UWAZI KWENYE MAPATO NA MATUMIZI YA VYAMA VYA MICHEZO NI MUHIMU
Uhai wa taasisi yoyote duniani hutegemea mambo kadhaa na mojawapo ya hayo mambo ni namna inavyoweza kusimamia rasilimali zake vizuri kwa ajili ya maendeleo endelevu. Uwajibikaji wa viongozi kwenye suala hilo nyeti ni jambo lenye kuhitaji umakini wa hali ya juu. Katika dhana ya utawala bora kwenye taasisi za michezo viongozi huhimizwa kuhakikisha kwamba wanakuwa wazi kwa wanachama wao juu ya mapato ambayo taasisi huwa inatengeneza na pia kuweka wazi namna mapato hayo yanavyotumika. Wanachama wanapofahamu mwenendo wa kifedha wa taasisi zao huwa inasaidia kuwajengea Imani na dhana njema kwa viongozi wao wanaowasimamia.
Baraza la michezo la Tanzania (BMT) limekuwa linasisitiza vyama wanachama wahakikishe kwamba zinakuwa na rekodi za taarifa ya mapato na matumizi ya taasisi zao na kuhakikisha kwamba mahesabu hayo yamepitiwa na mkaguzi wa mahesabu (auditor). Kanuni za michezo zinavilazimisha vyama kufanya hivyo na si kila chama cha mchezo ambacho hufanya hivyo.
Faida za uwazi na kama ifuatavyo:
Husaidia kujua kiwango cha madeni ambacho taasisi inayo. Kwa kawaida ukaguzi wowote ule wa fedha mwisho wa siku huweka wazi baada ya kupitia taarifa rasmi za mapato na matumizi ambazo huwa katika nyaraka za chama ni yapi madeni chama husika kinadaiwa. Kuyajua madeni ni muhimu kwani husaidia kutafuta ufumbuzi wa namna ya kuyalipa hayo madeni na kisha kuyamaliza kwa kutafuta namna ya kuyalipa madeni hayo bila ya kuathiri shughuli za kila siku za chama. Ni hatari sana kwa chama kutokuwa na taarifa halisi ya madeni yake ambayo inadaiwa.
Husaidia kwa wajumbe na wanachama kutoa maoni mazuri juu ya hatma nzuri ya taasisi zao katika siku zijazo. Wajumbe na wanachama wa chama cha mchezo wanaweza kutoa maoni vizuri juu ya kuboresha kwa taasisi yao kama nyaraka za fedha zinavyokuwa zimekaguliwa. Kwa ujumla kama nyaraka zinzkuwa hazijakaguliwa basi huwa inakuwa ni sintofagamu nyingi sana ambazo huwa hazina majibu rasmi.
Husaidia kujua kiwango cha kodi ambacho taasisi inatakiwa ilipe. Pindi taasisi ikifanya ukaguzi wa mapato na matumizi yake basi itakuwa kwenye hali nzuri ya kuweza kutambua ni kiwango kipi cha kodi ambacho taasisi hiyo inatakiwa ilipe na kwa wakati gani. Hii itasaidia taasisi hiyo isije kuingia kwenye mgogoro na mamlaka za kodi.
Husaidia kujua mali ambazo taasisi inazo. Kama taasisi itafanya ukaguzi wa mapato na matumizi yake ya fedha basi itakuwa ni rahisi kwa taasisi hiyo kuweza kujua kiwango cha mali ambazo taasisi hiyo inazo. Mali zinaweza zikawa zenye kuhamishika ama zisizo hamishika. Hili huwezekana kwa kuwa katika ukaguzi mali zote za chama nyaraka zake hulazimika kuwasilishwa kwa wakaguzi wakati wa zoezi likiwa linaendelea.
Hujenga hali ya kuaminiana baina ya viongozi na wadau wa taasisi hiyo. Katika zoezi la ukaguzi kiujumla huwasilishwa nyaraka zote za mapato na matumizi ya taasisi na pindi zinapowasilishwa nyaraka hizo na zikapitiwa na kuonekana hazina tatizo lolote lile katika kupatikana kwake na kutumika kwake basi hujenga hali ya kuaminiana baina ya watendaji wa vyama vya michezo. Watendaji wengi wa vyama vya michezo huwa hawaaaminiani kwa sababu taarifa za mapato na matumizi huwa haziko wazi.
Licha ya kwamba umuhimu wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za taasisi ni jambo ambalo ni misingi ya kanuni za utawala bora kwenye michezo lakini bado watendaji wengi wa vyama vya michezo hawalitekelezi na hili ni kwa sababu zifuatazo:
Mosi kutokujiamini kwa baadhi ya watendaji. Baadhi ya watendaji wa vyama vya michezo hawajiamini sana kweny utendaji wao na hudhani kwamba kama ikifanyika ukaguzi basi kama kuna mahala wataonekana wameteleza itashusha Imani ambayo wajumbe wa vyama hivyo kwao wao.
Pili kukosekana nyaraka muhimu wakati wa uendeshaji wa shughuli za vyama. Taasisi nyingi/vyama vya michezo utendaji wake wa kila siku huwa una mapungufu ya kiutendaji kiuweledi na mambo mengi hufanyika bila ya kufuata taratibu rasmi za kiofisi. Hili hupelekea kushindikana kufanyika kwa ukaguzi vizuri kwa kuwa nyaraka nyingi muhimu huwa zinakosekana pindi zinapokuwa zinahitajika. Manunuzi mengi ya kiofiisi hufanyika bila ya kuwepo kwa nyaraka.
Suala la ukaguzi wa taarifa za mapato na matumizi ni jambo ambalo ni la muhimu sana, kwani pindi lisipofanyika huwa lina athari nyingi sana hasi na miongoni mwa athari hizo ni pamoja na:
- Kupoteza wadhamini kutokana na kukosekana kwa nyaraka hizo; wadhamini hupenda kutoa pesa ama rasilimali zao kwenda kwenye maendeleo ya mchezo/klabu husika lakini sio kwenda kumnufaisha mtu binafsi na kama taasisi/chama itakuwa haina taarifa hizo basi hupoteza kuaminika kwake kwa wadhamini
- Migogoro isiyoisha kwenye vyama.vyama ambavyo taarifa zake za ukaguzi wa mapato na matumizi haziwekwi wazi kwa wajumbe huwa vina tabia ya kuwa na migogoro isiyoisha na hili hutokana na kwamba wajumbe huwa hawaamini viongozi wao kwa sababu hawajawahi kuziona taarifa za mapato na matumizi.
- Kuingia katika makosa ya kisheria na mamlaka. Taasisi ambazo huwa zinafanya ukaguzi mara kwa mara huwa viongozi wake hupewa maelekezo ya maeneo gani wayarekebishe ili waweze kutokuwa kwenye makosa ya ukiukwaji wa sharia kama vile ukwepaji kodi na mengineo.
Mwisho niunge mkono rai ya waziri wa utamaduni, Sanaa na michezo mheshimiwa Dokta Damas Ndumbaro aliyoitoa mnamo tarehe 19/06/2024 wakati anazindua mashindano ya mchezo wa mpira wa kikapu pale alipotoa agizo kwa vyama vyote vya michezo kuwasilisha taariza zao za ukaguzi wa mapato na matumizi kwa baraza la michezo ndani ya miezi 3 kufanya hivyo kutakuwa na manufaa mengi sana.
Comments
Loading…