UMEFIKA MUDA SASA KUBIDHAISHA MCHEZO WA BAO KIMATAIFA
Hakika ni wazi kabisa kwamba mchezo wa bao ni mchezo maarufu sana miongoni mwa wakazi wa miji ya ukanda wa Pwani ya Tanzania. Mchezo huu umekuwa unachezwa sana na watu wenye umri wa makamo ambao wamekuwa wanaucheza katika vijiwe vya kahawa ambapo wamekuwa wanakutana na kupiga stori na kubadilishana mawazo mbalimbali juu ya masuala ya kijamii. Mchezo huu una historia ndefu na wakazi wa Tanzania na kwa maoni yangu unafaa kutangazwa kama mchezo wa kitaifa na ukuzwe ndani na nje ya nchi kama ni mojawapo ya urithi wa kitaifa.
Bao ni mchezo wa jadi ambao unaochezwa baina unaochezwa na wachezaji wawili. Mchezo huu umesambaa sana katika nchi za afrika mashariki ikiwemo Msumbiji, Kenya, Malawi, Komorro,, Congo na Burundi. Kwa nchini Msumbiji mchezo huu unafahamika pia kwa jina la Mankala. Jina lenyewe la Bao linatokana na neno la Kiswahili “ubao” ikimaanisha ubao ambao unatumika kuchezea mchezo huo.Hakuna Ushahidi rasmi wa kihistoria juu ya ni lini mchezo huu ulianza rasmi ila una karne nyingi ukiwa unachezwa. Nakala ya ripoti ya msomi wa kifaransa aliyelikana kama Etienne de Flacourt ambaye alikuwa gavana wa Madagascar inaelezea kuwepo kwa mchezo kama huo ambao ulikuwa unapendwa na wakazi wa kaskazinimashariki mwa Madagascar. Baadhi ya wanahistoria hupinga kwamba mchezo huo unaozungumziwa ndio bao. Mshairi maarufu kwa jina la Muyaka bin Hajj kutoka Mombasa aliandika shairi “Bao Naligwa” katika miaka ya 1820 kusherehekea mchezo huo.
Mchezo huu umegusa hisia za watafiti wengi wa kimataifa ambao walitafiti juu ya mchezo huu na namna unaathiri saikolojia ya mchezaji ambavyo mchezo huu kwa sasa umeanza kupata mashabiki nje ya bara la afrika na unakuwa mkubwa. Mtaalamu wa mchezo huu huitwa bingwa au mda mwingine huitwa fundi.
Viongozi waasisi wa taifa hili walikuwa ni wachezaji wazuri wa mchezo huu wa bao kuanzia kwa Mwalimu Nyerere, Rashid Kawawa, Abeid Aman Karume, Ali Hassan Mwinyi na wengineo Inasemekana muasisi wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokutana na kiongozi wa taifa la China la wakati huo aliyekuwa anaitwa Mao Tse Tung walibadilishana dhana za michezo na mwalimu alipewa meza ya kuchezea mchezo wa tennis (Table Tennis) na Mao akapewa kifaa cha kuchezea mchezo wa bao. Hii inaonyesha wazi kwamba Mwalimu Nyerere alithamini sana mchezo wa bao na alitambua kwamba ni nembo ya taifa. Yasemekana hata aaliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume wakati anajeruhiwa na kuuawa alikuwa anacheza mchezo wa bao ndipo alipopigwa risasi.
