Wakati anazaliwa wazazi wake walimpatia jina la Joseph na hivyo akawa anatambulika kwa majina ya Joseph Mbilinyi. Mwenyewe anavyohadithia kupitia wimbo wake wa kiburi anasema kwamba wakati anakuwa mtaani walimuita kwa jina la “May” na mwenyewe anavyojisifu kwamba mtaa mzima walimtambua kwamba yeye ni mtoto wa nani. Katika kukua kwake kwenye Sanaa aliamua kujiita jina la “too proud” yaani akimaanisha mtu ambaye anajisifia kwa sana. Kiuhalisia yeye ni mtu ambaye mwenye haiba ya kujisifia sana. Baada ya kukaa kwenye kiwanda cha muziki kwa miaka kadhaa akaamua kubadilisha jina lake na kujiita tu MR 2.
Baada ya kupitia changamoto kadhaa katika kiwanda cha muziki ikiwemo suala la usambazaji wa kazi zake za Sanaa aliamua asambaze kazi zake yeye mwenyewe kwa kuwa anatembea nazo katika maeneo mbalimbali ya mji. Katika nyakati hizo ndipo alipoamua kwamba abadilishe jina lake na kujiita “sugu” akimaanisha kwamba mtu ambaye hakati tamaa kirahisi na mtu ambaye amepitia misukosuko mingi lakini hakati tamaa. Katika harakati hizo akaamua kutoa wimbo ambao aliuita DEIWAKA ambao nao ukaja kubeba jina la nembo zake za kibiashara ambapo ukawa kama kauli mbiu akionyesha namna wafanyakazi ambao wasiokuwa kwenye ajira rasmi wanavyopambana kutafuta maisha yao ya kila siku.
Hakuishia hapo akaamua kuanza kupanua mipaka na kuanza kutoka nje ya nchi kwenda kutafuta fursa za kimaisha na katika harakati hizo akajikuta anarekodi albamu zake nje ya nchi na albamu yake ya kwanza kurekodi nje ya nchi aliiita “nje ya bongo”. Wasanii wa muziki wa kizazi kipya humheshimu kama mwanzilishi wa mziki wa Bongo flava kwani yeye ni mojawapo ya wasanii wa mwanzo kuanza kupigwa kazi zake katika redio kwani kabla ya hapo kazi za wasanii wa kizazi kipya zilionekana kama ni kazi za wahuni. Hakuishia tu kwenye Sanaa kwani mwaka 2010 alikuwa ni msanii wa kwanza nchini Tanzania kuingia bungeni na kuwa mbunge katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania. Aliingia bungeni kwa rekodi ya kuwa mbunge aliyepata kura nyingi sana.
Na akaweza kuhudumu bungeni kwa mihula miwili na wakati anahudumu bungeni na ndipo alipojipa jina jipya la utani akajiita “jongwe” ambalo lilikuwa ni jina la utani la kiongozi wa zamani wa taifa la Zimbabwe hayati Robert Mugabe ambaye alikaa madarakani kwa mda mrefu sana. Alikuja kuwa pia msanii wa kwanza wa muziki wa kizazi kipya kuandika tawasifu(autobiography) ya maisha yake aliyoiita “muziki na maisha” ambapo iliuza nakala nyingi na chapa yake ya pili ilikuja kuzinduliwa na raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa mikutano wa Serena Hotel ambapo tukio hilo lilikuwa linaruka mubashara na mamilioni ya watanzania wakiliangalia katika runinga majumbani kwao.
Hakuishia hapo aliamua kuanzisha tamasha ambalo lilikuwa lina lengo la kuongeza thamani kwa wasanuuu ambao walichangia kwa namna moja ama nyingine katika maendeleo ya mziki wa kizazi kipya kwa kuanzisha tamasha alilolipa jina la “Bongo flava honors” na tamasha hili lilianza mapema mwaka jana na lilianza kwa kuwa linafanyikia katika ukumbi wa Alliance Francaise ambapo wasanii mbalimbali wa huko nyuma walipata nafasi ya kutumbuiza katika tamasha hilo ikiwemo TID, DULLY SYKES, MATONYA, BANANA ZORO, JUMA NATURE,MABAGA FRESH, MANDOJO NA DOMOKAYA, na wengineo. Mnamo Aprili 26 mwaka 2024 alifungua upya ukurasa wa tamasha la bongo flava honors kwa kuifanya katika ukumbi wa warehouse Arena uliopo katika mitaa ya Masaki katika jiji la Dar es salaam ambapo alilifanya na msanii AY. vituo vya runinga vya EFM na ETV vilikuwa ndio washirika wake kwenye tamasha hilo.
Sugu anasifika sana mtandaoni kwa kuweka post za kujisifia sana kwenye kurasa zake za kijamii mitandaoni. Ni mtu ambaye ni king’ang’anizi kwamba akilishikilia jambo huwa sio mwepesi kukata tamaa mapema sana. Kwa sifa hii inatosheleza kwa yeye kuingia rasmi kwenye tasnia ya michezo kwani inahitaji watu wenye haiba kama yake waingie kama wawekezaji katika sekta hiyo. Kuingia kwake katika michezo itakuwa sio jambo geni sana kwani aliwahi kuwa anajishughulisha na kutoa hamasa kwa klabu ya Mbeya City kwa nyakati tofauti.
Kama akiamua kuingia kwenye kiwanda cha michezo kama mwekezaji basi hatakuwa msanii wa kwanza duniani kufanya hivyo kwani huko Marekani na Ulaya wasanii wengi tu wamewahi kuwekeza kwenye michezo kwa namna moja ama nyingine. Nchini Marekani wasanii kadhaa wamewekeza kwenye michezo kwa ima kusimamia wachezaji mmoja mmoja ama kumiliki hisa katika vilabu vya michezo na hivyo kufanya kuwa ni sehemu ya wamiliki wa vilabu vya michezo na wengine wameshiriki katika shughuli za ukocha.
Tukianzia kwenye shughuli za ukocha msanii wa mitindo ya kufokafoka (rap) nchini Marekani anayefahamika kama Snoop Dogg anafahamika kwamba huwa anaupenda sana mchezo wa American Football na amekuwa anafundisha mara kwa mara vijana wa mjini kwake namna ya kucheza mchezo huo katika nyakati ambazo huwa anakuwa huru kwenye mapumziko na inasemekana kuna wachezaji kadhaa wakubwa ambao wanacheza kwenye ligi ya kulipwa ya mchezo huo wamewahi kupita chini ya mikono yake kama kocha ambaye aliwakuza.
Msanii Beyonce anamiliki hisa katika klabu ya mpira wa kikapu ya Houston Rockets, msanii Jay Z anamiliki hisa katika klabu ya kikapu ya Brooklyn Nets, Usher anamiliki hisa katika klabu ya Cleveland lackers, Msanii Justin Timberlake anamiliki hisa katika klabu ya Memphis Grizlies, wasanii ambao ni mume na mke Will na Jada Pinckett Smith wanamilimiki hisa katika klabu ya Philadelphia 76ers na msanii wa miondoko ya Rnb aitwaye Ciara anamiliki hisa katika klabu ya Seattle Sounders ambayo ni klabu ya soka ya nchini Marekani.
Sugu anaweza kujiingiza katika klabu mojawapo ya mchezo kama mmiliki kwa kununua hisa na kuwa ni sehemu ya maamuzi ama anaweza akawa ni promota wa michezo kwa kuwa ni muandaaji wa matukio ya michezo kupitia mojawapo ya kampuni zake anazozimiliki. Kiuhakika tasnia ya michezo nchini Tanzania inamhitaji Sugu.
Comments
Loading…