane ya EPL ambayo Chelsea wamecheza na kushinda michezo miwili pekee na kupata sare mbili.

Wengi wanaamini kuwa meneja huyo anakaribia kutimuliwa na wengine walidhani kuwa angeachia ngazi mwenyewe. Mourinho mwenyewe baada ya mchezo dhidi ya Southampton alisema kuwa hawezi kuachia ngazi na pia kama Chelsea watamtimua wamtimue lakini watambue kwamba yeye ndiye meneja bora  kuliko wote waliopita Chelsea.

Nina maswali kadhaa ya kumuuliza Mourinho kuhusiana na imani yake hii. Sihitaji anwani yake ya makazi wala msaada wowote wa kuniwezesha kukutana naye ana kwa ana. Nahitaji kupatiwa namba yake ili nimuulize maswali yangu kwa njia ya simu.

Gianluca Vialli
Gianluca Vialli

Huenda Mourinho yuko sahihi anaposema kuwa Chelsea haikuwahi kuwa na meneja bora kumzidi yeye. Nafikiri rekodi za nguvu alizowahi kuziweka akiwa na timu hiyo zinatosha kumfanya aseme hayo aliyoyasema. Hata hivyo nahitaji maelezo ya ziada kutoka kwake kuhusiana na hili.

Advertisement
Advertisement

Wananijia akilini mameneja kadhaa waliowahi kupita Chelsea. Nawakumbuka Gianluca Vialli, Carlo Ancelloti na Roberto di Matteo. Nataka nimkumbushe Mourinho kuhusu umahiri uliowahi kuonyeshwa na mameneja hawa ndani au na nje ya Chelsea ili ayapime tena maneno yake kisha anipatie jibu ambalo nitaridhika nalo pasi na shaka.

 Carlo Ancelloti
Carlo Ancelloti

Gianluca Vialli aliteuliwa kuwa meneja wa Chelsea Februari 1998 ambapo bado alikuwa mchezaji wa timu hiyo. Kinachomfanya Vialli awe mmoja kati ya mameneja bora kuwahi kuifundisha Chelsea ni kutwaa mataji mawili ya michuano ya Ulaya, Kombe la Washindi la UEFA 1998 ‘Uefa Cup Winners’ Cup’ na baadae ‘Uefa Super Cup’ ambapo aliiongoza Chelsea kuwazamisha Real Madrid kwa 1-0.

Vialli alishinda makombe hayo ya Ulaya kwenye msimu ambao takribani paundi milioni 10 pekee zilitumika kwa ajili ya usajili. Mourinho hakuwahi kushinda taji lolote la Ulaya akiwa na Chelsea na tayari zimeshatumika zaidi ya paundi milioni 400 kwa ajili ya usajili wa wachezaji akiwa meneja wa timu hiyo. Nataka nimuulize Mourinho anamuonaje Vialli.

Carlo Ancelotti ni meneja ambaye hata baadhi ya mashabiki wa Chelsea wanaamini ni bora kuliko Mourinho. Mei 9 2010 Ancelotti alipoiwezesha timu hiyo kutwaa taji la EPL baada ya kuwatwanga Wigan 8-0 ndani ya Stamford Bridge baadhi ya mashabiki walibeba mabango yaliyosomeka ‘KING CARLO MORE THAN SPECIAL’ wakiwa na maana Carlo ni zaidi ya Mourinho ‘Special One’.

Roberto di Matteo
Roberto di Matteo

Pia rekodi za Carlo za nje ya Chelsea ni bora zaidi ya rekodi za Mourinho. Meneja huyo anaongoza kwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mara nyingi zaidi (mara tatu) sawa na Bob Paisley wa Liverpool. Moja kati ya hayo matatu alilitwaa akiwa na Real Madrid mwaka 2014, timu ambayo Mourinho alishindwa angalau kuifikisha fainali alipoifundisha kwa misimu mitatu.

Nahitaji Mourinho anieleze pia anavyomchukulia Roberto di Matteo. Di Matteo ni meneja pekee aliyewahi kuiongoza Chelsea kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa. Alitwaa taji hilo kwenye msimu wa 2011-12. Mourinho ameshiriki michuano hiyo kwa misimu mitano akiwa meneja wa Chelsea lakini hakuwahi angalau kuipeleka timu hiyo fainali.

Ni hao mameneja watatu ambao nataka kujua jinsi Mourinho anavyowachukulia ili nikubaliane naye kuwa yeye ndiye meneja bora zaidi kuwahi kuifundisha Chelsea. Nipeni namba yake tafadhali.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Liverpool wamtimua kocha

Tanzania Sports

TIMU YA WIKI EPL