KWENYE mchezo wa mpira wa miguu yapo mabadiliko yanatokea kwa kasi. Zipo aina mbili za makocha hadi sasa badala ya ile moja iliyokuwa ikifahamika. Aina ya kwanza ya makocha ni wale wachezaji wa zamani ambao waligeukia kazi ya ukocha. Hawa walijiunga na mafunzo ya ukocha yanayotolewa na vyama vya soka kutoka kwa wakufunzi wa Kimataifa wa Shirikisho la Mpira duniani (FIFA). Mfano barani Afrika makocha wanatumia leseni ya shirikisho la soka Afrika (CAF) na wengine wa leseni ya Sirikisho la Soka Ulaya au Amerika kusini.
Kwa maana hiyo wengi wao walikuwa wale wachezaji wa zamani ambao wanatumia ujunzi wa kufundishwa darasani na kucheza mpira kwa manufaa ya timu wanazoajiriwa. Aina ya pili ni makocha ambao wamefundishwa darasani bila kuwa wachezaji mahiri katika ulimwengu wa soka. Kundi hili lina makocha wengi vijana na wazee. Mfano Jose Mourinho hakuwa mchezaji mahiri lakini aligeukia kazi ya ukocha. Andre Villa Boas aligeukia kazi ya ukocha bila kuwa mchezaji mahiri. Alionesha umahiri wa ufundi tangu akiwa klabu ya FC Porto na baadaye Chelsea na Tottenham Hotspurs akiwa kijana mdogo sana.
Julian Nangelsmann ni kocha mdogo kiumri na ndiye bosi wa Timu ya Taifa ya Ujerumani. Kabla ya hapo alikuwa kocha wa Bayern Munich na nyinginezo. Hakuwa mchezaji mahiri enzi za ujana wake. Hilo ni sawa na Fabian Hurzeler mwenye umri wa miaika 31 akiwa anaonesha ufundi wake Ligi Kuu England baada ya kuiwezesha St. Pauli ya Ujerumani kutinga Bundesliga.
Mabadiliko hayo ndiyo yamewaleta vijana wengi wapya kwenye mchezo wa kandanda. Baadhi yao waliamua kuachana na uchezaji wa mpira sababu walikumbwa na majeraha mara kwa mara na kusababisha kushindwa kuendeleza vipaji vyao vya kucheza. Humo ndimo wanamoibuka akina Abdihamid Moalin ambaye jina lake limekuwa maarufu siku za karibuni.
Ujio wa Moalin Ligi Kuu
Miaka mitatu iliyopita jina la Abdihamid Moalin liliingia katika medani ya michezo na burudani nchini Tanzania. Ilikuwa mara ya kwanza kulisikia jina hilo katika mchezo wa soka unaopendwa na maelfu ya watu. Ni jina lililokuwa sehemu ya Ligi Kuu Tanzania. Abdihamid Moalin aliingia Tanzania katika Ligi Kuu baada ya kuajiriwa kwenye benchi la ufundi la klabu ya Azam Fc ya Dar es salaam.
Baadaye alibadilishiwa majukumu na kuwa kaimu kocha mkuu wa Azam F.C kufuatia kuondoka kwa kocha wao George Lwandamina raia wa Zambia. Katika kipindi cha ukocha wa Lwandamina, klabu ya Azam FC haikuwa na mafanikio hivyo ikafungua mlango wa Mzambia huyo kuondoka.
Msimu wa kwanza
Safari ya ukocha wa Abdihamid Moalin katika Ligi Kuu Tanzania ilianza msimu wa 2021/2022 baada ya Afisa Mtendaji mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin kummkabidhi jukumu la kuwa kaimu kocha. Ni katika msimu huo Moalin alianza kukinoa kikosi cha kwanza cha Azam na kuonesha umahiri wake. Aliwavutia wadau wengi wa kandanda na mashabiki kwa ujumla. Ufundi aliokuwa nao ni ile hali ya kuibadilisha Azam FC kutoka timu inayokumbana na vipigo hadi kuimarisha uwezo wao. Azam FC ilibadilika kwa kiasi fulani na kumpa sifa Moalin kama mwalimu mzuri anayeweza kufanya vizuri akipewa muda na kupata uzoefu wa Ligi Kuu Tanzania.
Raia wa Marekani
Kwa asili Abdihamid Moalin ni kutoka nchi ya Somalia, lakini anao uraia wa Marekani. Aliwasili katika Ligi Kuu Tanzania akitokea nchini Marekani alikoonwa na Azam FC. Aliingia katika Ligi Kuu Tanzania kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Azam F.C. uzoefu wake wa soka kutoka Marekani akichanganya na Tanzania ndiyo ulitengeneza wasifu mzuri unaomfanya aendelee kubaki katika Ligi Kuu.
Ukocha KMC FC
Hakuwa na uzoefu wowote wa Ligi Kuu Tanzania, lakini kwa kipindi kifupi aligundua ipo fursa. Kuanzia hapo Moalin alitengeneza sifa ya kocha mwenye kuajirika popote. Haikushangaza wakati anaondoka Azam Fc na kwenda kujiunga na vigogo wa Kinondoni yaani KMC FC ambayo ni mali ya serikali. Moalin alipewa kazi ya ukocha baada ya kuondolewa Jamhuri Kihwelo “Julio” ambaye naye alichyukua jukumu hilo kutoka kwa Mnyarwanda Thiery Hitimana. Ufundi wake ndiyo uliwezesha KMC kubaki Ligi Kuu baada ya kuwa kwenye mstari wa kushuka daraja kwa muda mrefu. Umahiri wa Moalin ulionekana hapo, na aliendelea kukinoa kikosi hicho hadi Novemba 2024 alipoamua kung’atuka.
Majukumu makubwa
Haitashangaza Abdihamid Moalin akitangazwa kuwa mmoja wa makocha kwenye timu kubwa hapa nchini. Sababu ni kwamba Moalin amepata uzoefu wa kufundisha wachezaji wa Ligi Kuu. Amepata uzoefu wa hekaheka za Ligi Kuu na kuongeza ujuzi wake kwa vitendo kwenye mchezo wa soka. Kwa kufundisha soka Tanzania kipindi cha miaka mitatu na nusu ni dhahiri anaweza kuyapokea majukumu mengine makubwa zaidi ya sasa.
Comments
Loading…