in , , , ,

FAIDA NA HASARA KWENYE BIASHARA YA MICHEZO ..

Mdhamini mkuu wa klabu ya Simba bwana Mohammed Dewji amekuwa mara kwa mara ananukuliwa kulalamika hadharani hususani kupitia kwenye kurasa za mitandao ya kijamii juu ya kwamba hapati faida katika kuiendesha klabu ya Simba na amekuwa anatishia mara kadha kwamba iko siku ataacha kuendesha klabu hiyo.

Hajawahi kutoa kauli hadharani inayoonyesha kwamba anapata faida na wala hajawahi kutoa kauli yenye kuonyesha kwamba kuendesha klabu kama ni biashara yenye faida kwa sana. Kuna wakati Simba haikupata matokeo mazuri akalalamika kwenye ukurasa zake za kijamii na ujumbe wake ulisambaa sana hadi kumfikia bilionea tajiri mmiliki wa klabu TP mazembe bwana Moise Katumbi naye akajitokeza na kutoa kauli hadharani kupitia kurasa zake za kijamii kwamba timu inapofungwa mmiliki hautakiwi kupagawa na kwenda kwenye mitandao ya kijamii bali unatakiwa kujikaza na kutafuta suluhisho la changamoto hiyo kwani ukipagawa mmiliki basi utawachanganya na kuwakatisha moyo mashabiki wa timu yako.

 Suala la kupata hasara kwenye uendeshwaji wa vilabu sio huyo tu peke yake ambaye amewahi kulalamika bali haya aliyekuwa mmiliki wa klabu ya Gwambina Football Club aliwahi kulalamika hadharani namna ilivyo ni ngumu kuendesha klabu ya soka katika mazingira yaliyopo. Na baada ya kulalamika aliamua kuvunja timu na kuvunja kambi ya klabu na hivyo kutokuendelea tena na klabu ambayo ilikuwa inafahamika kama Gwambina na kwa sasa klabu hiyo imebaki tu historia haipo tena.

Suala la kupata hasara katika uendeshaji wa vilabu ni jambo la kawaida hata barani ulaya vilabu vikubwa navyo vimekuwa vinalalamika sana kwamba havijiendeshi kwa faida sana na hali hii ilipelekea hata shirikisho la soka barani Ulaya kuanzisha kanuni za usimamizi wa kifedha(financial fair play) ili kuhakikisha vilabu havijiendeshi kwa hasara kubwa mara 3 mfululizo katika miaka ambayo inafuatana. Na kuna vilabu kadhaa barani ulaya ambavyo vimewahi kuadhibiwa kwa kukiuka kanuni hizo za mapato na matumizi.

Ulipotokea mtikisiko wa kiuchumi wa kiulimwengu wa septemba  ya mwaka 2008 wanauchumi wengi walikiri kwamba hali ya kuendesha vilabu baada ya mtikisiko ule utakuwa mzito kidogo.  Mtazamo huo ulipewa nguvu na kauli ya aliyekuwa raisi wa shirikisho la soka barani ulaya UEFA bwana Michel Platini ambaye alitamka hadharani kwamba nusu ya vilabu vya ulaya vilikuwa kwenye wakati mgumu kiedha kuweza kujiendesha. Na hiyo ilitokana na kwamba vilabu vingi vilitangaza kwamba vinajiendesha kwa hasara kubwa.

Hata baada ya kutokea kwa janga la kiulimwengu la ugonjwa wa Covid 19 vilabu vingi sana viliyumba kwa kiasi kwenye masuala ya mapato. Vilabu vikubwa viliongoza kuyumba kutokana na kuwa na madeni mengi makubwa ambayo baadhi yake yalionekana kama hayawezekani kulipika. Katika hali ya mshangao hakuna klabu hata moja kubwa barani ulaya ambayo ilikufa baada ya janga hilo na baadhi ya  vilabu vidogo ndivyo vilivyokufa. Kilichovifanya vilabu vikubwa viendelee kuwepo mpaka hii leo na vilabu vidogo kufariki ni kutokana na kwamba vilabu vikubwa vimetengeneza nembo(brand) kubwa za biashara na hufanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba nembo zao za biashara hazifi na hili ndilo linalovifanya viendeleee kuwepo.