Mchezo wa bao kwa mda mrefu umekuwa ni mchezo ambao unawaunganisha watanzania katika shughuli mbalimbali. Makundi ya watu katika nyakati tofauti wamekuwa wanaucheza mchezo huu kama sehemu ya kujiburudisha na pia sehemu ya kukuza urafiki na mahusiano mema katika jamii. Katika baadhi ya maeneo nchini hususani karibu na barabara ni kawaida kuwakuta wazee watu wa makamo wakiwa kwenye vijiwe vya kahawa wanakunywa kahawa
Imefika mda sasa mchezo huu kubidhaishwa kwani una vigezo toshelezi vya kubidhaika. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa michezo inatakiwa itengeneze mpango kazi wa mda mrefu ambao utaufanya mchezo huu kuwa ni bidhaa na kuwa ni nembo ya taifa hili. Mchezo huu unaweza ukabidhaika kwa kufanya mambo yafuatayo:
Kwanza Kuweka nguvu mchezo huu katika mashindano ya Umiseta na Umitashumta. Mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA ni mashindano makubwa sana ya michezo nchini kwa ngazi ya chini(grassroot). Kwa ujumla mashindano hayo hukusanya vijana wengi sana ambao hushiriki michezo mbalimbali na kuwepo kwa mchezo huu katika mashindano hayo kutaufanya uzidi kuwa maarufu katika kizazi cha sasa na utawafanya wavutike kwa wingi kushiriki kwani kuna dhana mbaya imeanza kujengeka kwamba mchezo huo ni mchezo wa watu wa makamo(wazee) na baadhi ya vijana wameanza kuuogopa. Halikadhalika katika bgazi ya vyuo mashindano ambayo ni ya vyuo nayo yawe yana mchezo huo kwani itazidi kuondoa hofu juu ya ushiriki katik mchezo huo.
Pili Kudhamini mashindano ya kitaifa na kimataifa. Serikali kupitia mfuko wa utamaduni idhamini rasmi mashindano ya kitaifa ya mchezo wa bao. Mchezo wa bao kwa kuwa ni nembo ya taifa na ni sehemu ya urithi wa nchi basi mashindano hayo yana sifa ya kudhaminiwa na serikali kupitia mfuko huo. Mashindano hayo yakiwa yana nguvu ya udhamini ya serikali yataweza kuwa yenye nguvu na mvuto kwani serikali ina mkono mrefu.
Tatu Kuweka bajeti kwa ajili ya mafunzo ya mchezo huu. Serikali iweke mafunzo ya mchezo huu kwa walimu wa michezo ambao wanapatikana nchi nzima pamoja na maafisa michezo ili waweze kufundisha mchezo huu katika ngazi tofauti. Mafunzo hayo yaende kwa awamu tofauti kwa mujibu wa mikoa tofauti. Serikali pia iweke miundombinu ya kutathmini maendeleo ya mafunzo hayo na namna walimu waliopewa mafunzo wanavyoyapeleka mafunzo hayo kwa wanafunzi hao. Halikadhalika serikali itoe motisha kwa walimu ambao watakuwa wananya vizuri katika kufundisha na kuuendeleza mchezo huo.
Nne Kufanya ushawishi mchezo huo uingizwe katika michezo inayochezwa katika olimpiki na michezo ya jumuiya madola. Mashindano ya olimpiki ni mashindano ya kilimwengu na mashindano hayo huwa yanafuatiliwa na mamilioni ya watu duniani na kama mchezo huo ukichezwa basi watu wengi watapenda kutaka kujua historia yake na wakifahamu historia yake basi wataweza kuuhusisha na Tanzania na hivyo nchi itakuwa imetangazika. Ushawishi wa kuingizwa mchezo huu kwenye mashindano hayo ni lazima ufanywe kwa juhudi za serikali kwa kiwango kikubwa.
Tano Kuwepo kwa vipindi vya runinga vya mchezo wa bao. Mchezo huu kwa sasa lazima uwe na vipindi vya runinga ambavyo vitakuwa vinaonyesha matukio ya mchezo hu una kufanyika kwa hilo kutahamasisha watu wengi sana kushiriki katika mchezo huo.
Mwisho niseme kwamba kubidhaishwa kwa mchezo huu kutaleta faida za kiuchumi na kijamii kwani kuna ajira za msimu zinazowahusisha watengeneza bao na wengineo watakaokuwa kwenye mnyororo wa thamani wa mchezo wa bao.
Comments
Loading…