in , , ,

Man U, Everton, West Brom zangara

*Arsenal sare; Reading, Southampton, QPR mkiani

Mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umezidi kung’arisha baadhi ya timu, huku nyingine zikisukumizwa pembezoni.
Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson aliposema hivi karibuni kwamba mchezaji wake Javier Hernandez ‘Chicharito’ anamchanganya, hakukosea, kwani amefanya makubwa.
Chicharito aliyeingia kipindi cha pili alibadilisha hali ya mchezo, ambapo United walikuwa wameelemewa na Aston Villa kwa kuwa nyuma kwa mabao mawili, akayasawazisha na kupachika la tatu.
Wayne Rooney na Robin Van Persie walicheza pamoja lakini hawakuonekana kufurukuta au nyota haikuwa yao wikiendi hii.
Wakicheza kwa kujiamini nyumbani Villa Park, Aston Villa ambao msimu huu hawajacheza vyema, walipachika bao kila kipindi, kupitia kwa Andreas Weimann, lakini wakashindwa kuyalinda.
Wakati Villa wakiachwa nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi, United wamejihakikishia kubaki kileleni, baada ya kufikisha pointi 27.
Chelsea waliopokonywa uongozi na United wiki iliyopita, wana pointi 23, huku Manchester City wanaokipiga na Totenham Hotspur wakiwa na pointi 22 katika nafasi ya tatu.
Hii imekuwa wikiendi ya mwendelezo wa habari njema kwa West Bromwich Albion walioanza vizuri msimu huu.
West Brom wanaofundishwa na Steve Clarke waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wigan Athletic na kushikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi.
Mabao ya West Brom yalitiwa kimiani na James Morrison, kabla ya majalo ya Billy Jones haijamgonga Gary Caldwell na kuingia kwenye kamba za goli lake.
Wigan walipata bao la kufuta machozi kupitia umaliziaji mzuri wa Arouna Kone na wanabaki katika nusu ya chini ya msimamo.
Kwa jinsi West Brom wanavyokwenda vizuri, kocha wao wa zamani, Roberto Di Matteo anatakiwa kujihami anapowazuru wikiendi ijayo na wachezaji wake wa Chelsea.
Arsenal wameendelea na sintofahamu yao, baada ya kukubali sare ya mabao 3-3 nyumbani, walipocheza na Fulham katika mchezo mkali.
Mikel Arteta alikosa penati katika dakika ya mwisho ya mchezo, ambayo ingewafanya Arsenal waibuke na ushindi.
Hata hivyo, kwa uchezaji wa siku za karibuni wa timu hizo mbili, ni matokeo yaliyotarajiwa, ikizingatiwa pia kwamba majirani hao wa London walikuwa wamefungana kwa pointi 15 kabla ya mchezo huo.
Pamoja na kuachia pointi mbili, ilikuwa furaha kwa mshambuliaji Mfaransa wa Arsenal, Olivier Giroud aliyefunga mabao mawili, na kuonesha kigugumizi cha miguu yake mbele ya lango kinaanza kupotea.
Aliifungia timu yake pia kwenye mechi dhidi ya Schalke 04 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne iliyopita kama alivyofanya dhidi ya Reading kwenye Kombe la Ligi.
Ufungaji huo unaweza kukomesha mjadala dhidi yake, pamoja na matakwa ya wachezaji wenzake, Theo Walcott na Lucas Podolski kutaka wapewe jukumu la kufunga mabao hapo kati, badala ya kuchezeshwa pembeni.
Bao jingine la Arsenal lilifungwa na Podolski wakati Dimitar Berbatov aliiamsha Fulham usingizini baada ya kuwa nyuma kwa bao moja, kisha Alex Kacaniklic akasawazisha. Berbatov alifunga bao jingine kwa penati.
Historia inawanyima Fulham ushindi hapo Emirates, kwani kwa miaka 108 hawajapata kushinda, wakifanya vizuri sana huwa ni kuipata pointi moja kama hiyo.
Everton nao waliendelea na mtindo wa kukomboa mabao, baada ya kutanguliwa kufungwa bao na Sunderland.
Kwa ushindi wa mabao 2-1 Everton wanabaki katika nafasi nne za juu kwenye msimamo. Walianza kwa kuumizwa kupitia bao la Adam Johnson kabla tu ya nusu ya kwanza.
Hata hivyo, Everton waliweka jitihada zilizolipa kwa kuzaa mabao mawili kipindi cha pili, kupitia kwa Marouane Fellaini na Nikica Jelavic. Ulikuwa mchezo wa 400 kwa bosi wao, David Moyes na mara ya sita mfululizo wanaepuka kipigo kwa kurudisha bao au mabao.
Shinikizo na machungu ya Queen Park Rangers (QPR) ya Mark Hughes vimeendelea, baada ya kufungwa na Stoke City bao 1-0.
Licha ya mmiliki wa klabu hiyo, Tony Fernandes kumtetea kocha wake akisema mambo haya yanachukua muda, ni dhahiri uvumilivu unaweza kumshinda.
QPR inayobaki mkiani kwa kutoshinda hata mechi moja msimu huu, ilipokea kichapo cha bao la Charlie Adam, baada ya ngome ya QPR kubabaika mapema kipindi cha pili.
Wachovu wengine wa EPL walipanda msimu huu, Southampton waliambulia sare ya bao 1-1 kwa Swansea na kuwafanya Southampton kufikisha pointi tano tu.
Wenzao Reading waliopanda msimu huu pia waliendelea na mwendo wa kinyonga katika eneo lao la tatu za chini ya msimamo, kwa kutoka suluhu na Norwich.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

EPL

Liverpool wawakatalia Chelsea