in , ,

JUA LIMEZAMA KWA DAVID DE GEA

BINGWA wa fasihi raia wa England, William Shakespeare amewahi kuandika “all good things must come to an end”. Kwamba hakuna lililo na mwanzo likakosa mwisho ama mambo yote mazuri lazima yafikie mwisho wake. Hilo ndilo linalomtokea golikipa wa Kihispania David De Gea. Nyanda huyo ameaga rasmi mashabiki wa Manchester United, na kuwatakia heri wachezaji wenzake. Katika ujumbe wake wa kuaga inaonekana wazi ana huzuni na hakutegemea kulifanya hilo mwaka huu. Hata hivyo imeshatokea na David De Gea anaondoka klabuni hapo. Huyu ni golikipa ambaye alikuwa Moto wa kuotea mbali lakini zama zake kwa hakika zimefika tamati. 

TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu ambayo yamechangia Nyota huyo kutupiwa virago na Mashetani Wekundu wa Old Traford. 

1  Kuachwa Kombe la Dunia 2022.

Kama kuna kocha ambaye alituma ujumbe kwa Man United na golikipa huyo ni Luis Enrique. Wakati akitangaza kikosi cha timu ya Taifa ya Hispania jina la Davis De Gea halikuwepo. Badala yake alimwita golikipa wa Atletic Bilbao, Unai Simon.

Tanzania Sports

Kocha Luis Enrique alifanya uamuzi ambao ni sawa na kutoa ujumbe kwa Man United kuwa golikipa wao aliyesadikika kuwa nambari moja hakuwa na kiwango ama ufundi wa kutumikia Hispania. Bahati ni kwamba siku chache baadaye ilifahamika kuwa Luis Enrique alimpigia simu kumweleza kuwa hatamwita kikosini na bila shaka alimweleza Sababu.  Kufika hapo ni kama Zama zake zilifika mwisho kwenye kikosi Cha Hispania na hata kocha mpya De la Fuerte hajaonekana kuonesha nia ya kumpa namba katika kikosi chake. 

2. Makosa ya mara kwa mara.

David De Gea amefanya kazi nzuri mara kadhaa na kuipa uhai Man United. Lakini  kufungwa au kuruhusu kufungwa kutokana na makosa yake mara kwa mara limekuwa jinamizi ambalo Man United imeishi nalo na Sasa Eric Ten Hag ameamua kuachana nalo. Man United wamepita nyakati ngumu lakini makosa binafsi ya wachezaji akiwemo De Gea yamewagharimu Kupata matokeo mazuri.

3. Uwezo wa kucheza kisasa.

David De Gea ni golikipa wa kizamani. Makipa ambao walikuwa na kazi ya kukaa golini kulinda lango na kuokoa michomo na hatari zote zilizoelekezwa langoni mwao. Hata hivyo soka la kisasa linawanyima nafasi makipa wa aina hiyo. Makipa wanatakiwa kuwa kama mabeki namba tano (beki wa mwisho), sawa na kuwa na uwezo wa kucheza kwa miguu. Hilo Hilo lilimwondoa Joe Hart pale Ma. City. David De Gea ana tatizo la ubora wa kucheza kwa miguu (foot works). Ni kipa mzuri wa kuondoa michomo lakini anakabiliwa na kibarua kigumu kucheza katika mtindo wa kisasa. Golikipa anatakiwa kuwa sehemu ya mchezo, kupanga mashambulizi, kuingia katika mfumo wa kutengeneza na kucheza kitimu kama mmoja wa mabeki wa Kati. Kipa wa sasa anatakiwa kusogea hadi nje ya eneo la 18 na kupigiana pasi pamoja na kutafuta mbinu za kutengeneza mabao. Vile De Gea si mzuri kuanzisha shambulizi kwa mipira mirefu kama walivyo wenzake  Alisson Becker (Liverpool) au Ederson (Man City). Changamoto ya De Gea ndiyo ilikuwa kwa Aaron Ramsdale wa Arsenal, licha ya uwezo mkubwa wa kuokoa michomo na hatari zote zilizoelekezwa langoni mwake lakini alikuwa na upungufu wa kucheza kwa miguu (foot works). Hata Ramsdale huyu si yule, ameimarisha uwezo na kuwa miongoni mwa makipa wa kisasa. Makipa ambao wanatakiwa kuwasaidia mabeki watatu wanaolinda timu yao huku wengine wakisogea mbele kushambulia.

4. Ushindani wa kizazi kipya. 

Ni wazi De Gea anamepigwa kumbo na kizazi kipya Cha soka. Makipa wanaozalishwa Sasa ni wale wanaendana na mifumo ya kisasa. Mifumo ambayo inawaondoa kuwa makipa wa kukaa langoni pekee na kuwa mabeki wanaosaidia kuondoa hatari zote kwa kushiriki kusogea mbele zaidi ya eneo lao,kupigiana pasi na kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza. Eduardo Mendy, David De Gea hawajabadilika kama Sommer wa Bayern Munich ambaye zamani hakuwa na uwezo mkubwa wa kucheza na miguu. Lakini sasa amekuwa mtamu kiuchezaji baada ya kukutana na golikipa mtaalamu Manuel Neuer mkali wa makipa na bingwa wa kushambulia lango la adui kwa pasi ndefu.

5. Zama mpya za kocha ETH.

Tanzania Sports

Jina la Andre Onana ndilo linalotajwa pale Old Traford. Huyu ni kipa aliyefanya kazi na Eric Ten Hag wakiwa Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Wanajuana vizuri, ubora, udhaifu na namna walivyopata mafanikio. Andre Onana anaelekea Man United ni dhahiri kuwa uwezo wake wa kucheza kwa miguu (foot work) umempa dili la kuwindwa na timu mbalimbali. Inter Milan wana kibarua cha kumbakiza Nyota huyo kwani fedha za Man United zimelekezwa kwake. Onana ana uwezo wa kupangua michomo,kupanga mashambulizi, kuingia katika mfumo wa uchezaji kama beki au kiungo wa nyuma. Ameonesha hilo mara nyingi na wakati mwingine kudhaniwa anahatarisha lango la Inter Milan. ETH alifungwa bao nyingi na wapinzani wake wakuu ambao alidhamiria kutikisa ufalme wao, Liverpool na Man City, lakini eneo la golikipa lilimsaliti vibaya mno. Sasa, baada ha msimu mmoja tu amwirudisha Man United kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Sasa anaunda kikosi cha kusaka taji la kwanza la EPL. Hizi ni Zama mpya ambazo zinawaondoa wachezaji wengi waliodhaniwa watadumu klabuni.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
THE PRESIDENT

TFF WANGELETA SUPER LEAGUE YAO

Tanzania Sports

Zidane anasajili wachezaji wake Real Madrid