in , , ,

Fiston Mayele ni pigo Ligi Kuu Tanzania

INGAWAJE haijatamkwa rasmi kuwa aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele ameuzwa kwenda klabu mpya ya Pyramids na Ligi nyingine ya Misri, lakini mashabiki wa timu hiyo wameshajiandaa na wanaelewa nyota huyo hatakuwa sehemu ya kikosi chao cha msimu 2023/2024. 

Baadhi ya mashabiki wasioamini tetesi za kuuzwa nyota huyo walingojea kwenye Siku ya Mwananchi kuona kama Fiston Mayele atakuwepo kikosini au la. Kama ilivyotabiriwa na wengi, nyota huyo hakuwepo sambamba na wachezaji wengine wawili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kiungo mkabaji Yannick Bangala na beki wa kupanda na kushuka, Djuma Shaban. 

Hakuna taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa Yanga juu ya wachezaji hawa watatu, lakini inaelekea wazi hawatakuwa kwenye kikosi cha Yanga msimu ujao. Hata hivyo wakati Yanga ikiwa inanufaika na biashara ya kumuuza nyota wake Fiston Mayele na kupata kitita kikubwa cha fedha, kwa upande mwingine ni pigo kubwa kwa soka la Tanzania. Fiston Mayele anaweza kutumi kama mfano wa nyota wengi wa kisasa barani Ulaya, ambako katika Ligi kubwa wanalipwa fedha nyingi ili wabakie kwenye vilabu vyao. 

Kwa mfano nyota wengi wakubwa kutoka Ligi nyingine wamekuwa wakimiminika katika timu za EPL. Leo  hii utaona matangazo mengi ya usajili wa nyota kutoka Ligi kama vile Italia, Ujerumani, Ufaransa, Hispania na kwingineko. Kila Ligi inataka kubakia na nyota wao ambao wanaleta mvuto wa aina fulani. nyota hao wanaongeza mapato kwa timu na Ligi kwa ujumla wake. Kwahiyo pale wanapohamaia timu za Ligi nyingine maana yake wanakuza thamani ya Ligi hizo wanazohamia. 

Wakati wa sakata la usajili wa Kylian Mbappe, ilibidi Rais wa Ufaransa, Emmanuel Maceon aingilie kati ili nyota huyo asihame PSG na kwenda Real Madrid. Rais wa Ufaransa alikaririwa kumwambia Mbappe kuwa yeye ndiye alama ya soka la Ufaransa kwenye ligi yao maarufu kama Ligue 1. Kwamba umaarufu wa Ligi hiyo na thamani unapokea mchango fulani kutoka kwa Mbappe anapokuwa PSG. 

Juhudi za kuhakikisha nyota huyo haondoki PSG zilifanikiwa miaka miwili iliyopita, ingawaje sasa hali imekuwa tete. Cristiano Ronaldo alipoondoka Manchester United alihamia klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia na kukuza umaarufu wa Ligi ya nchi hiyo Saudi Pro League. Kwa sasa nyota mbalimbali wanahamia Saudi Pro League na kuikuza thamani yake. 

Nguvu ya fedha za Waarabu zimeongeza mvuto kwa wachezaji, ambapo wengi wanaelekea kulipwa fedha nyingi. Makocha nao wameungana huko kuzinoa timu za Saudi Arabia. Steven Gerard na Robbie Fowler ni miongoni mwa nyota wa zamani wa Liverpool ambao wamepokea majukumu ya kufundisha timu za Saudi Arabia katika ngazi tofauti ya ligi. Hii maana yake ujio wa nyota hao unakuza ligi ya Saudi Arabia na kuongeza mvuto. 

Tukirudi katika Ligi Kuu Tanzania inaonesha wazi kuwa kuhamwa na mshambuliaji Fiston Mayele ni pigo kubwa. Inawezekana nyota wengi wamecheza Ligi Kuu na kuhama, lakini wote kwa nyataka tofauti walikuwa na mchango wao. Kuwa na nyota kama Patrick Ochan, Emmanuel Okwi,Calinhos, Khalid Aucho,Peter Banda, Cletous Chama,Tuisila Kisinda, Kevin muguna,Dejan,Yannick Bangala,Meddie Kagere,Amis Tambwe,Bruno Gomes, Michael Sarpong, Yacoba, na makocha kama  James Siang’a, Nasredine Nabi,Milutin Micho, Trot Moloto kwa nyakati tofauti inakuza na kuongeza thamani ya Ligi. 

Unapohamwa na mshambuliaji mahiri kama Fiston Mayele ni dhahiri unapoteza kitu muhimu chenye mchango wa maendeleo ya Ligi Kuu. Mayele hakufanya kila kitu peke yake, lakini huwezi kubeza mchango wake kwenye soka la Tanzania. Hii ina maana wengi wa makocha,mawakala na wataalamu watakuwa wanatupia macho kwenye Ligi ya Tanzania kuvuna vipaji, huku mastaa wakiwa wanalengwa zaidi. Unapoona nyota kama Mayele anaondoka kwa fedha nyingi bado inaleta pigo kwenye msisimko wa Ligi Kuu. 

Fiston alikuwa na ushangiliaji wake uliowavutia mashabiki wa soka wa kila rika hadi viongozi na kumfanya rais mstaafu Jakaya Kikwete kutumia staili ya ushangiliaji wake kwenye moja mikutano ya chama cha CCM. Kimsingi kuondokewa na Fiston Mayele ni pigo kwa msisimko wa Ligi Kuu. Kuchanua kwa Ligi Kuu kunahitaji nyota wenye mvuto ndiyo maana kwenye Ligi za Ulaya baadhi ya vilabu hukataa kuwauza nyota wao, huku viongozi wakitia maneno na fitina ili mastaa hao wasiuzwe kwenda kuongeza thamani Ligi nyingine. Lakini mpira wa miguu ni biashara ambayo Yanga hawawezi kuikwepa pale inapoleta manufaa makubwa kwao. Kwa upande wa msisimko Ligi Kuu inampoteza mchezaji muhimu. Labda tusibiri msimu mpya utakapoanza tuone msisimko ulioanza kwa nyota mpya Mahatse Makudubela ‘Skudu’ huenda ukaongeza mvuto na nyota huyo kuwa kivutio cha washabiki wengi nchini.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Cameroon, taifa lenye mafanikio kuzalisha makipa bora

Tanzania Sports

Ufalme wa Miquissone kurejeshwa tena Simba?