in , , ,

Man U wamfuta kazi Amorim baada ya miezi 14

Ruben Amorim

Manchester United wamemfuta kazi kocha wao mkuu, Ruben Amorim, baada ya miezi 14 tu tangu ateuliwe kuiongoza klabu hiyo.

Mchezo wa mwisho wa Amorim ulikuwa sare ya 1-1 dhidi ya Leeds United Jumapili, matokeo yaliyoiacha United nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu England baada ya mechi 20.

Aliyekuwa kiungo wa kati wa United na sasa kocha wa timu ya Under-18, Darren Fletcher, ataiongoza timu kwa muda kama kocha wa mpito, akianza na mchezo wa ugenini dhidi ya Burnley Jumatano usiku. Uteuzi wa kocha wa kudumu unatarajiwa kufanyika majira ya kiangazi.

Uongozi wa klabu, ukiwemo mkurugenzi mkuu Omar Berrada na mkurugenzi wa michezo Jason Wilcox, umefikia uamuzi huo kufuatia kuvunjika kwa mahusiano nyuma ya pazia. Kwa mujibu wa mkataba aliotia saini Amorim alipoondoka Sporting CP kujiunga na United Novemba 2024, hakuna kipengele cha kuondoka kwa gharama nafuu, hivyo United watalazimika kulipa mkataba wake wote, uliokuwa unaisha mwaka 2027, ukiwa na chaguo la kuongezwa mwaka mmoja.

Kupitia taarifa rasmi ya klabu, United wamesema uamuzi huo umefanywa “kwa masikitiko” lakini ni “wakati sahihi wa kufanya mabadiliko” ili “kuipa timu nafasi bora zaidi ya kumaliza juu iwezekanavyo kwenye Premier League”.

“Klabu inamshukuru Ruben kwa mchango wake na inamtakia kila la heri siku zijazo,” ilisema taarifa hiyo.

Akizungumza baada ya sare hiyo Elland Road, Amorim alidokeza kuwepo kwa mvutano na watu waliokuwa wakifanya kazi naye, akisisitiza kuwa yeye ni “meneja” wa United, si kocha tu.
“itakuwa hivi kwa miezi 18 au hadi bodi itaamua kubadilisha,” alisema. “Sitajiuzulu. Nitafanya kazi yangu hadi mtu mwingine aje kunibadilisha.”

Amorim alikosolewa kwa kukosa kubadilika kiufundi, hasa kwa kushikilia mfumo wake anaoupenda wa 3-4-3. Ingawa kulikuwa na majaribio ya mifumo mingine mazoezini, alirejea mara kwa mara kwenye mfumo huo, hata alipodokeza kuwa klabu ilishindwa kumsajili wachezaji anaohitaji kuutekeleza kikamilifu.

United waliilipa Sporting €11m (£9.25m) kumsajili Amorim, ambaye aliwahi kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu Ureno (2021 na 2024) pamoja na Kombe la Ligi mara mbili. Alimrithi Erik ten Hag, aliyeondoka baada ya miaka miwili na nusu Old Trafford.

Katika kipindi chake, United walipata msimu wao mbaya zaidi katika historia ya Premier League, wakimaliza nafasi ya 15 na pointi 42 pekee. Walitolewa FA Cup raundi ya tano, Carabao Cup robo fainali, na kupoteza fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham, hali iliyowafanya kumaliza msimu bila taji na kukosa soka la Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2014.

Klabu ilitumia zaidi ya £200m kusajili wachezaji wapya majira ya kiangazi 2025, akiwemo Benjamin Sesko, Bryan Mbeumo na Matheus Cunha, lakini matokeo hayakuwa kama ilivyotarajiwa. Msimu huu, United walipata mwanzo wao mbaya zaidi tangu 1992-93, wakikusanya pointi saba tu katika mechi sita za mwanzo.

Uchambuzi unaonyesha kuwa kauli za Amorim baada ya sare na Leeds, zilizoashiria wazi mvutano na uongozi, ndizo zilizoharakisha kuondoka kwake. Alionekana kuhitaji ama kuungwa mkono kikamilifu au kufutwa kazi — na uongozi ukachagua njia ya pili, kwa makubaliano na familia ya Glazer.

Tangu Sir Alex Ferguson astaafu mwaka 2013, Manchester United wamekuwa na mameneja sita wa kudumu, na hawajawahi kumaliza juu zaidi ya nafasi ya pili. Zaidi ya £50m zimetumika kuwalipa mameneja waliotimuliwa.

Kuondoka kwa Amorim kunaacha maswali makubwa kuhusu mwelekeo wa uongozi wa klabu chini ya INEOS na Sir Jim Ratcliffe, hasa ikizingatiwa kuwa aliwahi kusema Amorim anastahili angalau miaka mitatu kuthibitisha uwezo wake.

Sasa macho yote yataelekezwa kwa Darren Fletcher na uongozi wa United, wakitafuta mwelekeo mpya baada ya kipindi kingine kigumu Old Trafford.

Report

Written by Israel Saria

I have been involved with sports in Tanzania as a Volleyball Coach for many years—and was a Tanzania Amateur Volleyball Association (TAVA) leader. I studied sports management at Leipzig University in Germany and understand the science behind sports. That led me to work as a football pundit, with the BBC ( Swahili service) in London. That experience and exposure took me to covering the 2010, World Cup in South Africa. This provided me with a great insight into international level football commentary and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics.I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany, Italy, Belgium, Ireland, France, Kenya etc, and visited almost all of the key football stadiums across United Kingdom, and Europe.

What do you think?

73 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tarryn Allarakhia

Morocco 1-0 Tanzania

Darren Fletcher

Uhaba wa makocha wa kiwango cha juu England