MWAKA 2015 unamalizika na kuanza 2016 ukishuhudia Arsenal wakiwa
vinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL huku Aston Villa wakiwa
na dalili za kushuka daraja.
Baada ya ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Bournemouth na Leicester
kutoshana nguvu na Manchester City, Arsenal wanaongoza ligi kwa
tofauti ya mabao, kwani wao na Leicester wana pointi 39 baada ya mechi
19.
City wamebaki katika nafasi ya tatu kwa pointi zao 36, Tottenham
Hotspur nao waking’ang’ania nafasi ya nne kwa pointi 35 huku
Manchester United wakiwa wa sita na pointi zao 30 baada ya kutoshana
nguvu na Chelsea kwenye mechi ya Jumatatu iliyopita.
Liverpool waliowafunga Sunderland wamepanda hadi nafasi ya saba huku
wakiwaacha Sunderland na kazi ngumu, lakini kocha Sam Allerdyce
anasema kuna maendeleo mazuri kwa kikosi chake licha ya kufungwa.
Sunderland wanashika anfasi ya 19 na pointi zao 12, Newcastle wakiwa
wa 18 na pointi 17 huku Villa wakiwa hoi nafasi ya mwisho na pointi
nane tu. Ligi hiyo inaendelea Januari 2 mwakani katika mwendelezo wa
mechi nyingi za msimu wa sikukuu.
Liverpool walishinda mechi yao ya Jumatano hii kwa bao la Christian
Benteke, nao wakimaliza mwaka kwa ushindi mzuri na bao la mapema zaidi
katika kipindi cha pili, sekunde ya 22.