in , , , ,

Clement Turpin ni refa wa aina yake

MZIGO mzito wa Ligi Kuu Tanzania mpe Ahmed Aragija. Ahmed Aragija ni jina kubwa katika kazi ya urefa kwenye Ligi Kuu Tanzania akiwa amechezesha mechi nyingi na wakati mwingine anapofanya uamuzi unabaki unashangaa, kwa sababu unamkuta anatabasamu au kumchekea mchezaji bila ule ukali ambao unawafanya wachezaji wamwogope. Ukigeukia Ulaya, hasa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa, Clement Turpin ni miongoni mwa marefu ambao wanasisimua kila wanaposhika filimbi kuchezesha mechi mbalimbali. 

Ingawaje yeye ni binadamu, lakini kuna jambo ambalo analifanya na linawafundisha waamuzi wetu wa Tanzania. Kihistoria, Clement Turpin kila akichezesha mechi za Real Madrid, mara nyingi huwa wanashinda, na mchezo dhidi ya Man City ulikuwa  wa nane kushinda. Lakini nini hasa kinachomfanya Clement Turpin kuwa mahiri na kuchaguliwa mara kwa mara kucheza mechi ngumu na zenye ushindani mkubwa pamoja na kuwa gumzo zaidi duniani? TANZANIASPORTS inamchambua mwamuzi huyo na hulka zake awapo uwanjani.

Tabia za wachezaji

“kabla ya fainali ya Kombe la Dunia, niliwatazama wachezaji wa Brazil na Ujerumani. Nilisoma tabia zao wanapocheza, wnaavyozungumza na mwamuzi. Niliwajua kwa majina hasa Brazil na hulka zao. Kwahiyo kila aliyenijia nilielewa ni nani na ana tabia gani.” Hii ni kauli ya mwamuzi bora kuwahi kutokea duniani, Piereluigi Collina raia wa Italia. Kauli hiyo alitoa wakati akizungumzia mchezo wa Fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002 uliochezwa huko Tokyo nchini Japan. 

Collina anasifika kwa umakini, ukali, tabasamu na kufuatilia mchezo wote kila hatua. Kwa sasa ndiye mmoja wa mabosi wa marefa kupitia FIFA. Ukiangalia uchezeshaji wa Clement Turpin unaonesha ni mtu ambaye anazifahamu hila na tabia za wachezaji kiwanjani. 

Uwezo wake wa kuwamudu katika ubinafsi wao na hasiti kuwaelewesha kila wkaati anapochukua uamuzi. 

Jinsi anavyozungumza na wachezaji uwanjani ni jambo lingine linalovutia kumwona akicheza mechi, siri kubwa ya refa ni kuzijua tabia za wachezaji mbali ya sheria 17 za soka. Collina alizisoma hulka za Wabrazil na majina yao. lakini Turpin anaonekana kuwasoma wachezaji wote, kuanzia ujanja wao wa kumhadaa mwamuzi na kushawishi maamuzi fulani. Ule utulivu wake anapokabiliana na wachezaji au mechi kubwa ni somo lingine ambalo marefa wanatakiwa kuchukua.

Utawala na kujiamini

Kuna wakati nilidhani Mark Clettenburg angefikia daraja la Piereluigi Collina. Lakini haikutokea hadi alipondoka EPL na kwenda Arabuni. Ukitazama mwenndo wa Clement Turpin akiwa dimbani anaonesha ni mtawala asiye na mashaka. Ni bosi ambaye anatawala mchezo, anaongoza, anasimamia, anaelekeza na kuamuru kila hatua inayotakiwa na halali. Kasi yake inavutia na anakuwa karibu na matukio muhyimu ambayo yanaweza kuzua utata. 

Clement Turpin ana macho makali kuona makosa na kufuta utegemezi wa VAR ingawaje kwenye tukio la penati dhidi ya Real Madrid alitumia takribani dakika 4 kusikiliza wasaidizi wake wanasema nini. Bila kutegemea VAR, Turpin aliona makosa yaliyofanywa na Dani Caballos hivyo alipoamuru adhabu ya penati alikuwa sahihi na VAR ilimhakikishia hilo. Uwezo wake kujiamini ndiyo unaomfanya awe mwamuzi bora wa UEFA. Uamuzi wa shirikisho la soka kumkabidhi mechi kubwa na zenye presha nyingi unamaanisha uwezo wake ni wa hali juu. kuwatawala wachezaji 22 wanaocheza mpira pamoja na mabenchi yao ya ufundi, kisha mamilioni ya watu duniani wkaimwangalia yeye, inahitajika mtu mwenye utulivu. Amechezesha fainali nyingi za UEFA pamoja na kuchezesha mashindano ya EURO.

Heshima za Turpin kama Collina

Kama unaweza kufananisha basi Turpin ungemfananisha na Collina. Haiba zao za utawala ndizo zinawafanya wawe tofauti na wengine. Wanapokuwa uwanjani ni kama wazazi wanalea watoto wao. Utawala wa Turpin uko wazi na mara nyingi hawezi kuwakimbia wachezaji pale wanapoleta shinikizo fulani. Huyu ni mwamuzi ambaye anapendwa na wachezaji, makocha, na viongozi wengi kwa sababu anawaheshimu na anaenenda tabia za Collina. Wachezaji wanapomkaribia hasa kulalamikia matukio yenye utata, wanakwenda kwa nidhamu na wanaonenkana wazi wanamheshimu mwamuzi huyu. Katika maizngira hayo hata mwamuzi mwenyewe anavyozungumza na wachezaji au makocha anaonekana kutoa heshima kubwa na kuwaheshimu kwa kazi zao. Hii ni hulka mojawapo ya Collina.

Mzigo mzito mpe Turpin

Ukiondoa mechi ngumu ya Manchester City dhidi ya Real Madrid, rekodi zinaonesha kuwa shirikisho la soka la UEFA huwa linamkabidhi mechi zenye hekaheka zaidi. Refa huyo alikabidhiwa mechi ngumu kama vile fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Liverpool na Real Madrid mwaka 2022 iliyochezwa nyumbani kwao Ufaransa katika dimba la Stade De France. Man City dhidi ya Juventus, mechi hiyo ilikuwa chini ya refa huyu ambapo Kibibi kizee cha Turin kilishinda mabao 2-0. Hizo zilikuwa mechi ngumu sana msimu huu lakini zimesimamiwa kirahisi na utawala wa Turpin umeonekana dhahiri.

Ni nani huyu Turpin?

Clement Turpin alizaliwa mwaka 1983 kwa mujibu wa UEFA. Turpin aliteuliwa kuwa mwamuzi wa FIFA tangu mwaka 2010 na UEFA mwaka  2012. Alichezesha mechi za Kombe la dunia katika hatua ya robo fainali mwaka 2014. Mwaka 2016 alichaguliwa kuwa refa bora wa Ligi ya Ufaransa. Mwaka huo huo pia alichaguliwa kuchezesha michezo ya mashindano ya Olimpiki nchini Brazil. Mwaka 2017 alichezesha mchezo wa fainali ya Kombe la dunia chini ya miaka 17 huko nchini India. Mwaka 2018 alichezesha mechi ya kombe la Dunia. Mwaka 2021 alichezesha fainali ya Europa League kati ya Vilarreal na Manchester United. Turpin alichaguliwa na UEFA kuchezesha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2022 kati ya Liverpool na Real Madrid. Mwaka 2024 alichezesha fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya nchini Ujerumani kati ya England na Hispania.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Jinsi Manchester City wanavyoharibu mechi yao

Tanzania Sports

Jude Bellingham amejibu kwanini yupo Real Madrid