Awali tulitangaza kuhusu ujio wa Makocha wa kikapu toka Marekani kuja kufundisha timu yetu ya Taifa, ambao ni Albert Sokaitis (Kocha Mkuu) ambaye ni Kocha mwenye uzoefu wa miaka 24 kwa sasa ni Kocha Mkuu wa timu ya Chuo Kikuu cha Post huko huko Marekani katika jimbo la Connecticut. Pia amewahi kufundisha timu na kuendesha mafunzo nchi za Uchina, Lebanon, Ugiriki na Japan.
Ambaye atasaidiwa na Kocha Jocquis L. Sconiers ambaye nae ana uzoefu wa miaka mingi na kwa sasa ni Kocha Mkuu Msaidizi wa timu ya Chuo Kikuu cha Post huko Marekani katika jimbo la Connecticut.
Katika utekelezaji wa mpango huo katika awamu ya kwanza Kocha Sconiers anatarajiwa kuwasili nchini leo tarehe 02/11/2012 na ataelekea Tanga siku inayofuata katika Mashindano ya Kombe la Taifa ili kuchagua wachezaji watakaonda timu za Taifa (wanawake na wanaume) na baada ya hapo ataanza mafunzo rasmi kwa timu zote mbili tarehe 5/11/2012. Kocha Mkuu Sokaitis atakuja nchini baadae kuungana na Sconiers ili kuendeleza mafunzo haya katika mpango wa maendeleo ya kikapu wa miaka 4, ambao tutakuwa tunaufanyia tathimini kila baada ya miaka 2.
Awamu hii ya kwanza ya mpango wa mafunzo unadhaminiwa na watu wa Marekani kupitia ubalozi wao hapa Tanzania, tunawashukuru sana watu wa Marekani.Afisa wa mambo ya Umma wa ubalozi wa Marekani nchini ndugu Roberto Quiroz ndio atakuwa mgeni rasmi katika kufungua kambi hii ya timu ya Taifa itakayofanyika katika viwanja vya Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Masaki.
Tunaomba wadau wote mtuunge mkono kwa hali na mali kufanikisha mpango huu wa mafunzo kwa timu ya Taifa na kwa makocha wetu wazalendo kwa faida ya vijana wetu na Taifa letu.
Comments
Loading…