Wakati namwandikia barua Jamal Malinzi, akilini mwangu kuna mtu alikuwa anapita kila wakati, Taswira yake ilikuwa inakuja, mpaka nikawa na shauku ya siku moja kupata nafasi ya mimi kumwandikia barua na yeye.
Barua ambayo itakuwa na maswali mengi sana lakini swali kuu litabaki ni kwanini hakufanikiwa kucheza ligi kwenye nchi zilizoendelea kimpira? Kwanini uliipa ruhusa miguu yako kuzeekea hapa?
Miguu ambayo ilikuwa na nguvu kubwa, miguu ambayo haiendani na eneo ambalo unatoka, eneo ambalo watu wengi huamini kuwa linatoa watu rojorojo kwa sababu ya wao kula urojo sana. Tuachane na hayo, ilikuwa utani tu! Usinune rafiki yangu Nadir Haroub “Cannavaro”.
Miguu yako ilikuwa haina urojo hilo nalikumbuka sana kaka yangu Nadir Haroub ndiyo maana tuliamua kukubatiza jina la Cannavaro, beki mahiri wa Italy ambaye aliwahi kuchukua ballon d’or, Hii inaonesha kuwa wewe ulikuwa mahiri sana.
Katika hadithi nzuri na ya kusisimua ni hadithi ya mafanikio ya Nadir Haroub “Cannavaro” katika ardhi ya nchi hii. Ndiye mchezaji pekee mwenye mafanikio makubwa tangu miaka 2000 mpaka 2020. Ndani ya miaka 20 iliyopita hakuna mchezaji mwenye mafanikio makubwa kwenye soka la ndani kama Nadir Haroub “Cannavaro”.
Najua na nina kupa heshima kwa hilo kuwa una mafanikio makubwa sana kaka yangu, hongera sana kwa hilo. Wewe ndiye mchezaji ambaye una mataji nane (8) vya ligi kuu Tanzania bara, una vikombe vine (4) vya ngao ya jamii, una vikombe viwili (2) vya Tusker Cup, umebeba vikombe viwili (2) vya Cecafa na kikombe kimoja cha Azam Federation Cup.
Kwa kifupi kaka yangu Nadir Haroub “Cannavaro” una vikombe 17 ulivyobeba kwenye soka lako tangu uanze kucheza ligi kuu Tanzania bara mwanzoni mwa miaka ya 2000. Narudia tena kukupongeza sana kwa kubaki kuwa mchezaji pekee mwenye mafanikio makubwa hapa nchini kwa kipindi cha mwaka 2000 mpaka mwaka huu wa 2020.
Mafanikio haya yalichangiwa sana na ubora wake kwa kiasi kikubwa na miguu yako imara, miguu ambayo iliwahi kupunguza kasi ya Samuel Etoo, ikadhoofisha ubora wake na mwisho wa siku akakufuata na kukuomba jezi kama kumbukumbu ya yeye kuwahi kukutana na beki imara.
Naendelea kukupongeza kaka, wewe ulihakikisha ukuta wa Yanga ni imara muda mwingi, kuna wakati ulikuwa unatetereka bila uwepo wako. Kuna wakati hata mioyo ya mashabiki wa Yanga na timu ya taifa ilikuwa haiwezi kutulia bila uwepo wako.
Wewe ulikuwa zaidi ya beki, wewe ulikuwa kiongozi imara, kitambaa cha unahodha kilikuwa kwenye mikono salama kabisa. Kitambaa cha unahodha kilijihisi fahari kubwa kuwepo kwa mkono wako.
Wewe ulikuwa mchezaji imara sana, mchezaji bora, mchezaji mwenye hekima kuanzia kichwani mpaka kwenye miguu. Moyo wako ulikuwa wenye busara na miguu yako ilijaa ukatiri kwa washambuliaji wengi, hakuna mshambuliaji ambaye angependa kukutana na beki kama wewe kwa kipindi hicho.
Kwa kifupi ulikuwa mchezaji ambaye ulikuwa umekamilika haswaa, ukamilifu wako unaleta maswali mengi sana ambayo naulizwa na wachezaji wanaochipukia kwa sasa, swali lao kubwa ni kwanini hukufanikiwa kucheza ligi ya nje ya nchi kama ambavyo kina Simon Msuva na Mbwana Samatta walivyofanikiwa kucheza?
Macho yao yanawaonesha kuwa ulikuwa na uwezo wa kufika huko , lakini ugumu wa majibu wa hili swali kwanini hukufanikiwa. Mimi sina jibu sahihi zaidi ya mimi kubashiri majibu ya swali hili.
Nimechoka kubashiri kuwa wewe hukuwa na meneja sahihi wa wewe kuipeleka miguu yako kwenye ligi ya nje. Inawezekana kabisa labda malengo yako yalikuwa kucheza hapa , nabashiri tu sina uhakika . Uhakika unao wewe , kwanini hukufanikiwa kucheza ligi ya nje pamoja na kuwa na kiwango bora?