in

Ni wakati wa Liverpool kufanya mabadiliko

Liverpool

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu England Liverpool hawapo kwenye mbio za kulinda taji lao, na zaidi wametolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya robo fainali baada ya kuruhusu kutoka suluhu na Real Madrid katika mchezo wa marudiano. Mchezo wa kwanza Liverpool walikubali kipigo cha mabao 3-1.

Baada ya mchezo huo kocha Jurgen Klopp alisema kuwa anaelekeza nguvu zake kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Hii ikiwa na maana hawapo kwenye mbio za ubingwa, bali wanajaribu kutafuta nafasi nne za juu.

Kutokana na msimu mbaya waliokumbana nao tayari mjadala umeanza ni mchezaji gani anastahili kubaki kwa majogoo hao. Mjadala huo unaongozwa na swali moja, je klabu hiyo inatakiwa kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake ama kuachwa kama kilivyo?

Ni vigumu kuficha kuwa safu ya ulinzi ya Liverpool ni chanzo cha timu hiyo kuterereka na kuwa si lolote si chochote mbele ya wapinzani wao wa Ligi Kuu England, na kuvuna aibu ya msimu mzima. Hilo linaonesha ni kiasi Liverpool wanatakiwa kufanya mabadiliko kwenye kikosi chao, na kama watapuuza hilo watakuwa wamefanya makosa makubwa kwani wanaweza kuwa na msimu mbaya zaidi kuliko walionao kwa sasa.

Majeruhi ya mabeki wao ni kiini cha kuporomoka Liverpool msimu huu, huku wachezaji tegemeo Virgil van Dijk na Joe Gomez waliondolewa kikosini kutokana na majeraha hayo hivyo kutoshiriki mashindano yoyote msimu huu.

Aidha, kuvurugika kwa safu ya ulinzi kulimlazimu kocha Jurgen Klopp kuwatumia baadhi ya wachezaji wake wa safu ya kiungo kucheza nambari nne na tano, kwa mfano viungo wakabaji Herndoson na Fabinho walilazimika kucheza safu ya ulinzi kwa muda mrefu katika mechi za Ligi Kuu.

Na imesemwa kuwa katika mechi mbili dhidi ya Real Madrid, safu ya ulinzi ya Liverpool iliyokuwa chini ya Ozan Kabak na Nat Phillips hawakuwa na ujuzi wa kutosha kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wala mashindano ya Ligi Kuu England.

Tanzania Sports
Liverpool

Mara kadhaa msimu huu Jurgen Klopp ameonekana kuzidiwa na uchovu kutokana na vipigo mbalimbali, hali ambayo baadhi ya wachambuzi wa soka wanaamini kuwa huenda ndiyo mwisho wake wa kuinoa Liverpool.

Liverpool walimchukua kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ambaye amewaletea mafanikio waliyoyakosa, lakini litakuwa jambo la kufirika tu iwapo mabosi wa timu hiyo wamejiandaa kwa maisha bila Kloop ama kuamini kuwa wanatakiwa kuachana naye haraka.

Kwa mafanikio aliyoleta Liverpool, litakuwa jambo la busara kumwacha Klopp aendelee kuwanoa majogoo hao, na kwamba wasije wakafanya makosa kama aliyofanya Mwenyekiti wa Tottenham Hotspurs, Daniel Levy kuachana na Mauricio Pochettino ambaye kwa sasa nyota yake inang’ara PSG wakiwa wamefaika nusu fainali kwa mwaka wa pili mfululizo.

Kushindwa kufanya mabadiliko katika kikosi chao kwa kuongeza wachezaji wa daraja la juu, ni sababu mojawapo ya kutofanikiwa Hotspurs na kufeli kwa sera zao sokoni. Timu ilihitaji kuimarishwa katika maeneo mbalimbali kwa kuleta wachezaji wapya, lakini vitu hivyo chini ya Pochettino havikufanyika.

