in

Makocha wetu hawana nafasi ya kudhaminiwa kusoma nje?


SHIRIKISHO la soka TFF ndiye mlezi, mzazi, msimamizi na
mwendeshaji mkuu wa mchezo huo. Serikali kwa upande wake
kama bosi wa nchi inawajibika kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua
katika maendeleo ya soka.


Hata hivyo kumekuwa na upungufu wa makocha wenye viwango
vya kimataifa, badala yake wengi wao wamekuwa makocha wa
kuzunguka timu za hapa hapa nchini au kupata elimu ya ukocha.


Idadi kubwa ya makocha tulionao ni wale ambao wamehudhuria
kozi hizo katika mazingira ya hapa nchini, badala ya kuvuka mipaka
kwenda nje kupata elimu zaidi ambayo itawasaidia kujifunza
utamaduni na misingi ya mataifa mengine yaliyoendelea kisoka.


Lipo kundi la makocha vijana ambao wanatakiwa kusomeshwa kwa
masilahi ya nchi yetu. Vijana kama vile Selemani Matola wanastahili
kupelekwa shuleni kwa kuwa tayari sasa amekuwa kocha msaidizi
wa Taifa Stars, pamoja na kuwa msaidizi kwenye klabu ya Simba.


Tangu alipokuwa akikinoa kikosi cha Simba B, Seleman Matola
ameonyesha mwelekeo mzuri ambao unatakiwa kuongezewa
maarifa. Amekuwa kocha wa Lipuli FC ya Iringa na sasa Polisi
Tanzania ya mkoani Kilimanjaro.


Vijana wenzake kama Salvatory Edward, Zuberi Katwila,Yusuf
Macho, Hemed Morocco, Daudi Lawrence, Dennis Kitambi,

Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mecky Mexime, na Amri Said kwa
kuwataja wachache.


Kundi hili na wanaolingana nao linastahili kupewa udhamini wa
masomo ya ukocha ili kulisaidia taifa. Wengi wao ambao wanapewa
nafasi ya ukocha kwenye klabu zetu ni matunda ya kozi
zinazoendeshwa na Shirikisho la soka nchini, lakini hawatumii fani
kuvuka mipaka ya nchi.


Kama wangepelekwa kwenye nchi zilizoendelea kupata elimu huko
wangekuwa na mchango mkubwa zaidi ya sasa. Seleman Matola
amecheza soka Ligi Kuu Afrika kusini katika klabu ya Supersport,
hivyo amevuna ufundi kiasi kutoka Afrika kusini kuliko wengine
waliocheza soka hapa na kunolewa ukocha hapa.


Soka la Tanzania litapiga hatua kubwa zaidi iwapo TFF na serikali
itahakikisha tunao makocha wenye viwango vya kimataifa na
waliopata elimu kwenye mataifa makubwa. Nchi kama Ujerumani,
Uingereza, Ufaransa, Hispania, Italia na mataifa mengine ya kati
kama vile Denmark, Sweden, Norway, Bulgaria yamekuwa na
mipango ya namna hiyo kuendeleza taaluma ya ukocha.


Hoja yangu ni kwamba Matola na wenzake ni ushahidi kuwa
tunacho kizazi ambacho kimeingia kwenye shughuli za ukocha,
lakini kinahitajika kupatiwa elimu zaidi ya fani hiyo ili kuleta tija
kwa nchi.


Serikali na TFF zinaweza kuchagua walau makocha watano vijana
wakapelekwa nchi za ng’ambo kusomea ukocha kwa nia ya
kuchochea kiwango cha ufundishaji nchini.

Makocha hao watatumika kuendeleza wengine wa Ligi Kuu ama
muundo mzima wa utoaji mafunzo ya ukocha nchini. Makocha
hao wanaweza kuja kuinoa Taifa Stars, Serengeti Boys,
Ngorongoro, Kilimanjaro Stars, Zanzibar Heroes na vikosi vingine
vya vijana. Nazungumzia nje ya utaratibu wa FIFA wa kutoa kozi
mbalimbali za ukochaa.


Makocha wetu wengi tulionao hawaendi nje ya nchi. Kwa sasa
Tanzania tunafundishwa na kocha kutoka Burundi, na tumeona
makocha kutoka nchi hiyo wakizidi kupata nafasi kwenye timu za
Ligi Kuu Tanzania, huku makocha wetu wakiendelea kuzunguka
hapa hapa bila kutafuta fursa ya kufundisha nje.


Kama makocha wa Burundi, au hata wale wa Uganda na Kenya,
wamekuwa wakipata fursa hapa nchini, maana yake wazawa wetu
pia wanaweza kupata timu za kufundisha katika Ligi za Uganda,
Kenya, Burundi, Rwanda na kwingineko barani Afrika.


Kuwapeleka makocha nje angalau watano kunaongeza tija kwa
nchi katika kukuza mchezo wa soka. Makocha hao wanaweza
kupelekwa kila baada ya miaka mitatu,jambo ambalo litasaidia
kuinua soka kupitia mafunzo sahihi.


Tumekuwa tukisisitiza kuanzishwa kwa vituo vya soka yaani
Academy. Vingi vya vituo hivyo vinakabiliwa na ukosefu wa
walimu wenye sifa zinazotakiwa.

Tanzania Sports
Wachezaji wa yanga wakiwa mazoezini


Academy nyingi hazina makocha wenye viwango au waliopitia
mfumo sahihi wa ukocha badala yake ni mapenzi binafsi ya
wanaofundisha mchezo huo pamoja na kutafuta faida za kibiashara

kutokana na mauzo ya vijana wanaowafundisha kwenda klabu za
Ligi Kuu au madaraja mengine.


Upande mwingine timu za taasisi nazo zinaweza kuwa na utaratibu
wa namna hiyo, kuhakikisha wale wenye kiu ya kuwa makocha
mara wanapomaliza vipindi vya uchezaji soka wanapelekwa kwenye
mafunzo sahihi ya kuja kuwa makocha wa timu hizo au wakufunzi.


Serikali ihakikishe inashirikiana na TFF katika kuinua kiwango cha
makocha wetu nchini kwa kuwapeleka shuleni. Serikali na TFF
wanaweza kuiga mfumo uliofanywa na nchi ya Ujerumani.


Mwaka 2000 baada ya kutupwa mapema kwenye kundi lao la
michuano ya Mataifa ya Ulaya (Euro) likijumuisha Romania,
England, Ureno na Ujerumani, lilishuhudia ikiambulia vichapo
vikali na kudorora kwa soka lao.


Tangu hapo Ujerumani iliamua kuanza mpango wa kupata
makocha wapya, ambao wangetekeleza programu ya kusaka vipaji
nchi nzima.Mafanikio yao yalikuja baada ya miaka 14 ambapo walitwaa
Kombe la Dunia.

Katikati hapo walifanikiwa kufika fainali mwaka
2002 na nusu fainali ya kombe hilo mwaka 2006, kutwaa Euro na
Kombe la dunia kumetokana na mafanikio ya mipango ya kuandaa
makocha wa kizazi kipya. Hivi ndivyo wenzetu wanavyotafuta
mafanikio ya taifa. Mambo yanakwenda namna hiyo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Arteta na Lampard

Arsenal, Chelsea safi

SIMBA

Manara katudaganya mchana kweupe!!