in , , ,

Jerry Muro anavyoigawa YANGA

Hakuna shaka yoyote kwa sasa Yanga iko katika hali ambayo siyo tulivu kabisa kutokana na matokeo ambayo wanayapata ndani ya uwanja. Sare nne mfululizo!

Unapoteza alama nane tena timu ambayo inautaka ubingwa wa ligi kuu, timu ambayo inataka kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao, lazima kusiwe na utulivu.

Kwa muda huu nilijua kabisa Yanga inapigana kwa kiasi kikubwa kuleta utulivu kuanzia ndani ya timu mpaka nje ya timu, kwa pamoja Yanga izingumze lugha moja.

Unajua kwanini? ni kwa sababu ya mechi ya tarehe nane. Mechi ambayo Yanga wanaiwaza zaidi kuliko ubingwa. Kushinda kwao kunaweza kukawa zawadi kubwa kwa Yanga kuliko ubingwa.

Lakini huwezi kushinda mechi hii kama hakuna utulivu, kuna mambo mawili ambayo nilitegemea Yanga wayafanye ili walete utulivu ndani ya timu ya Yanga na nje ya Yanga.

Mosi, nilitegemea kuona viongozi wa Yanga kwa pamoja na wadhamini wao wakae na timu ili kuimarisha morali ndani ya kikosi cha Yanga. Morali ambayo ingefanya kikosi cha Yanga kibadilishe hizi sare kuwa ushindi.

Kwa sasa Yanga wanatakiwa kubadilisha hizi sare wanazozipata ili side ushindi. Hiki ndicho kitu cha kwanza kuelekea mechi dhidi ya Simba . Wana mechi tatu mkononi kabla ya mechi dhidi ya Simba.

Mechi ambazo walitakiwa kuzibadili kutoka kwenye kupata sare kwenda kwenye kupata ushindi. Kuzibadili sare hizi kuwa ushindi kulitakiwa kuwe na utulivu ndani ya timu .

Baada ya kuhakikisha utulivu ndani ya timu, viongozi wenyewe ndani ya klabu walitakiwa kushikamana kwa sasa, waonekane wako pamoja kwa sasa wakijenga nyumba moja.

Mshikamo huu wangeenda kuusubiri nje Kwa mashabiki. Wangehubiri injili ambayo ingewafanya mashabiki waje uwanjani, waiunge timu yao kwa nguvu zote.

Hapa ndipo jicho langu la kumtazama Jerry Muro linapoanzia. Tuanzie hapa wote kwa pamoja. Jana Jerry Muro alionekana na katibu mkuu wa Yanga ambaye ni mtendaji mkuu wa klabu, alionekana pia na Makamu mwenyekiti wa Yanga kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Walionekana wote kwa pamoja, wakaizungumzia Yanga kwa pamoja, wakajigamba sana kuhusu ukubwa wa Yanga, jambo ambalo lilikuwa bora na sahihi kabisa kwao.

Mwisho wa siku Jerry Muro akasema kuwa amerudi rasmi Yanga, kitu ambacho alikisema mbele ya viongozi wakubwa wa Yanga, katibu mkuu wa Yanga pamoja na makamu mwenyekiti wa Yanga.

Kauli ambayo ilipewa baraka na viongozi hawa wa juu kabisa wa klabu ya Yanga . Kuwa na katibu ambaye ni mtendaji mkuu wa klabu , makamu mwenyekiti ina maana kuwa una uongozi wa Yanga .

Picha ipi ambayo ilionekana nje ya mkutano ule wa waandishi wa habari ? Jerry Muro alikuwa amebarikiwa na viongozi wa Yanga kuja kurudisha hamasa nje ya uwanja kuelekea mechi ya Simba .

Kitu ambacho ni kizuri sana tena hakukuwepo na dhambi kwenye hilo. Yanga inahitaji sana hamasa kwa sasa kuelekea kwenye mechi ya Simba . Huu ndiyo ukweli na kumpata Jerry Muro ilikuwa karata sahihi.

Sasa watu tulianza kusubiri kitakachofuata baada ya ule mkutano na waandishi wa habari. Jerry Muro atafanyaje kazi yake sasa ya kuwahamasisha mashabiki .

Hili ndilo swali kubwa ambalo kila mmoja wetu alikuwa anatamani jibu lake. Jibu ambalo limekuja ni jibu ambalo linatia maswali maswali mengi ya ziada maswali ambayo yanaleta mgawanyiko ndani ya klabu.

Jerry Muro akizungumza na Wasafi Fm kwenye kipindi cha Sports Arena amedai kuwa Yanga ina kocha mbovu, kocha wao Luc Eymael siyo mzuri ukilinganisha na kocha Boniface Mkwasa, pia wachezaji kama Molinga na Yikpe ni wabovu.

Inawezekana sawa Wachezaji wa Yanga ni wabovu, kocha mbovu. Inawezekana kabisa ni sahihi na Jerry Muro akawa sahihi kabisa. Swali la kujiuliza ni hili, Ukianza kuzungumza ubovu wa wachezaji waliopo sasa hivi kwa muda huu ambao dirisha La usajili limefungwa inasaidia?

Kama haisaidii kipi Yanga walikuwa wanahitaji? kuzungumza ubovu wa wachezaji wao hadharani? bila shaka jibu ni hapana. Kitu pekee ambayo Yanga wanahitaji ni kurudi mchezoni, Kurudi mchezoni kwa kuzibadilisha sare kuwa ushindi.

Kurudi mchezoni kwa kuongeza hamasa nje ya uwanja, Jerry Muro ana nguvu kubwa sana , tazama hii picha, Jana kwenye mkutano na waandishi wa habari alikuwa na mtendaji mkuu wa klabu akawa na makamu mwenyekiti wa klabu, kwa picha ya haraka haraka klabu imeamua kutumia nguvu na ushawishi wake kwa ajili ya kurudisha morali ndani ya timu (kwa wachezaji) mpaka nje ya timu (Kwa mashabiki, wanachama na viongozi)

Kwa hiyo alipaswa kutumia vizuri mwamvuli wa mkutano waa jana na waandishi wa habari kudumisha mapokeo hayo. Alichoenda kukiongea Leo kwenye redio kinaenda kuigawa Yanga. Sasa hivi kaibua mjadala mpya ambao ulikuwa hautakiwi kuelekea kwenye mechi hii. Mjadala wa kocha fulani siyo sahihi na kocha fulani ni sahihi, Mchezaji fulani mbovu mchezaji fulani ni mkali.

Mjadala ambao siyo muda sahihi kwa sasa hivi, Mjadala pekee ambao ulikuwa unahitajika kwa sasa hivi, timu ya Yanga inaanza rasmi kubadilisha sare ziwe ushindi. Wanafanyeje? timu irudi na morali, mashabiki warudi na morali wote wazungumze lugha moja ila sasa hivi lugha zinazozungumzwa ni mbili ambazo hazitoleta maelewano katika ujenzi wa mnara wao wa babeli ya jangwani.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Zamu ya Anthony Joshua na Tyson Furry?

Tanzania Sports

Mabingwa Ulaya sasa patamu