in , , ,

Mourinho abwatukia wachezaji

*Akana kupigana na United kwa Pedro

*Bodi ya EPL yakosoa bao la Benteke

Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amelalamikia kiwango cha wachezaji wake waandamizi sita, walioshindwa kuisaidia timu na kufanya ianze vibaya msimu kuliko ilivyopata kutokea katika miaka 17 iliyopita.

Mourinho ambaye amekuwa na wakati mgumu ndani na nje ya uwanja, amemtaja nahodha na swahiba wake mkubwa, John Terry, kuwa ni mmoja wa walioshindwa kucheza kwa kiwango kwenye mechi mbili za awali na kuambulia pointi moja tu.

Kocha huyo alimtoa uwanjani Terry baada ya nusu ya kwanza ya mechi dhidi ya Manchester City, ambapo Chelsea walichapwa 3-0. Mabingwa hao watetezi Jumapili hii wanasafiri hadi West Bromwich Albion kucheza nao, timu iliyowafunga Chelsea 3-0 mwishoni mwa msimu uliopita.

Mourinho alitaja wachezaji wengine ambao itabidi wajirekebishe kuwa ni mabeki wa pembeni Cesar Azpilicueta na Branislav Ivanovic, mlinzi Gary Cahil, kiungo mkabaji Nemanja Matic na Cesc Fabregas ambaye hucheza kiungo cha kati au cha ushambuliaji.

Fabregas alichambuliwa na baadhi ya wataalamu wa soka, ‘akiangushiwa jumba bovu’ kutokana na jinsi alivyocheza, ikielezwa alishindwa kuwakata Man City hivyo kusababisha majanga kwa timu yake. Msimu uliopita alicheza vizuri mwanzoni, lakini kuelekea ukingoni alishuka kiwango.

“Siridhishwi na mtu yeyote, sifurahishwi na kiwango cha Branislav Ivanovic, Gary Cahill, John Terry, Cesar Azpilicueta, Eden Hazard, Cesc Fabregas, Nemanja Matic. Siridhishwi na kiwango change kwa sababu nilikuwa Napata matokeo mazuri zaidi ya ninayopata sasa,” akasema kocha huyo maarufu kwa kujisifu na kushambulia wenzake.

SIKUSHINDANA NA UNITED KUMPATA PEDRO – MOURINHO

Pedro
Pedro

Kocha Jose Mourinho amebeza madai ya vyombo vya habari kwamba alifanya makusudi kuwazibia Manchester United kumpata mshambuliaji wa Barcelona, Pedro Rodriguez, aliyebadili mawazo dakika za mwisho na kujiunga na Chelsea.

Mourinho alisema yeye hana sababu ya ‘kuwashinda’ Man U nje ya uwanja, hataki kwenda kwenye mwelekeo huo, bali anapenda kuwashinda dimbani. Man United walishajipanga kumchukua Pedro na hata Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa United, Ed Woodward alikwenda Hispania kukamilisha mambo.

Hata hivyo, inadaiwa kwamba wakati bosi huyo akiwa huko, Mourinho alinyanyua simu, akazungumza na Pedro kisha akamuungisha na Mhispania mwenzake, Fabregas, akamshawishi abadili njia na kwenda London badala ya Chelsea, na ikawa hivyo.

Kadhalika, inaelezwa kwamba kuna wachezaji waliomshawishi Pedro asijiunge na Man U kwa maelezo kwamba kocha wao, Louis van Gaal ni mbabe na kwamba huenda mambo yake yangeharibika. Kwa kuzingatia hayo, Pedro akasajiliwa Chelsea kwa pauni milioni 21, wakati Van Gaal alikuwa ameshaanza kumzungumzia.

“Mimi siwapigi Manchester United nje ya uwanja, bali napenda kufanya hivyo uwanjani. Sitaki kwenda mwelekeo huo. Kazi yetu si kuchukua mchezaji anayetakiwa na klabu nyingine. Lakini dirisha la usajili linapokuwa wazi hatuna budi kutumia fursa hiyo,” akasema Mourinho.

BAO LA BENTEKE HALIKUSTAHILI KUKUBALIWA

Bao hili limekosolewa na bodi ya ligi
Bao hili limekosolewa na bodi ya ligi

Bodi ya Ligi Kuu ya England imetamka kwamba bao alilofunga mshambuliaji mpya wa kati wa Liverpool, Christian Benteke dhidi ya Bournemouth Jumatatu iliyopita halikustahili kukubaliwa kwa sababu kulikuwa na kosa la kuotea.

Katika taarifa yake, bodi hiyo imethibitisha kwamba mchezaji Philippe Coutinho alifanya kosa hilo, kwa sababu alijaribu kuucheza mpira akaukosa ndipo Benteke akatia wavuni, wakati marekebisho ya kanuni yapo wazi kwamba halingeweza kuwa bao.

Hata hivyo, kutokana na utaratibu kwamba uamuzi wa mwamuzi uwanjani ndio wa mwisho kwa maana ya matokeo, itabidi Bournemouth wabaki na maumivu yao, na kocha wao Eddie Howe alisema tangu siku hiyo kwamba uamuzi uliwagharimu.

Aliwasiliana na mkuu wa waamuzi, Mike Riley kwa ajili ya kutaka ufafanuzi. Pamoja na ufafanuzi huo, bodi imerejea tena kufafanua ni wakati gani na kwa vipi mchezaji atakuwa ametenda kosa la kuotea hata kama hakuugusa mpira. Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alidai hakuona tukio hilo lakini cha muhimu kwake ni kwamba uamuzi ulikuwa ni bao na wakachukua pointi tatu muhimu.

advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

YANGA NA AZAM TULETEENI NAFASI NNE

MAN CITY WATATWAA UBINGWA MSIMU HUU?! SABABU TANO HIZI HAPA