Sevilla ngangari, Napoli wabanwa
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Europa, Sevilla wamefanya vyema kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali kwa kuwacharaza Fiorentina 3-0.
Wakicheza nyumbani, Sevilla walijilinda vyema na kushambulia, ambapo mabao yake mawili ya kipindi cha kwanza yalitiwa kimiani na beki wake wa pembeni, Aleix Vidal.
Mashindano ya mwaka huu yana umuhimu wa kipekee, kwa sababu bingwa ataingia moja kwa moja kwenye hatua za makundi za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao.
Bao la tatu lilitiwa kimiani na Kevin Gameiro sekunde 28 tu baada ya kuingia akitokea benchi na tangu hatua za awali za mashindano haya Sevilla walionekana kuyapa uzito mkubwa tofauti na baadhi ya timu, hasa za England.
Sevilla ndio walikuwa pia mabingwa mara mbili mfululizo, kwa mwaka 2006 na 2007. Hakuna timu iliyopata kushinda michuano hii mara nne, na Sevilla wanataka kuweka rekodi hiyo.
Fiorentina ndio walioanza vyema kuliko wenyeji, huku Mario Gomez akikaribia kufunga mara mbili ndani ya robo ya mwanzo.
Wengine waliokosa mabao ni pamoja na Matias Fernandez na mchezaji wa Chelsea aliye kwa mkopo Fiorentina, Mohamed Salah.
Fiorentina walimwingiza beki Micah Richards baada ya kipindi cha kwanza lakini hawakuweza kuubadili mchezo badala yake wakachapwa la tatu.
Mechi ya mkondo wa pili itafanyika Florence Alhamisi ijayo na mshindi kwa uwiano atacheza na ama Napoli au Dnipro Dnipropetrovsk katika fainali itakayofanyika Warsaw, Poland.
NAPOLI WABANWA NYUMBANI
Dnipro Dnipropetrovsk wamewanyong’onyesha washabiki wa Napoli waliojazana kwenye uwanja wa nyumbani, baada ya kusawazisha dakika 10 za mwisho.
Katika nusu fainali hii ya Ligi ya Europa, Napoli walikuwa wakiongoza kwa bao moja hadi wakati huo, kwa bao lililofungwa na David Lopez Silva na Kocha Rafa Benitez alinekana kuwa na uhakika wa ushindi.
Silva alifunga kwa kichwa baada ya mpira wa kona wa Lorenzo Insign katika dakika ya 50.
Dnipro kuona mambo magumu walimnyanyua Yevhen Seleznyov kutoka benchi na ndiye aliyekuja kusawazisha aliposhika mpira wake wa kwanza, kutokana na majalo ya Artem Fedetskiy.
Napoli, katika Serie A wapo pointi nne nyuma ya mstari wa kufuzu kwa UCL msimu ujao.
Benitez anataka kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutwaa taji la Uefa au Europa akiwa na klabu tatu tofauti.
Kocha huyu wa zamani wa Liverpool alitwaa mataji akiwa na Valencia 2004 na kisha akiwa kocha wa muda wa Chelsea miaka miwili iliyopita.