Baada ya kuanza kuyumba Daniel Levy aliamua kumtoa kafara Pochettino na kumwajiri Jose Mourinho. Licha ya kubadili kocha, sasa tunaona Pochettino yuko nusu fainali ya Mabingwa Ulaya, wakati Mourinho anahangaika kuipandisha timu hiyo kutafuta nafasi ya kufuzu angalau Europa League msimu ujao na wala haipo kwenye mbio za ubingwa kama ambavyo iliongoza Ligi kwa muda.

Kumbadili Klopp kwa sasa kunaweza kuivuruga kabisa klabu hiyo, na mmiliki wake John W. Henry anatakiwa kutoa fedha za usajili wachezaji wapya ambao wataongeza mchango na kuwapa ushindani nyota waliopo.

Sehemu ya kwanza ya kuongeza nguvu ni safu ya ushambuliaji, lakini Liverpool ilipata mafanikio kupitia nyota wanaounda safu hiyo kama vile Sadio Mane, Roberto Firmino,Mohamed Salah chini ya Klopp kwahiyo litakuwa jambo la busara kuongeza nyota wengine eneo hilo.

Roberto Firmino hajafumania nyavu kwa siku nyingi, kiwango chake kimeshika mno na ushirikiano katika safu hiyo imeibua maswali kama unatakiwa kuendelezwa ama kuletwa nyota wapya wa kushindana nao.

Uhodari wa safu ya ushambuliaji wa sasa umeyoyoma, ujio wa Diogo Jota utakuwa sehemu ya mpango wa kufanya mabadiliko kikosini, ikiwemo kuwaruhusu kuondoka kati ya Mane,Salah na Firmino au wote watatu kuuzwa.

Mane ana miaka 29, Salah ana miaka 28, Firmino ana miaka 29, kwahiyo hawa tayari muda wao wa kutamba kwa muda mrefu umeisha. Ingawaje wanaweza kufanya vizuri klabuni hapo, lakini kama wakibaki inabidi ufanyike usajili wa nyota wapya ambao watawaweka benchi mastaa hao na kuwafanya kuwa wachezaji wa akiba kutokana na uzoefu wao.

Kujenga kikosi kipya hakuepukiki, hilo ni pamoja na kuingia sokoni kiushindani kuisaka sahihi ya Kylian Mbappe na nyota wengine. Diogo Jota anatakiwa kupewa nafasi, lakini Liverpool wanahitaji wachezaji wa kiwango cha juu zaidi yake katika maeneo mbalimbali na wenye ari na umri mzuri.

Ousmane Dembele anaweza kuwa mchezaji sahihi wa Liverpool, lakini kupatikana kwake ni kama atakataa mkataba mpya na Barcelona. Jadon Sancho bila shaka atatafuta timu ya kuhamia kama Borussia Dortmund watashindwa kufuzu mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao, ingawa changamoto hiyo ipo pia kwa Liverpool hivyo huenda asilekee huko.

Thiago Alcantara anatumikaje Liverpool? Hilo ni swali lingine la kupatiwa majibu. Nyota huyo ana kipaji kizuri, na pengine ndiye kiungo mkabaji wa asili ndani ya kikosi cha Liverpool, lakini inaonekana kama Klopp hajagundua namna ya kukitumia kipaji cha Thiago katika kikosi chake.

Tanzania Sports
Liverpool

Thiago amelelewa La Masia kabla ya kuhamia Bayern Munich baada ya kushindwa kupata nafasi Barcelona. Awali alitaka kumsajili kabla hajaenda Bayern Munich, lakini sasa amefanikiwa kumpata baada ya kutoka Munich na kwenda Anfield, je anamtuiaje nyota huyo? Ni swali gumu.

Licha ya Thiago kutazamwa kiuwezo kama Xabi Alonso bado hajaonekana kuonesha makeke yake kila anapopata nafasi, lakini pia alitarajiwa kuchukua nafasi kubwa kitu ambacho hajafanikiwa hadi sasa. Kwa mchezaji ni shida, na kwa kocha ni shida. Kilichobaki ni mabadiliko Liverpool.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

70 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Casemiro

Casemiro ni bora kuliko Neymar?

Tanzania Sports

Mnyukano wa European Super League na UEFA