in

EPL bila udambwidambwi itawezekana kweli?

Ligi kuu England

JUNI 17 kidumbwendumbwe cha Ligi Kuu England kitarejea kayika viwanja mbalimbali. Ni ligi inayofuatiliwa zaidi nchini Tanzania. Ni ligi inayowapa watu mlo. Wapo wanaotegemea ligi hiyo kujipatia chakula kizuri mezani kupitia kampuni za kubashiri. Wapo wanaopata fedha kupitia kumbi mbalimbali znazoonesha mechi moja kwa moja. Wapo wanaotanua na kujigamba mitaani kwa fedha za EPL. 

Hivyo ni ligi inayowapa burudani,furaha na utemi wa kiuchumi. Hivyo wengi hutamani kuona matokeo ya mapenzi yao kwa EPL yanakuwa na tija kila uchwao.

Kwa mashabiki wa Ligi ya England wamezoea kuona shamrashamra viwanjani. Kuna wanywaji wa bia. Kuna wanaopenda timbwili vitini. Wale wanaopenda full shangwe tangu ya dakika ya kwanza hadi ya mwisho. 

Kuna manjonjo na madoido. Kuna kebehi na majigambo. Kuna zomea zomea na amsha amsha kama zote. Mashabiki hupenda kuwatia nguvu wachezaji. Wapo wanaozomea wachezaji wao au timu pinzani. Ari ya uchezaji huchochea mabao matamu tunayoona viwanjani. 

KUFULI YA KORONA

Hata hivyo lipo tushio linalowafukuza mashabiki viwanjani. Mechi nyingi za EPL zitachezwa bila mashabiki viwanjani. Wachezaji watakosa ari ya ziada kutoka maukwaani. Mashabiki watakosa amsha amsha za wachezaji wao kutoka viwanjani. 

Mbwembwe za mashabiki zimepigwa kufuli kwa hofu ya kuenea virusi vya Korona. Baa zitakuwa zimefungwa. Mashabiki hawatakuwa na fursa ya kupata mzuka kupitia kilaji. 

Hekaheka za uwanjani kati ya mashabiki wa timu mbili hazitakuwpeo. Viwanja vitakuwa vitupu kama mwanadamu anapobadili viwalo ama akiwa bafuni. Maduka ya kubashiri yatafungwa wakati wote hadi ligi imalizike. 

MTIHANI BILA PESA

Ni wazi mashabiki wapo kwenye mitihani. Makocha wapo kwenye mitihani. Wachezaji wapo kwenye mitihani. Ingawa wote watakaokuwapo uwanjani yaani wachezaji,makocha na maofisa wao watakuwa wamepimwa lakini ule ugwadu wa soka bila shaka utakuwa umepungua. 

Mtihani utakuwa kwa pande zote kuhakikisha hazipati maambukizi ya virusi hivyo hata kama watakuwa wamepimwa na kuthibitishwa hawana korona.

Tanzania Sports
Uwanja wa Emirates ukiwa umefura..

Korona imeleta mtihani huu kwa mashabiki. Mtihani kwa wachezaji na makocha wao pamoja na viongozi. Mitihani kwa shirikisho la soka na wamiliki ambao watakuwa wameathiriwa kutokana na kupungua vipato. Vipato vya timu mbalimbali vitakuwa vimepungua kiasi kwamba mtihani wa kulipa mishahara utazikumba timu nyingi.

Wachezaji wakiwa na hofu ya korona, kisha waingie viwanjani wakiwa na mawazo ya kupunguziwa mishahara ni mtihani. Utakuwa mtihani mwingine pia wachezaji hawatajua hatima zao kama wanabaki au wanaondoka. 

Je, ikiwa wachezaji hawatakiwi kukabana kwa nguvu ama wapunguze migusano bila shaka itashuhudia viwango vibovu vya soka. 

Hapo ndipo mtihani unazidi, huku pesa ikizidi kuzipiga chenga timu mbalimbali. Ni nani anapenda kucheza kwenye viwanja vitupu? Ni mchezaji gani hapendi kutiwa moyo na mashabiki wa timu yake? Ni mchezaji hapendi jina lake kuimbwa viwanjani? Ama wote watakuwa kama Mesuit Ozil ambaye kwake yupo yupo hajulikani anapenda au hapendi. Lakini huu mtihani ni wa wote, nani atavumilia zaidi? 

Nani atavumilia kuketi kwenye masofa nyumbani kutazama mpira? Bila shaka ni michosho tu. Watu watakuwa wameboreka mno, na pengine ghadhabu au kushuhudia malalamiko na kuwaomba wahusika wa soka kuangalia namna nzuri ya kuwaruhusu mashabiki inaweza kujitokeza.

TIKETI ZA MSIMU

Wapo mashabiki waliolipia tiketi zao za msimu mzima. Ama wale waliolipia mechi nyingi zaidi na wakajikuta wanazikosa sababu ya Korona, hivi leo wataelewa kweli wanapoambiwa wasiingie viwanjani? Machozi yao nani atayafuta katika kipindi hiki? 

Pesa imekwenda au klabu zitarudisha? Kama zitarudisha vipi hali zao kiuchumi kwa kuendesha shughuli za vilabu? Bila shaka ni mtihani mwingine kwa waendeshaji wa soka na vilabu vyao. Mtihani kwa mashabiki kukubali kuwa pesa zao hazikutumika kama walivyotaka.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Sifa ya kikosi bora Simba,Yanga na Azam

Sifa ya kikosi bora Simba,Yanga na Azam

Tanzania Sports

Tanzania na utumiaji wa viwanja vya michezo