in

Muziki wa Bongofleva ni mkubwa kwa sasa

Diamond Platnumz

Nimeona kampeni kubwa dhidi ya mwanamuziki Nassib Abdul mwenye lakabu ya Dimaond Platinumz ambaye anawania tuzo ya kimataifa inayotolewa na BET. 

Aliyekuwa mgombea wa urais mwaka 2020, Tundu Lissu alianzisha kampeni za kutaka waandaaji wa tuzo za BET wamuondoe Diamond Platinumz kwa kile alichokiita kushirikiana na watu ambao wamekuwa na taswira mbaya kwa jamii kutokana na matendo yao. 

Lissu aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter anaonekana kumkosoa Diamond Platinumz kwa hatua yake ya kushiriki kampeni za kisiasa za chama tawala, kushirikiana na viongozi ambao anawaita wamevunja haki za binadamu nchini Tanzania. 

Naye mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema alidaka kampeni hiyo na kuwaomba wafuasi wa chama chake waungane kupinga uteuzi wa Diamond kuwania tuzo hizo. Ni kampeni ambazo zinaoenekana kumilikiwa na wafuasi wa baadhi ya vyama vya upinzani na wanaharakati wengine.

Aidha, Mwanaharakati Maria Sarungi naye akaanza kampeni ya kupiga kura dhidi ya Diamond Platinumz kushinikiza kuondolewa kwa mwanamuziki huyo katika orodha ya wanaowania tuzo za BET mwaka huu. Bila kujali ni sahihi au si sahihi, kampeni dhidi ya Diamond Platinumz zina matokeo chanya na hasi. Katika makala haya nitaangalia namna mtu aliye katikati ya kampeni hizi yaani hana upande wowote.

Diamond Platnumz returns with colorful new music video for ‘Jeje’

Niseme mapema makala haya si msimamo wa TANZANIASPORTS bali maoni binafsi ya mwandishi nikiwa mwananchi wa Tanzania. 

Nimezitazama hekaheka hizo kwenye mitandao ya kijamii na sababu zake, nalazimika kuwaheshimu wote wanaofanya jitihada ashindwe na wengine wanaotaka ashinde tuzo ya BET. Lakini kwa jicho la tatu ninafurahia mnyukano huo; nina sababu chache za kueleza katika hilo.

Mosi, nafurahi kuona muziki wa Bongofleva umekuwa kwenye mjadala wa kitaifa. Kutoka Joseph Mbilinyi (Sugu) kuongoza tasnia hiyo kuheshimiwa na baadaye kufanikiwa kuipeleka bungeni yaani kuwa Mbunge akiwakilisha jimbo la Mbeya Mjini, hadi kushuhudia mjadala wa kitaifa kumhusu Nassib Abdul kukumbana na kampeni dhidi ya ushiriki wake wa tuzo ya muziki ya kimataifa, kwa hakika muziki wetu wa Bongofleva unapiga hatua kubwa sana, ni jambo la kujivunia. 

Kutoka kuwaona akina King Sapeto, Mr.Nice, Da Jo, Zay B, Sista PO, King GK, AY, Mwanafalsafa, Profesa Jay na wanamuziki wengineo kama wahuni au kuona mziki wenyewe kuwa ; muziki wa kihuni, sasa akili zinakwenda kubadilika taratibu katika mwelekeo wa kupaa juu na kuchukua nafasi yake ya umuhimu kama sehemu ya ajira, kuelimisha na kusisitiza utamaduni. 

Kwamba muziki huu uliobezwa mwanzoni sasa umefanikiwa kupenya katika mifumo ya utawala ikiwemo kupata wabunge waliochaguliwa katika majimbo, mfano Joseph Haule (Mikumi,Morogoro) na Hamis Mwinjuma (Muheza, Tanga), pamoja na madiwani Said Fela na Babalevo.

Pili, nafasi ya muziki wa Bongofleva ni kubwa kwa sasa katika maisha ya watanzania. Kampeni dhidi ya Diamond Platinum ni ujumbe kwa wale wazazi wanaolazimisha watoto wao wenye vipaji vya muziki waonekane kama wahuni au hakuna jambo la maana katika muziki wa Bongofleva. 

Sasa wanaoneshwa umuhimu na nafasi ya muziki huo katika utoaji wa ajira kwa kiasi kikubwa moja kwa moja au kwa njia nyingine ambayo inahusiana na muziki huo. Muziki ni ajira na biashara ambayo inawanufaisha wengi mno nchini na kimataifa.

Tatu, hekaheka dhidi ya Diamond Platinumz zinaonesha namna uhuru wa maoni ulivyotanua na kukua miongoni mwa watanzania. Kwamba kila mtu ashinde mechi, hata kama watakuwepo watu wanaokera lakini ni vizuri kuwasikiliza, kuwavumilia na kusonga mbele. kama walivyosema wahenga, ukitaka kupiga hatua mbele ni muhimu kuacha kutupia mawe kila mbwa anayekubwekea.

Nne, hekaheka hizo zinathibitisha ukubwa wa jina la Diamond Platinumz katika jamii ya kitanzania, Afrika Mashariki, Afrika na Kimataifa zaidi. nimeona baadhi ya raia wa Uganda na Kenya mitandaoni wanakumbushana umuhimu wa kumpigia kura Diamond Platinumz. 

Tano, ni dhahiri jina la Diamond Platinumz linakwenda kutangazwa zaidi na atawavutia wengi ambao watataka kujua zaidi kuhusu mwanamuziki huyo. Midomoni mwa wadau wa muziki Afrika na kimataifa,viongozi wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na hata wale ambao sio mashabiki wa muziki watakuwa wakivutiwa zaidi na jina la mwanamuziki huyo na kutaka kujua mengi kumhusu.

Ni suala la Diamond mwenyewe kutambua hiki kinachoendelea ni uthibitisho wa nafasi yake katika jamii na nini afanye, nini asifanye, nini zungumze, kipi asizungumze na wapi aende na wapi asiende. Ni suala la kuangalia fursa hii inayoonekana kupitia minyukano ya pande mbili za washindani wake na wafuasi wake dhidi ya itikadi za siasa.

Sita, kampeni hizi zimeonesha kwamba watanzania tumekuwa wazuri kwa kupiga kelele juu ya jambo fulani kwa kuwa si sehemu ya jambo hilo, ila tukiingia huko nasi tunakuwa hivyo hivyo. Wengi ni kwa sababu hawajapata kile alichokipata Diamond Platinumz kwahiyo wanadhani kuhakikisha anaondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho itabadili maisha yetu kutoka hali moja kwenda hali nyingine.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Harry Kane

Harry Kane bila mataji atadumu Spurs ?

Tanzania Sports

Fahamu mambo muhimu mashindano ya EURO 2020