Tanzania ina nafasi ya kupeleka klabu mbili tu kwenye michuano ya kimataifa ya Afrika. Utaratibu ambao umekuwa ukitumika ni kwamba mshindi wa Ligi Kuu anapata nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika na mshindi wa pili kushiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kuanzia msimu huu utaratibu unabadilika. Hii ni baada ya TFF kutangaza kuwepo kwa michuano mipya ya Kombe la Shirikisho la TFF. Michuano hii itaanza kutimua vumbi Novemba na itajumuisha timu zote 16 za Ligi Kuu, timu zote 24 za Ligi Daraja la Kwanza na zile 24 za Ligi Daraja la Pili.

Mshindi wa kombe hili la TFF ndiye atakayekuwa akipata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Atakuwa anachukua nafasi aliyokuwa akiipata mshindi wa pili wa Ligi Kuu. Hivyo kwenye Ligi kuu ni mshindi pekee atakayekuwa anapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Nafikiri hapa ladha ya Ligi Kuu itakuwa inapungua mwishoni mwa msimu. Kutakuwa hakuna tena umuhimu wa kushindania nafasi ya pili baada ya kujulikana bingwa. Lakini pengine hili si jambo baya sana kwa kuwa michuano mipya ya Kombe la TFF inatuletea ladha nyingine.

Nafasi mbili za kushiriki michuano ya kimataifa ambazo tunazipata kutoka kwa Chama cha Soka cha Afrika (CAF) ni chache. Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zinapewa nafasi mbili tu na CAF kutokana na utaratibu wa upangaji wa viwango wa CAF unaofahamika kama ‘CAF 5-Year Ranking’.

advertisement
Advertisement

Utaratibu huu wa CAF unazipa nchi 12 tu nafasi ya kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa ya Afrika ambapo mbili zinaingia kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika na mbili kwenye Kombe la Shrikisho.

Nchi hizi 12 ni zile ambazo klabu zake zimefanikiwa kukusanya alama nyingi kupitia utaratibu wa ‘CAF 5-Year Ranking’. Klabu itakusanya alama endapo tu itafanikiwa kuingia hatua za makundi za michuano ya Klabu Bingwa Afrika ama Kombe la Shirikisho.
Kwenye Klabu Bingwa Afrika timu bingwa inakusanya alama 5, mshindi wa pili alama 4, inayoingia nusu fainali inakusanya alama 3 na mshindi wa tatu kwenye kundi alama 2 na alama 1 kwa mshindi wanne wa kila kundi.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho timu bingwa inakusanya alama 4, mshindi wa pili alama 3, inayoingia nusu fainali inakusanya alama 2 na inayoishia kwenye makundi inakusanya alama 1.

Alama hizi hutumika kugawa nafasi ya idadi za klabu ambazo nchi shiriki zitaingiza kwenye michuano ya kimataifa ya Afrika kwa miaka mitano ya mbeleni ukitoa mwaka unaofuatia.

Kwa sasa nchi 12 zilizo na alama nyingi zaidi kwenye mfumo huu ni Tunisia, Misri, Kongo DRC, Algeria, Sudan, Ivory Coast, Morocco, Cameroon, Congo, Mali, Nigeria na South Africa.

Tanzania hatuna hata alama moja kwa sasa kwa kuwa klabu zetu zimekuwa zikifanya vibaya na kushindwa kutinga angalau hatua za makundi kwenye michuano ya kimataifa.

Klabu zetu za Yanga na Azam zilizopata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa itakayoanza mapema mwakani zinatakiwa kufanya juhudi ili zifike mbali na kutukusanyia alama za kutosha.

Klabu hizi ziiwezeshe Tanzania kuwa na alama nyingi na hata kuingia kwenye nchi 12 za juu mara moja. Hapo tutakuwa tumepata nafasi ya kuingiza klabu nne kwenye michuano ya kimataifa ya Afrika. Tukiwa na nafasi nne mshindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pia atapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kama ilivyokuwa awali.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Abramovich amwaga £100m

Mourinho abwatukia wachezaji