in , ,

Gerardo Martino Kocha Mkuu Barcelona


*Tito Vilanova aanza kupambana na saratani
*Kifungo Nigeria, Cameroon sasa huru kisoka
*Higuain awapotezea Napoli kusubiri Arsenal

Mabingwa wa Hispania wamemteua Gerardo Martino ‘Tata’ kuwa kocha wao mkuu.
Tata, raia wa Argentina amekubali mkataba wa miaka mitatu Camp Nou, kuchukua nafasi ya Tito Vilanova anayekwenda kwenye matibabu, baada ya saratani ya koo kurudia tena.
Tata anachukua nafasi hiyo akiwa na benchi lake la kawaida la ufundi, wakiwamo wasaidizi Elvio Paolorroso na Jorge Pautasso. Haikujulikana mara moja hatima ya wasaidizi wa Vilanova, Jordi Roura na aliyeajiriwa hivi karibuni, Joan Francesc Ferrer Sicilia ’Rubí’.
‘Tata’ (50) alikubaliana na Barca mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kujulikana kwamba Vilanova angeachia ngazi na kufikia makubaliano Jumatatu hii asubuhi.
Anatarajiwa kuingia Barcelona Jumatano hii kwa ajili ya kutambulishwa rasmi, lakini hatarajiwi kuwaongoza Barca kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Bayern Munich wanaoongozwa na Pep Guardiola, mtangulizi wa Vilanova.
Kocha huyo alikuwa akitafutwa na klabu nyingine, Real Sociedad na Málaga, zote za Hispania. Alikuwa kocha wa Newels’ New Boys waliofika nusu fainali dhidi ya Atletico Mineiro katika Copa Libertadores, lakini walitolewa.
Barcelona walikuwa wametarajia kumchukua kiungo wake wa zamani aliyepata kuifundisha timu yao ya pili, Luis Enrique, lakini tayari alishasaini kwa ajili ya kuwafundisha Celta Vigo msimu ujao.
Mwingine ni Ernesto Valverde aliyekuwa huru Vilanova alipougua, lakini tayari amejiunga Athletic Bilbao, kwani ilitarajiwa Vilanova angerejea moja kwa moja.

VILANOVA AANZA MATIBABU

Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Barcelona, Tito Vilanova (44) anaanza awamu ya pili ya mapambano yake dhidi ya saratani ya tezi za koooni.
Ameandika barua inayoleta simanzi kwa wadau wa Barca na wadau wa soka kwa ujumla, akiwaaga watu wake na kusema kwa aina ya matibabu yanayomsubiri, hataweza kujitoa kwa klabu kwa asilimia 100.
Wachezaji nguli wa klabu hiyo, Lionel Messi na Andres Iniesta nao walipata nafasi ya kutoa salamu za heri kwa mwalimu wao aliyedumu kwa muda mfupi baada ya kumrithi Pep Guardiola mwishoni mwa msimu wa 2011/12.
Jose Mourinho aliyekuwa hasimu wake Real Madrid na sasa amehamia Chelsea, naye amemwandikia salamu za kumtakia heri kwenye ukurasa wa Twitter wa klabu yake mpya. Mourinho aliwahi kumrushia kidole machoni Vilanova wakati wa mechi baina ya miamba hao wawili wa Hispania.
Naye mtoto wa Vilanova mwenye umri wa miaka 15 ambaye yumo kwenye kikosi cha timu ya vijana cha Barca, Adria, aliandika pia akisema; “asanteni sana nyote kwa msaada wenu katika hili, mmekuwa wema sana, kila kitu kitakwenda sawa, kila la heri.”

KIFUNGO CHA MAISHA NIGERIA

Nigeria imechukua hatua kali ya kuwafungia maisha wachezaji na waamuzi waliohusika na upangaji matokeo wa klabu nne, ambazo mechi kati yao ziliisha kwa ushindi wa mabao 79-0 na 67-0.
Plateau United Feeders waliibuka na ushindi wa ajabu wa 79-0 dhidi ya Akurba FC huku Police Machine FC wakiwabomoa Bubayaro FC kwa mabao 67-0.
Klabu zote hizo hazitaruhusiwa kushiriki kwenye soka kwa miaka 10, ambapo kamati ya utendaji ya Chama cha Soka Nigeria (NFF) ilipendekeza waamuzi pia wafungiwe maisha.
Rekodi ya mabao mengi zaidi katika soka ni ile ya mwaka 1885, ambapo Arbroath waliwafunga Bon Accord nchini Scotland kwa mabao 36-0.
Mwaka 1995 Manchester United waliwatandika Ipswich Town mabao 9-0 , na ni rekodi ya aina yake kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).
Mwaka 2001 ulishuhudia Australia wakiwafunga American Samoa mabao 31-0 katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia.
Lakini mwaka 2002 AS Adema waliwafunga Stade Olympique L’Emyrne wa Madagascar mabao 149-0.

FIFA YAWAONDOA CAMEROON KIFUNGONI

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeondoa marufuku dhidi ya Cameroon, baada ya kuwa wamefungiwa kwa serikali kuingilia masuala ya Chama cha Soka.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuanza mchakato wa kusawazisha mambo kwa kamati maalumu kuanza kazi ya kuendesha shughuli za michezo nchini humo Jumatatu hii.
Kamati hiyo inaongozwa na Waziri wa Zamani wa Elimu na Michezo, Joseph Owona.
Kamati hiyo itafanya kazi chini ya uratibu wa Mjumbe wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Fifa, Primo Carvaro, hivyo wakifuzu, Cameroon wataruhusiwa kushiriki Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Kadhalika, klabu ya Coton Sport wataruhusiwa kuendelea kushiriki kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya kushindwa kuanza mechi katika kundi B.
Hatua hiyo inakuja baada ya ziara ya hivi karibuni ya Rais wa Fifa, Sepp Blatter aliyezungumza na ujumbe wa serikali, akiwamo Waziri wa Michezo, Adoum Garoua.

HIGUAIN AWASUBIRI ARSENAL

Hatima ya usajili wa mshambuliaji wa Real Madrid, Gonzalo Higuain, bado haijajulikana, baada ya kuomba muda kuamua iwapo atajiunga na Napoli ya Italia.
Klabu yake imekubali dau la pauni milioni 30 kutoka kwa klabu hiyo inayoongozwa na kocha Rafa Benitez, lakini Higuain ameonesha shaka na kuomba saa 48 afikirie.
Inachukuliwa kwamba amefanya hivyo ili kuwapa muda Arsenal wawasilishe dau jingine, kwani awali alikubaliana nao, lakini Madrid wakakataa dau la pauni milioni 25 walilokuwa wametoa.
Madrid pia walidai Higuain hauzwi, lakini wamekubali dau la Napoli, ingawa mpachika mabao huyo anapenda zaidi kwenda Arsenal. Madrid ghafla waliongeza dau kutoka pauni milioni 24 hadi milioni 32.
Wakimuuza mchezaji huyo, watakuwa wamepata fedha za kumpandia dau Luis Suarez wa Liverpool, anayewaniwa pia na Arsenal, na hilo litakuwa pigo kubwa kwa klabu hiyo ya kaskazini mwa London.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

TUMEJIANDAA KUIKABILI UGANDA- KIM

Arsenal wawatega Liverpool