in

Ligi Kuu England ni ipi hasa?

Tofauti kati ya Uingereza na England

LIGI Kuu ya England (EPL)  iliyoingia mzunguko wake wa tano wikiendi iliyopita ina mengi ya kufundisha, kutokana na mvuto wake na jinsi wachezaji mahiri kutoka kona tofauti za dunia wanavyoitumikia.

Hii ndiyo ligi inayoongoza kwa umaarufu duniani, ikifuatiwa na zile za Hispania (La Liga), Italia (Serie A), Ujerumani (Bundesliga), Ufaransa (Ligue 1) na nyinginezo, huku ile ya Marekani – Major League Soccer (MLS) nayo ikipaa kwa umaarufu.

Ipo tofauti kubwa sana kusema Ligi Kuu ya England na Ligi Kuu ya Uingereza. England si Uingereza na Uingereza si England. Ilivyo ni kwamba England ni sehemu ya Uingereza na kwa Kiingereza, Uingereza ni Great Britain au United Kingdom.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ndicho chombo ambacho kimetilia mkazo kutumia jina sahihi la ligi hiyo na nimekuwa nikifanya kazi humo ya kuchambua soka mechi zinapochezwa na nimeona ni muhimu kueleza umma uelewe tofauti iliyopo.

Kuweka kumbukumbu sawa ni kwamba hakuna kitu kama Ligi Kuu ya Uingereza au Ligi ya Uingereza kwa maana hiyo, kwa sababu mataifa yanayounda Himaya ya Uingereza yana ligi zao na wala hakuna Ligi ya Muungano.

Falme ya Uingereza ambayo tangu 1952 ipo chini ya utawlaa wa Malkia Elizabeth II inajengwa na mataifa manne – England, Scotland, Wales na Ireland Kaskazini na wakati mwingine hurejewa kama  United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland, lakini kwa ujumla wake wenyewe hupenda kuiita kwa kifupi UK.

Soka iliyo maarufu zaidi ni hii ya England, moja ya vipande vinne vya Uingereza na hutambulika zaidi kama English Premier League na wakati mwingine kutokana na umaarufu wake wa tangu kitambo huitwa tu Premier League.

Nilitangulia kusema kwamba kila nchi kwenye falme hii zina mfumo wao wa michezo na soka, lakini niharakishe kueleza kwamba Wales iliyo magharibi mwa England na yenye mwingiliano mkubwa zaidi na England mchezo wake mkuu ni rugby, ambao umekuwa pia ukirejewa kama soka sehemu nyingine.

Soka tuijuayo ya Chama cha Soka (FA) kule si maarufu na wala hakuna timu nyingi, ndiyo maana wao wana Ligi ya Rugby na pia hakuna timu nyingi za soka huko.

Ni kwa msingi huo, England imezikubalia timu za Wales ziingie kwenye EPL na kwa wafuatiliaji wazuri wa soka watamaizi kwamba pamekuwapo timu mbili EPL kutoka Wales, nazo ni Cardiff na Wales.

Hata hivyo, Cardiff au Bluebirds waliopanda daraja kwa mara ya kwanza msimu wa 2013/14 walicheza msimu huo tu na kushushwa kutokana na kushika moja ya nafasi tatu za mwisho miongoni mwa timu 20 za EPL na sasa wapo kwenye Championship, inayoweza kusemwa ni Ligi Daraja la Kwanza au lile la zamani la pili kwa Tanzania. Wana uwanja wao uitwao Cardiff City Stadium walikohamia mwaka 2009 kutoka Ninian Park.

Swansea ambao jina lao kamili ni Swansea City Association Football Club au Swansea AFC na jina la utani ni The Jacks au The Swans, walipanda 2011 na kuwa timu ya kwanza ya Wales kucheza EPL. Katika mashindano ya Ulaya huiwakilisha England, japokuwa zamani walikuwa wakiiwakilisha Wales.

