*Arsenal nafuu kidogo, Chelsea chali


*Man U bado, Mourinho afoka tena

Ligi Kuu ya England (EPL) wikiendi hii imeingia raundi ya 30 kwa baadhi ya timu, huku matokeo yakibadilikia kadhaa.

Wakati vinara Chelsea walichapwa na Crystal Palace, tena wakicheza nyumbani kwao Stamford Bridge, Arsenal wameonesha kupata nafuu kwa kwenda sare ya 2-2 na Manchester City.

Chelsea, hata hivyo, bado wapo juu kwa tofauti ya pointi saba, kwani katika mechi 29 wamefikisha pointi 69 wakifuatiwa na Tottenham Hotspur wenye 62 kwa idadi hiyo hiyo ya mechi.

Kocha wa Chelsea, Antonio Conte alisema kufungwa kwao kunaifanya EPL kuwa tamu na yenye ushindani zaidi, akawaonya wachezaji wake kwamba bado wana kazi kubwa mbele, ikiwa wanataka kutwaa ubingwa wa England.

Akiwa kwenye msimu wake wa kwanza England akitoka Italia, Conte amekumbwa na changamoto kwenye mfumo wa ulinzi, ambapo mabeki walielekea kuchanganyana kwenye mechi ya juzi. Aliubadilisha mfumo huo tangu walipofungwa na Arsenal 3-0 na kuanzia hapo wakaenda bila kufungwa mechi 13 mfululizo.

ARSENAL NAFUU, SARE NA CITY

Arsenal wakicheza nyumbani Jumapili hii huku kukiwa na shinikizo kwa kocha Arsene Wenger kujiuzulu, walianza kufungwa mapema dakika ya tano, kwa bao la Leroy Sane kabla ya Theo Walcott kusawazisha kabla ya mapumziko, lakini dakika mbili tu baadaye Serguo Aguero akwarejesha mbele City.

Arsenal waliendeleza jitihada zao za kukataa kufungwa hapo na alikuwa beki wa kati, Shkrodan Mustafi aliyesawazisha mambo dakika ya 53 kwa kuruka juu na kuupata mpira wa kona. Ilikuwa mechi nzuri na yenye ushindani. City wamepata kuwafunga Arsenal hapo Emirates mara moja tu katika mechi 20.

Kocha Guardiola alitabiri upinzani mkali, akisema ni bora kucheza na Arsenal waliotoka kushinda hata mechi nyingi kuliko kukabiliana nao wakiwa na majeraha ya kufungwa.

Katika mechi tano zilizopita, Arsenal walikuwa wamepoteza nne, hivyo washabiki kutaka Wenger asipewa mkataba mpya baada ya alio nao kumalizika kiangazi hiki. Hata hivyo, wakuu wa Arsenal wameshampa mkataba wa miaka miwili ambao hajaamua kuusaini au la, akisema ataamua hivi karibuni.

Wenger amewapongeza washabiki kwa moyo wanaoonesha kuipenda klabu yao, lakini alipata kusema awali kwamba hata akiondoka si kwamba watashinda mechi zote, na kwamba amefanya mengi kwa klabu na mawazo yake yote yapo Arsenal. Juzi alisema kwamba mawazo ya kustaafu kwa watu wa umri wake ‘yanakufa’ sasa, akionesha kwamba bado atakuwapo.

Katika mechi nyingine Jumapili hii, Swansea waliowakaribisha Middlesbrough walikwenda nao suluhu.

MANCHESTER BREKI, MOURINHO ALIA NA SHAW

Manchester United walikwenda suluhu na West Bromwich Albion kwenye mechi iliyofanyika Old Trafford, ambapo Kocha Jose Mourinho alionekana kutokuwa na raha, akadai kwamba hapakuwapo uwiano mzuri kwenye mechi hiyo.

Katika hatua nyingine, ametoa ishara kwamba ataondokana na beki wake, Luke Shaw, ambaye amecheza mechi chache msimu huu, akihoji juu ya kujituma kwake na tabia yake mazoezini, akidai hawezi kumfananisha na wengine kama Daley Blind.

Alikuwa akijibu swali la mwana habari aliyetaka kujua iwapo mchezaji huyo wa kimataifa wa England hangeweza kutumiwa zaidi kwenye kikosi chake na kuleta matokeo mazuri. Alihitimisha majibu yake kwa kusema “Joe Hart (wa Manchester United) ni mchezaji wa kimataifa wa England lakini anacheza kwa mkopo Italia (Torino).

MATOKEO MENGINE EPL WIKIENDI HII

Katika mechi nyingine, Liverpool wakicheza nyumbani Anfield walifanikiwa kuwakung’uta watani wao wa jadi wa Merseyside, Everton, kwa mabao 3-1, Burnley wakakwamia nyumbani kwao kwa kupigwa 2-0 na Spurs na Hull wakawakandamiza West Ham 2-1.

Mabingwa watetezi ambao wameshindwa kufanya kama msimu uliopita, Leicester, waliwapiga Stoke 2-0, Watford wakazidi kuwapeleka Sunderland eneo la kushuka daraja kwa kuwafunga 1-0 huku Southampton na Bournemouth wakitoshana nguvu pasi na kufungana.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Wachezaji wa kuchungwa Azam vs Yanga

Tanzania Sports

NILICHOKIONA KWENYE BAADHI YA MECHI ZA EPL WIKI ILIYOPITA