Vilabu kama Real Madrid, Manchester United vimejenga nembo zao kwa miaka mingi kwa kushinda mataji makubwa na hili ilivipelekea vilabu hivi kuwa na mashabiki wengi sana wakubwa na hatimaye kuvifanya vifanye biashara nzuri sokoni.

Msingi mkubwa wa mafanikio wa biashara ya vilabu vya soka ni matumizi ya klabu katika soko la wachezaji. Kwa msingi huu vilabu vikubwa barani ulaya vimekuwa vinatumia gharama kubwa kusajili wachezaji wenye majina makubwa kwa ajili ya malengo ya kuhakikisha wanawafanya mashabiki wao waendelee kushabikia vilabu hivyo na hao wachezaji wawapatie mafanikio ya kubeba mataji mengi iwezekanavyo.

Na hali hii imevifanya vilabu hivyo viendelee kuwa kwenye madeni makubwa kwani kwenye usajili wa wachezaji wakubwa wamekuwa wanakopa madeni makubwa ili kuhakikisha linafanikiwa hilo. Madeni ya klabu kubwa yamekuwa yanaongezeka kila uchao lakini mapato ya vilabu hivyo yamekuwa yanakuwa pia.

Vilabu hukopa hela kutoka kwenye mabenki na mda mwingine hukopa hela kutoka kwa wamiliki wa vilabu hivyo ambao huingiza hela ambapo hutarajia kulipwa hela hizo baada ya mda Fulani. Maendeleo ya mitandao ya kijamii yamesaidia vilabu kuweza kujua kiwango cha mashabiki ambao vilabu wanao kutokana na namna mashabiki wao wanavyochangia mijadala katika mitandao hiyo. Mikataba ya haki za kurusha matangazo(broadcasting rights) yamevifanya vilabu vingi sana vikubwa viweze kuendelea kukusanya mapato mengi sana kwani kwa kuendelea kusaini wachezaji wenye majina makubwa kumewafanya wawe na mvuto kwa mashabiki wa maeneo tofauti duniani  na hiyo kupelekea vituo vya kurushia matangazo(broadcasters kulipa gharama kubwa sana za fedha ili kuweza kurusha matangazo ya mechi zao. Mnamo mwaka 2014 klabu ya Real Madrid ilibeba ukombe wa klabu bingwa ulaya na ivyo kuifanya kuwa ni klabu iliyobeba kombe hilo mara nyingi Zaidi na kuifanya kuingiza mapato mengi sana ndani ya huo mwaka.

Wachambuzi wa masuala ya fedha za michezo wanasema kwamba kiwango ambacho klabu hiyo ilikipata ndani ya mwaka huo hakuna klabu ambayo iliwahi kutengeneza kiasi cha fedha kama hicho katika historia ya michezo duniani.

Ni dhahiri kwamba mwekezaji kama Mohammed Dewji hataachana na klabu kama Simba licha kwamba inaonyesha kumpa hasara Fulani ya kipesa kwa mujibu wa baadhi ya kauli zake ila uhalisia mtaji wa mashabiki ambao klabu hiyo inao ndio unaomfanya aendelee kusalia katika klabu hiyo na ndio maana vilabu kadhaa alivyowahi kuvimiliki huko nyuma kama African Lyon aliviuza lakini hiyo ameendelea kukaa nayo. Anachotakiwa kufanya ni kuweka mkakati ambao utafanya nembo ya klabu hiyo kutoshuka katika soko na kuwekeza kwenye majina makubwa ambayo yataleta matokeo yatakaoifanya klabu hiyo iendelee kung’ara barani Afrika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

33 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

JIPYA GANI KEN GOLD ITAKUJA NALO LIGI KUU?

Tanzania Sports

PAMBA INAWEZA IKAWA NI LEICESTER CITY YA BONGO?