Hawa wanacheza mechi zao za nyumbani katika uwanja wao – Liberty Stadium na kwa sasa ndiyo timu pekee kutoka Wales katika EPL. Hata hivyo Wales wanayo timu ya taifa ya soka – The Dragons  na ipo chini ya Football Association of Wales (FAW).

Ni huko wanakotoka wachezaji kama Gareth Bale aliyeuzwa kwa bei ghali zaidi na anayeshikilia rekodi ya dunia sasa akiwa Real Madrid, Aaron Ramsey wa Arsenal, Ashley Williams wa Swansea. Wales hawatambuliki kwenye michuano ya Olimpiki, hivyo wachezaji wake hujiunga na wa England kama Zanzibar wanavyoingia Tanzania kwenye michuano mbalimbali ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Scotland waliopiga kura ya kujitoa au kubaki UK na kuamua kubaki humo, licha ya hayo wanayo ligi yao na wachezaji wao kwa namna yoyote ile hawaichezei England. Ligi yao kuu –  Scottish Professional Football League iliyochukua nafasi ya Scottish Premier League 2013 ni maarufu kiasi na wanajiwakilisha wenyewe Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) na Fifa.

Ligi yao, tofauti kabisa na ya England, ina timu 12 wakati ile ya daraja la chini yake – Scottish Championship – ina timu tano tu. Celtic ni maarufu kwani imeshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na msimu wa karibuni waliwafunga Barcelona. Hawa walikuwa na kocha maarufu Neil Lennon aliyechoka makombe ya ubingwa wa nchi akang’atuka na sasa anataka kufundisha klabu za England, hata kama za daraja la chini kama Fulham na Cardiff.

Ireland Kaskazini pia wana mfumo wao tofauti wa ligi ya soka, hivyo kwamba itakuwa makosa makubwa kuendelea kusema ‘Ligi Kuu ya Uingereza’ isiyokuwapo. Ireland Kaskazini (tofautisha na Ireland walio nje ya Uingereza) wana mfumo wa ligi katika ngazi tatu – wakubwa, wa kati na wadogo.

Wamejigawa zaidi kiutawala kwa soka, kwani kuna vyama vinne vinavyosimamia mchezo huo, navyo ni North East Ulster Football Association (pia ikijulikana kama County Antrim & District Football Association), Mid-Ulster Football Association, North West of Ireland Football Association na  Fermanagh & Western Football Association.

EPL inatamba kwa sababu ya mvuto wake, matangazo ya televisheni na kampuni nyingi kuingia udhamini kwenye soka yake na timu kubwa zaidi zinazojulikana hata nyumbani Afrika Mashariki ni Manchester United na mahasimu wao Liverpool, Manchester City waliopanda baada ya kupata dola za mafuta, Chelsea na Arsenal.

Ligi hii imevutia wachezaji wengi kutoka mabara tofauti, ikiwamo kwetu Afrika, wakiwamo akina Yaya Toure, Didier Drogba lakini pia wa Ulaya, Marekani na Asia kama Thierry Henry, Robin Van Persie, Wayne Rooney, David Silva, Sergio Aguero, Clint Dempsey, Tim Howard bila kuwasahau walioingia kiangazi cha mwaka huu, Radamel Falcao, Angel Di Maria na wengineo.

Mfumo wa ligi hii ni kuanza Agosti na kumalizika Mei ya mwaka unaofuata, mechi zikijaa ufundi, ujuzi pasipo kuacha vituko vya watu aina ya Mario Balotelli, Joey Barton,  Sir Alex Ferguson, Paolo Di Canio, Roberto Mancini na Jose Morinho mwenye majina mengi kama The Only One, The Special One na The Happy One.

NB-Hii habari niliichapisha miaka michache iliyopita, kufuatia mada hii kuwa maarufu miongoni mwa wasomaji wangu, basi, nimeirudia tena.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Vita ya kubaki EPL

Vita kubaki EPL ngumu

Mikel Arteta bado anadaiwa na Arsene Wenger

Mikel Arteta bado anadaiwa na Arsene Wenger