Kelele tulizipiga sana, tuliandika sana, watu wakaongea sana kwenye
redio kama ni wimbo ungekuwa wimbo unaohusu kuhamasisha wakazi wa
Kariakoo wamiliki viwanja vyao binafsi.
Viwanja ambavyo vingewawezesha watu wa Kariakoo waondokane na adha ya
kuomba omba kila wakati.
Ni aibu kubwa sana vilabu kama Simba na Yanga vyenye umri mkubwa kuwa
vinaomba omba viwanja na wakati mwingine kunyimwa na wamiliki.
Miaka yao ni mingi mno, umri wa mtu mzima ambaye angefaa kuwa na
maendeleo makubwa sana, maendeleo ambayo yangemfanya aishi kwa amani
na furaha kwenye umri huu alionao.
Lakini imekuwa tofauti sana kwao, hakuna maendeleo makubwa ndani ya
hivi vilabu vya Simba na Yanga ingawa vina umri mkubwa sana.
Inasikitisha na kuuma pale unapogundua hata viwanja vya mazoezi
havijawahi kujengwa na vilabu hivi. Wamekuwa wakipoteza pesa nyingi
sana kukodi viwanja vya mazoezi kila uchwao.
Tuliimba sana huu wimbo wa kuhamasisha, wimbo wetu ukaonekana kama
umewaingia viongozi wa Simba na Yanga, habari mpya zikaanza kupenyeza
kwenye ngoma za masikio yetu.
Habari ya Bunju ilikuja kwa kasi sana, tukaoneshwa shamba ambalo Simba
walinunua kwa ajili ya kujenga Bunju Arena, wanachama wakafurahia hiyo
habari
Wakahamasika vya kutosha hata baada ya wao kutakiwa na viongozi kubeba
panga ili wakafyeke shamba la Bunju walienda , hii yote ilikuwa
kujitolea kwa ajili ya timu yao.
Hii yote ilikuwa kwa ajili ya kukwepa masimango mengi ya wao kutokuwa
na uwanja, kiu yao kubwa ilikuwa kuona timi yao ikiwa na uwanja wake
ambao utakuwa unawafanya wawe huru kuutumia.
Hata baada ya kuombwa kuchangia mifuko ya simenti, hawakusita kutoa
hata mfuko mmoja wa simenti. Nafsi zao zilihamasika sana kichwani mwao
walikuwa na ramani ya Bunju Arena.
Ramani ambayo ilikuwa inaonesha jinsi ambavyo uwanja wao utakuwa mzuri
tena wa kisasa, nyasi za bandia ziliagizwa ndipo hapo moto ukazidi
kuwa mkali kwenye mioyo ya watu.
Kila mtu alihamasika sana, ilionesha wengi walikuwa tayari kutoa hata
mia moja kwa ajili ya kuisaidia klabu imiliki uwanja wao.
Lakini mwisho wa siku ukali wa moto umeanza kupungua, miaka mingi
imepita tangu watu wafyeke nyasi kule Bunju lakini hakuna hata tofali
moja lililosimama kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa Bunju Arena.
Hata zile simenti zilizotolewa kuna hatari kubwa zimeishia muda wake
wa matumizi, vitu vingi vimebadirika na vinaenda kwenye kasi ndogo
tofauti na kasi ya mwanzo.
Ndiyo maana niliposikia kasi waliyoanza nayo Yanga kule Geza Ulole
nilitamani kuupa nafasi kwanza muda.
Niliamini muda una majibu yote muhimu kuhusu na hicho kitu, jiwe la
msingi liliwekwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na hostel ambao
ulitakiwa kuanza mara moja.
Na huu ujenzi ulikuwa nje ya makubaliano ya kukodisha timu, lakini
tangu Yanga wapewe eneo hilo hakuna kitu kikubwa walichokifanya.
Sarakasi hizi za Bunju na Geza ulole zinatosha kuonesha kuwa tunapenda
sana kuanza kwa moto tena maneno mengi yakiwa yametujaa midomo mwetu.
Midomo yetu hushindwa kuiamrisha miguu kupiga hatua za kusonga mbele,
ndiyo maana ni ngumu sisi kuwahi maendeleo makubwa kama wenzetu.
Kuna haja ya sisi kuacha kuongea sana na kukaa kwenye meza za
kibiashara na kuziendesha vilabu vyetu kibiashara.
Bunju Arena ingejengwa na shirika la nyumba la Taifa kwa makubaliano
ya kibiashara kama ya kuuita uwanja ule kwa jina la shirika la nyumba
ya Taifa kwa muda wa miaka ambayo itatumika kulitangaza jina la
shirika la nyumba la Taifa kupitia nembo ya Simba.
Hakuna biashara iliyofikia sehemu kubwa inayofanywa na mtu mmoja,
biashara zote hufanywa kwa ushirikiano wa wafanyabiashara wenye maono
ya kufikia biashara kubwa duniani.