lakini kuondoka kwangu kumekuja baada ya miaka 7 ya kutumikia klabu hiyo. Nimeondoka nikiwa Baba ambaye nimetimiza ndoto zangu zote na Man City…
Aliyekuwa nahodha wa Manchester City, Ilkay Gundogan amekiri kumwambia kocha wake Peo Guardiola kuwa anaondoka klabuni hapo na kwenda kujiunga na Barcelona ya Hispania. Katika mazungumzo yake na vyombo vya Habari imethibitika kuwa Gundogan hakuona sababu yoyote ya kukata ofa ya Barcelona, huku akiwa ametwaa kila kitu katika klabu ya Manchester City.
Uamuzi wa kuondoka Manchester City ulikuwa mgumu kwa Nyota huyo lakini alikuwa na Sababu nyingi za Msingi katika historia yake ya kucheza kandanda. Kwa upande mwingine Barcelona wanaweza kujisikia huzuni kushindwa kumrudisha staa wao Lionel Messi baada ya Nyota huyo kwenda Ligi ya Marekani akijiunga na Inter Miami, hata hivyo kufanikiwa kuinasa saini ya Ilkay Gundogan ni jambo la kujivunia ingawa limemwachia uchungu Pep Guardiola ambaye alikuwa na matumaini nyota huyo angeongeza mkataba wake wa kutumikia Man City.
Kumsajili Ilkay Gundogan ni ujumbe kuwa Barcelona bado inao ushawishi katika soka la Ulaya licha ya matatizo ya kiuchumi waliyonayo.
Baada ya kuthibitisha usajili wa nyota huyo Mjerumani mwenye asili ya Uturuki, Barcelona na Gundogan wanaweza kuanza maisha mapya bila Messi. Lakini kuondoka kwake Man City kumeacha huzuni kama ilivyothibitishwa na nyota huyo kupitia makala yake katika ambayo TANZANIASPORTS imefanikiwa kuyasoma. Katika makala hayo Gundogan amewashukuru Man City kwa muda wote waliokuwa pamoja na mashabiki wake.
Gundogan anasema, “nilipojiunga kwa mara ya kwanza, nilikuwa kijana mdogo, sikuwa na watoto, lakini nilikuwa na ndoto nyingi. Ni vigumu kwangu kuamini kuwa nimeondoka, lakini kuondoka kwangu kumekuja baada ya miaka 7 ya kutumikia klabu hiyo. Nimeondoka nikiwa Baba ambaye nimetimiza ndoto zangu zote na Man City.
MAISHA YAKE MAN CITY
Katika kipindi alichokuwa Man City, kiungo huyo ametwa makombe matano ya EPL, mawili ya FA, manne ya Carabao, na hivi karibuni ameongeza taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Makombe yote hayo ametwaa akiwa na kocha wake Pep Guardiola ambaye alikuwa anasaka taji la UEFA tangu alipoondoka Barcelona.
Gündogan ametoa sifa nyingi kwa Pep Guardiola kwa mafanikio makubwa aliyopata kama mchezaji.
Nyota huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Pep Guardiola.
Gundogan amekiri kuwa alikuwa na wakati mgumu kumwambia kocha wake kuwa anaondoka klabuni hapo.
“Jambo moja gumu lilikuwa kuzungumza na Pep Guardiola ni namna ya kumwambia naondoka Man City. Nilipatwa na kigugumizi lakini nilitakiwa kumweleza. Ninachoweza kufanya sasa ni kuwaambia Man City asanteni sana kwa miaka 7 yenye mafanikio. Ni mafanikio mengi, si kwa sababu ya kile tulichofanya msimu huu au kwa makombe yote, lakini kwa uamuzi wao wa kunisajili toka Ujerumani na kuja England. Sitasahau nilipoumia enka msimu wa mwisho nikiwa Borussia Dortmund na kulazimika kufanyiwa upasuaji. Nilikuwa na hofu kwamba Man City wangejitoa katika mpango wao wa kunisajili. Lakini Pep Guardiola alinipigia simu na kuniambia nisiwe na wasiwasi kwani hakuna mabadiliko katika usajili wangu. Man City walikuwa tayari kunisubiri bila kujali ingechukua muda gani hadi kupona,
“Hayo yasingewezekana kama si juhudi za Pep. Kuna wakati alikuwa anataka makubwa sana kwa kucheza vile atakavyo kiasi kwamba ilikuwa vigumu kiakili kumudu shinikizo lake. Lakini kila mmoja anapoelewa kile anachotaka, kila kitu kinakwenda vizuri na kuleta furaha uwanjani. Lazima kusimamia,kuuhisi na kuamini mfumo wa Pep Guardiola, pamoja na kutumia jitihada na maarifa. Daima nilikuwa karibu na matakwa yake.
NI BARCELONA TU
Gundogan anasema kuwa alichukua uamuzi wa kuondoka Manchester City na kumwacha kocha ambaye ametwaa naye mataji mengi akiwa na sababu. Wengi wanatamani kujua ni kwanini ilikuwa hivyo.
“Kama kuhama Man City, basi ni timu moja tu ningeifikiria hapa duniani, ni Barcelona tu. Tangu utotoni niliota ndoto siku moja nitavaa jezi za Barcelona. Najiamini sasa bado ningali na miaka kadhaa ya kucheza mpira wa miguu kwa kiwango cha juu na kuirudisha Barcelona pale inapostahili. Pia litakuwa jambo zuri kuungana tena na Lewandowski kucheza chini ya kocha ambaye nilipenda uchezaji wake. Nilipozungumza na Xavi kuhusu mipango mipya ya timu, ilikuwa jambo la kawaida, na mazungumzo yalikuwa ya kawaida tu. Mambo mengi tunafanana katika tabia zetu namna tunavyouona mchezo.
CHANGAMOTO MPYA
Gundogan anasema aliamua kuondoka Manchester City ili kutafuta changamoto mpya. Manchester City walimpa ofa ya mshahara wa pauni million 12 kulinganisha na ofa ya Barcelona ya pauni Milioni 9 pamoja na mkataba wa miaka miwili na nyongeza ya mwaka mmoja. Man City wao walimpa ofa ya mwaka mmoja tu na nyongeza ya mwaka mwingine.
Comments
Loading…